Monday, April 29, 2013

MuCoBa YAWAPATIA WAKULIMA MIKOPO YA BIL. 1.3


 Baadhi ya wateja wa Benki ya wananchi wa Mufindi- MUCOBA wakipatiwa huduma za kifedha.

Ben Mahenge meneja mauzo wa benki ya Wananchi wa Mufindi- MUCOBA akiwa nje ya jengo la benki hiyo akitoa maelekezo. 
 Meneja mauzo wa Benki ya wananchi wa Mufindi - MUCOBA Bw. Ben Mahenge akitoa ufafanuzi wa malengo ya benki hiyo.
 Meneja mauzo wa Benki ya wananchi wa Mufindi - MUCOBA Bw. Ben Mahenge akiwa na Waziri mkuu mstaafu Edward Lowasa.

BENKI ya wananchi wa Wilaya ya Mufindi – MUCOBA, imetoa mikopo ya shilingi Bilioni 1.3 kwa zaidi ya  wakulima 1000 wa Wilaya ya Kilolo, kwa lengo la kuinua shughuli  hizo za kilimo ili  kuwawezesha wakulima kuendesha kilimo bora nacha kisasa.

Akizungumzia mpango huo wa mikopo kwa kundi hilo la wakulima, meneja mauzo wa benki ya wananchi Mufindi- MUCOBA,  Ben Mahenge alisema mpango huo  umelenga kutanua wigo wa utoaji wa huduma za benki hiyo ya MUCOBA-kutoka Wilaya ya Mufindi hadi kuzifikia Wilaya zote za mkoa mzima wa Iringa.

Mahenge alisema utoaji wa huduma za kifedha MUCOBA inakabiliwa na changamoto kubwa ya umbali katika kuwafikia wananchi waishio vijijini, huku baadhi ya wateja wasio waaminifu wakishindwa kurejesha mikopo kwa wakati.

Aidha alisema kukosekana kwa elimu kwa baadhi ya wananchi hususani waishio vijijini - ni moja ya sababu inayoikabili  jamii, huku baadhi yao wakishindwa kuelekeza fedha za mikopo katika malengo yaliyokusudiwa hatua inayosababaisha MUCOBA kuwa na madeni chechefu ya zaidi ya shilingi Milioni 600.

“Kuna baadhi ya maeneo tunalazimika kutembea umbali wa km 150 kuwafuata wateja, lakini unakuta kuna baadhi ya wateja ambao sio waaminifu wanashindwa kurejesha mikopo yao, hii inatokana na kukosekana kwa elimu ya mikopo kwa wananchi,” Alisema Mahenge.

Alisema ipo haja kwa taasisi za kifedha kutoa elimu hiyo kwa wananchi ili kutambua umuhimu wa kuhifadhi fedha benki, ikiwa pamoja na kuwa na uelewa juu ya mikopo ili kuepuka mali zao kubinafsishwa baada ya kushindwa kurejesha mikopo.

Hata hivyo Mahenge alisema benki hiyo imekusudia kuwafikia wananchi wa mkoa mzima wa Iringa, na baada ya kuwafikia wananchi wa Wilaya aya Kilolo wameanza kufanya harakati za kufikisha huduma hiyo Manispaa ya Iringa.


MWISHO
  

No comments:

Post a Comment