Monday, June 4, 2012

CHADEMA WATOA ONYO KWA MWEKEZAJI



Dr. Wilbroad Silaa akiwa katika moja ya mikutano yake kuwahutubia wananchi







CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya kimetoa onyo kali kwa mwekezaji wa shamba la Mbarali Estate lililopo katika Wilaya hiyo kwa madai ya kutumia shamba hilo kisiasa.


Tamko hilo limetolewa na mwenyekiti wa CHADEMA wilaya ya Mbarali Bw. Peter Mwashiti katika viwanja vya mikutano Kata ya Ubaruku wakati wa mkutano wa chama hicho na kuwa mwekezaji huyo anatumia vibaya shamba hilo la serikali ambalo ni mali ya wananchi wote, kwa kuigawa jamii ya Taifa.

Bw. Mwashiti amesema mwekezaji huyo amekuwa akiwanyang’anya mashamba wananchi wanaolima katika shamba hilo baada ya kugundua hawana itikadi ya chama anachokitaka yeye hatua ambayo inaweza kuleta madhara endapo serikali haitaingilia kati ubaguzi huo, kwani tabia hiyo inawanyima fulsa ya kuendesha shughuli za kilimo wananchi wanaoshabikia vyama vya upinzani.

Diwani wa Kata ya Ubaruku Mh. George Mbilla wa CHADEMA amesema hata yeye  alinyang’anywa ekari 19.7 ambazo alikuwa tayari alikuwa amelipia shilingi Milioni 3, na hatua hiyo ilikuja mara tu baada ya kutangaza nia ya kugombea kupitia CHADEMA.


Ofisa mahusiano wa shamba hilo la Mbarali Estate Bw. Ignas Mgao
alikataa kufanya mahojiano yoyote na mwandishi wa habari, kwa madai yeye yupo kazini na hana muda wa kuzungumzia uzushi wa wananchi hao.


CHADEMA kinataraji kufanya mkutano katika viwanja hivyo vya Ubaruku siku ya jumapili, kwa lengo la kupinga tabia hiyo na kutoa tamko juu ya madai mbalimbali yanayotokea katika Wilaya hiyo, mkutano unaodaiwa kuhudhuliwa na viongozi wa ngazi za juu.
                                                   

No comments:

Post a Comment