Thursday, May 5, 2011

Wafanyakazi 540 wa mgololo wadai malipo yao ya miaka 6

LICHA ya wafanyakazi kuadhimisha siku ya wafanyakazi duniani mei mos- kila mwaka, wafanyakazi 540 wa kiwanda cha karatasi Mgololo Paper Mills (MPM) kilichopo Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wamelalamikia kutolipwa madai yao kwa zaidi ya miaka sita.

Wakizungumzia tatizo hilo kijijini hapo wafanyakazi hao walisema kutolipwa mishahara yao kumesababisha wao kuwa na hali ngumu pamoja na watoto wao kushindwa kwenda shule.


Juliana Haule mmoja wa wafanyakazi wa iliyokuwa Southern Paper Mills (SPM) alisema serikali kabla ya kubinafsisha kiwanda hicho cha SPM wao walikabidhiwa kwa mwekezaji kama wafanyakazi wa kiwanda kipya cha MPM na mwekezaji kukubali kulipa madai yao.


Magnus Mlelwa na Patric Mpolwa walisema kutolipwa fedha zao kwa kipindi kirefu cha mika 6 kunasababisha kuishi maisha magumu huku watoto wao wakishindwa kwenda shule kutokana na kukosekana kwa fedha za kulipa ada.

“Unajua idadi ya watu 540 wenye hali ngumu ni mara tatu kwani wake zetu na watoto wote hatuna maisha bora, na serikali ijue kuwa hii ni athari kubwa kwani kundi kubwa kama hilo ambalo halina kazi kwa serikali ni hasara na pia hakuna kitu tunachokifanya, hatufanyi shughuli zozote za kiuchumi na kuwa mzigo kwa Taifa,” Walisema.

Walisema hata hali ya uchuma katika Bonde la Mgololo ni duni kutokana na kundi kubwa kutokuwa na shughuli zozote, kwani hata baadhi ya michango ya maendeleo kama ya ujenzi wa shule wanashindwa kuchangia kwa kukosa fedha.

John Mlasu alisema serikali kutowasaidia kupata haki zao ni sawa na familia isiyo na mzazi kwani baadhi ya viongozi ndiyo wanachangia kuichafua serikali, na kuwa hali hiyo ni sawa na maafa kwani hata fedha za matibabu hukosa na wakijikuta wakipoteza maisha kila siku.


Mark Chambuso katibu wa ufuatiliaji wa malipo ya wafanyakazi hao alisema kukosekana kwa haki ya malipo hayo kutazaa idadi kubwa wananchi wanaoichukia serikali pamoja na kuwepo kwa watoto wasiopatiawa fulsa ya kwenda shule na hivyo baadaye serikali kuwa na kundi kubwa la wananchi wasio na kazi kutokana na kukosa elimu.

Walisema serikali inatakiwa kutenda haki juu yao kwa kulipa madai yao ambayo wamekuwa wakifuatilia kwa muda mrefu bila mafanikio.

“Bajeti ya malipo ya wafanyakazi wa kiwanda cha mgololo tunajua ilikuwepo, lakini ilichakachuliwa na viongozi wachache wasioitakia mema serikali, tunaitaka serikali kama inataka kurudisha imani kwetu na vizazi vyetu itulipe haki zetu jamani,” Walisema.

Jailosi Mtonyole alisema maisha magumu wanayoishi yamesababisha kundi kubwa la watoto wa kike kupata mimba kwa kukosa fulsa ya kusoma na hivyo kuwa watoto wa mitaani kutokana na jamii kuwachukulia ni watu wazima kutokana na hali ngumu ya maisha wanayoishi.

“Watoto wetu wameathil;ika zaidi kwani wanarubuniwa kwa vitu vidogo na kufanyiwa unyama, mimi watoto wangu nimeshindwa kuwapeleka shule na wote wapo nyumbani wanamimba,” Alisema Mtonyole.

Walisema hata hali ya kunyonywa juu ya haki hiyo ni moja ya magamba makubwa yaliyopo ndani ya serikali ambapo kama kweli Chama tawala kina nia ya kusafisha maovu yaliyotendwa na baadhi ya viongozi wenzao hata kunyimwa haki nao wanatakiwa kujivua magamba ili kuleta imani dhidi yao.


Mwenyekiti wa ufuatiliaji wa mafao ya wafanyakazi hao John Njalamoto alikili kuwepo kwa matatizo hayo katika chama cha wafanyakazi wa kiwanda hicho cha Mgololo na kuwa bado wanaendelea kufutilia malipo ya fedha za wafanyakazi hao.


Meneja wa kiwanda aliyefahamika kwa jina la Chogo hakupatikana kiwandani hapo na alipotafutwa kwa njia ya simu alisema yupo rikizo na atakaporejea kazini atatolea ufafanuzi wa tatizo hilo.

Mwisho

No comments:

Post a Comment