Friday, January 20, 2012

WANANCHI WA IHAHI WACHANGA MIL. 20 KUJENGA SHULE




ZAIDI ya shilingi Milioni 20 zilizochangwa na wananchi wa Kata ya Ihahi katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya zimefanikisha ujenzi wa shule.

Akizungumzia mafanikio hayo, ofisa mtendaji wa Kata ya Ihahi Costantino Tandika  amesema wananchi waliazimia kujenga shule baada ya wanafunzi kutumia muda mrefu kutembea, kwa kufuata elimu katika shule ya sekondari Mengele.

Tandika amesema kila mwananchi alichanga shilingi elfu 10 na makisio yao ilikuwa kukusanya shilingi milioni 15 na jitihada za wananchi hao zimefanikisha kupatikana shilingi Milioni 20.

Amesema fedha hizo zimesaidia ujenzi wa vyumba 4 vya madarasa pamoja na Visima viwili vya maji, vilivyogharimu shilingi laki 3 na kuwa mpango huo ni ushirikiano wa kijiji cha Kibaoni, Muwale na Ihahi.


Naye diwani wa Kata hiyo ya Ihahi Salum bahati amesema Halmashauri iliwaahidi kuwaunga mkono wananchi hao kwa kuwapa shilingi Milioni 40, lakini mpaka sasa hawajapata fedha yoyote, jambo linalosababisha shule hiyo kushindwa kukamilika.

Amesema lengo la mwaka huu 2012 lilikuwa kujenga jengo la utawala na nyumba za walimu, na wananchi wameonyesha mwitikio wa kufanya shughuli za maendeleo kwani mpaka sasa wamefyatua tofali laki moja na 20.




No comments:

Post a Comment