Thursday, February 20, 2014

CCM WABEZA PINGAMIZI LA CHADEMA

 Mgombea wa chama cha demokrasia na maendeleo CHADEMA Bi. Grace Tendega akiwa na mratibu wa CHADEMA nyanda za juu kusini Bw. Frenk Mwaisumbe katika ofisi ya CHADEMA Iringa wakipitia baadhi ya viambatanishi vya Pingamizi la mgombea wa CCM Bw. Godfrey Mgimwa.
 Kushoto- Bw. Frenk Mwaisumbe na Bi. Grece Tendega.
 Kushoto ni Bw. Godfrey Mgimwa ambaye ni mgombea wa kiti cha Ubunge kwa tiketi ya CCM akitazama "Passpot" yake iliyoshikwa na katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Bw. Hassan Mtenga ikionyesha uthibitisho wa mgombea huyo uzawa na uraia wake wa Tanzania.
 "Passport" ya mgombea wa CCM Bw. Godfrey Mgimwa anayelalamikiwa na CHADEMA kuwa si raia wa Tanzania.
 Barua ya Godgfrey Mgimwa iliyotoa majibu ya pingamizi lililotolewa dhidi yake na mgombea wa CHADEMA Bi. Grace Tendega, kupinga kushiriki katika kampeni na mchakato wa kuwania kiti cha Ubunge jimbo la kalenga, lililoachwa wazi baada ya Dr. Willium Mgimwa mbunge wa jimbo hilo kufariki dunia mapema Januari 2014.
 Passport ya Bw. Godfrey Mgimwa- mgombea Ubunge kwa tiketi ya  CCM jimbo la kalenga- Iringa.
 Msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo la kalenga Bi. Pudensiana Kisaka akizungumzia sakata hilo la Pingamizi na hatua zinazoendelea.

Bi. Pudensiana Kisaka.

<<<<<<<<<<<<<<<HABARI>>>>>>>>>>>>
MGOMBEA wa chama cha mapinduzi CCM amebeza pingamizi lililotolewa na mgombea wa chama  cha demokrasia na maendeleo CHADEMA Bi. Grace Tendega pingamizi lililoitaka tume ya uchaguzi, kumuengua mgombea wa ubunge kupitia CCM - Godfrey Mgimwa kwa madai ya  kutokidhi vigezo vya ushiriki wa uchaguzi huo mdogo jimbo la kalenga, kikiwemo cha mgombea huyo wa CCM kutokuwa raia halali wa Tanzania.

Akizungumzia hatua ya pingamizi hilo Mgimwa amesema hali hiyo inaonyesha dhahiri jinsi CHADEMA wanavyohofia ushindi wa CCM na kuwa pingamizi hilo halina mashiko wala ukweli wowote, huku akiwataka wananchi na wapigakura wa jimbo la Kalenga kuwabeza CHADEMA kwa uzushi huo.

Aidha Mgimwa amesema yeye ni mzaliwa wa mkoa wa Iringa na raia halali wa Tanzania, na kuwa elimu yake ya msingi kuanzia darasa la kwanza hadi la saba aliipatia katika shule ya msingi Wilolesi ya mjini Iringa, huku elimu ya sekondari akisoma  shule ya Azania na St. Mery’s za jijini Dar es salaam.

Aidha Mgimwa amesema kwa kifupi shutuma za CHADEMA siyo za kweli hata kidogo kwani huku nje ya nchi alikwenda kwa ajili ya kupata elimu ya chuo cha Uingereza, degree ya miaka mitatu na elimu ya juu kwa mwaka mmoja na akarudi nchini kwa ajili ya kuijenga nchi kwa kile alichokisomea.

“Ninatoa masikitiko yangu makubwa kwa CHADEMA kwani shutuma hizo siyo za kweli, kwa ufahamu wangu nchi ya Tanzania hairuhusu mtu mmoja kuwa na uraia wa nchi mbili, kwani mimi ni raia mzawa halali wa Tanzania na Pasport yangu hii hapa, wazazi wangu wote niwa Tanzania na nimezaliwa katika Hospitali ya mkoa wa Iringa, lakini CHADEMA wameshindwa kudhibitisha juu ya shutuma wanazozielekeza kwangu,” Alisema Mgimwa.

Katibu wa CCM Wilaya ya Iringa Amina Himbo amesema kuhusiana na Stakabadhi za wadhamini wa Mgimwa hilo sila ukweli kwani wadhamini wa mgombea wao ni viongozi wa jimbo la kalenga, na wanachama wa CCM wa jimbo la Kalenga na kuwa pingamizi hilo nila uongo nala hila lenye kutaka kuwadanyanya wapigakura wa Kalenga.

