Wednesday, January 4, 2012

WAMTAKA WAZIRI KUINGILIA KATI SHULE YA MGUHU


WANANCHI wa kijiji cha Nyabula kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa wamemtaka waziri wa elimu Shukuru Kawambwa kuingilia kati hali halisi ya shule ya msingi mguhu ambayo baadhi ya wanafunzi hulazimika kusomea katika uzio wa nyasi na walimu kukaa katika kibanda cha nyasi kama ofisi kutokana na shule kuwa na vyumba viliwi pekee vya madarasa huku walimu wakiwa hawana huduma muhimu ya choo.


Wakizungumza katika mkutano wa hadhara nje ya ofisi ya serikali ya kijiji cha Nyabula wananchi hao walisema mazingira mabovu yaliyopo katika shule ya msingi Mguhu  yanachangia kwa asilimia kubwa na baadhi ya viongozi ambao wamekuwa wakipotosha matumizi ya michongo hiyo.

Walisema ili kutendewa haki juu ya fedha zao ambazo huchangishwa kila mwaka ikiwemo michango ya nguvu kazi wanamtaka waziri wa elimu kuingilia kati suala hilo ambalo viongozi wamekuwa wakipotosha ukweli wa shule hii huku hali halisi ikionekana.

“Sasa wamewakataza walimu kukaa katika kibanda kile cha nyasi ambacho walikuwa wanakitumia kama ofisi pamoja na kujikinga na jua, eti waandishi wasije wakawakuta hapo, mimi nasema hili si suluhisho la tatizo la shule, kinachotakiwa ziletwe hela na vifaa shule ijengwe, hali hii inawadhalilisha sana walimu kwani hawana hata choo, wanajisaidia polini, hii ni hatari sana, sijui elimu yetu tunaipeleka wapi!!”, Alisema.

Onesmo Magubika alisema fedha nyingi zilzochangwa haziendani na majengo yaliyopo na hivyo kupoteza hamasa ya kuendelea kuchangia ujenzi huo, ambapo hadi sasa walimu hawana ofisi, choo na hata baadhi ya wanafunzi kutokana na idadi kubwa iliyipo kulazimika usomea katika uzio wa nyasi, mbinu iliyobuniwa na walimu ili kuwasaidia wanafunzi kuendana na vipindi vya masomo.

Damian Ng’asi alisema wananchi wamekuwa wakifanya kazi za maendeleo ambapo kila mmoja  mmoja hufyatua tofari 300, kubonda Kokoto, kusomba mawe  pamoja na mchango wa fedha wa shilingi elfu 1500 yote ikiwa ni mchango wa ujenzi wa shule ya msingi Mguhu.

Ng’asi alisema shule hiyo ilianza kujengwa tangu mwaka 1999 mpaka sasa ina vyumba viwili pekee vya madarasa, huku likiwemo jengo ambalo halijaisha na hivyo kuwepo kwa mazingira magumu ya ufundishwaji na ufundishaji wa wanafunzi.

“Hivi miaka yote hiyo kila mwaka tunachangia ujenzi wa shule ya Mguhu lakini hali ipo pale pale, baadhi ya wanafunzi wanalazimika kusomea katika uzio wa nyasi kutokana na uchache wa vyumba vya madarasa, hii ni aibu sana hata kwetu wananchi wakati tunakamuliwa michango,” Alisema Ng’asi

Bonus Fivao mwenyekiti mstaafu wa kijiji cha Nyabula alisema mazingira ya shule hiyo yanakatisha tama kwa wananchi, walimu na wanafunzi kwa kuwa shule hiyo haina huduma muhimu ya vyoo vya Walimu, haina ofisi pamoja na  nyumba za walimu.

“Kuna kiti tulianza kujenga tangu mwaka 2000 lakini mpaka sasa hakuna maendeleo yoyote, kimebaki kama kilivyo, viongozi hawatusomei mapato na matumizi ya michango yetu, hali hii inavunja nguvu ya wananchi kuendelea kuchangia, ni aibu sana wanafunzi kusomea katika uzio wa nyasi na walimu kutumia kibanda cha nyasi kama ofisi, walimu wanalazimika kutumia mbinu hizo ili kuwasaidia wanafunzi kupata vipindi vya masomo, hapa tunaiomba Halmashauri ya wilaya, pamoja na mbunge wetu atusaidie ujenzi,” Alisema.

Aidha wananchi walisema kusuasua kwa ujenzi wa shule hiyo kunatokana na baadhi ya viongozi kuwa na maslahi binafsi na hata kuwepo kwa ubadhilifu wa fedha kwani majengo hayo yalilazimika kubomolewa kutokana na kujengwa chini ya kiwango kisichokubaliwa na ramani inayotakiwa katika Halmashauri.

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Nyabula Robart Balama alikili kuwepo kwa hali hiyo ya wanafunzi kusomea katika uzio wa nyasi huku walimu wakijibanza katika kibanda cha nyasi kutokana na kutotoshereza kwa vyumba vya madarasa kwani shule ina zaidi ya wanafunzi 200 huku madarasa yakiwa mawili pekee.

Afisa elimu wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa  Kabiru  Mbawala alisema shule hiyo ni mkondo “B” na ujenzi wake ulitokana na kuwepo kwa  idadi kubwa ya wanafunzi wa shule ya Nyabula  ndipo wananchi waliamua kuanzisha shule hiyo na mpaka sasa ilitakiwa kuwa na vyumba angalau vitano na siyo viwili kama ilivyo sasa.                                                                                                                                                                                                                                                                                    
Naye afisa elimu wa mkoa wa Iringa Joseph Mnyikambi alisema mazingira ya shule hiyo yataboreshwa ili kuendana na utoaji wa elimu shuleni hapo.

Hata hivyo ofisi ya mkuu wa mkoa kupitia afisa habari wake Denis Gondwe alisema mkoa utatoa tamko juu ya shule hiyo ambayo inakabiliwa na changamoto mbalimbali.

MWISHO

No comments:

Post a Comment