Katibu wa CCM Mkoa wa Iringa Hassan Mtenga ameitaka CHADEMA kutafuta mbinu nyingine za kuwadanganya wananchi wa kalenga kwa madai kuwa mgombea wao ni Mtanzania na hana dosari yoyote inayomfanya asishiriki uchaguzi huo mdogo wa jimbo la kalenga.

Akizungumzia juu ya pingamizi lake mgombea wa CHADEMA Grace Tendega amesema anachopinga si uraia pekee ndiyo  ameuwekea pingamizi dhidi ya mgombea wa CCM Mgimwa, bali hata baadhi ya wadhamini wa Mgimwa  shahada  zao za kupigia kura zinaonyesha kutokuwa niza wakazi wa jimbo la Kalenga.

“Kweli nimeweka pingamizi kwa mgombea mwenzagu wa CCM Godfrey Mgimwa, na niliweka hilo baada ya kusoma fomu yake iliyobandikwa kwenye ukuta ambapo mgombea Mgimwa alionyesha kuwa na mapungufu mbalimbali likiwemo la kutokuwa  raia wa Tanzania, pili katika fomu yake aliyodhaminiwa wadhamini wake hawakutoka Kalenga, na hili tuna ushahidi nalo, kwani kuna  shahada za kupigia kura zinaonyesha baadhi ya wadhamini wametoka Songea, Njombe na Iringa vijijini na siyo jimbo la Kalenga- Lakini lingine ni juu ya kiasi cha fedha za kuendeshea kampeni ambacho kila mgombea alipaswa kuweka bayana ili kuujulisha Umma kuwa ni kiwango gani kitatumika katika kuendeshea kampeni na hili nila sheria za gharama za uchaguzi,  lakini Mgimwa hakujaza kiasi chake cha fedha katika fomu hiyo, hilo nalo limo ndani ya pingamizi,” Alisema Tendega.

Aidha Tendega amesema hata tarehe ya uteuzi mgombea wa CCM amejaza kuwa ni tarehe 16 mwezi wa tatu mwaka 2014 badala ya tarehe 18 mwezi wa pili jambo linaloonyesha CCM bado wanasubiri uteuzi utakaofanyika tarehe 18 mwezi wa tatu na kuwa mgombea aliyopo sasa hafai kushiriki katika kampeni zozote kwa sasa.


Pia Tendega amesema pingamizi lingine ni uwepo wa sahihi tofauti zilizopo katika fomu za udhamini na zile zilizo katika vitamburisho vya kupigia kura, jambo linaloonyesha mgombea wa CCM kuwa na mapungufu ya vigezo vya kushiriki kampeni na uchaguzi huo.


Mratibu wa CHADEMA kanda ya kusini Frenk Mwaisumbe amesema CHADEMA inafuatilia kwa makini kila kitu na kuwa ipo  haja kwa tume ya Taifa ya uchaguzi kutenda haki kwa vyama vyote pasipo kubagua kama kuna uvunjifu wa sheria za uchaguzi.


Hata hivyo msimamizi mkuu wa uchaguzi jimbo la Kalenga Bi. Pudensiana Kisaka amesema amepokea pingamizi hilo siku ya tarehe 19 majira ya saa tisa jioni, kutoka kwa mgombea wa CHADEMA  Grace Tendega dhidi ya Godfrey Mgimwa na kuwa kazi yake kama msimamizi ni kumuandikia barua mgombea aliyewekewa pingamizi hilo huku barua hiyo ikiambatana na Pingamizi.

Kisaka amesema mgombea aliyewekewa Pingamizi baada ya kupata barua iliyoambatana na pingamizi kutoka kwa mgombea wa CHADEMA, amejibu shutuma zinazomkabiri, na kuwa upande uliotoa Pingamizi (CHADEMA) unapaswa kupeleka vielelezo katika ofisi yake ya msimamizi mkuu wa uchaguzi  haraka iwezekanavyo.

“Mimi nikipokea pingamizi ninapaswa kumuandikia barua na kumpatia mgombea aliyewekewa pingamizi hilo huku barua hiyo nikiambatanisha na pingamizi alilowekewa,  na katika kifungu cha 40 cha sheria ya uchaguzi kifungu kidogo cha 4 ”a” kinaruhusu kutoa uamuzi kwa pande zote mbili na kama upande mmoja haujaridhika unaweza kukata rufaa,” alisema Kisaka.


Wakati hayo yote yakiendelea kampeni za uchaguzi kwa mujibu wa tume ya Taifa ya Uchaguzi tayari zimeanza tangu tarehe 19 mwezi huu wa pili  licha ya kuwa kila chama kinataraji kuzindua rasmi kampeni zake kwa kuwashirikisha viongozi wa vyama vyao Kitaifa.


MWISHO

No comments:

Post a Comment