Tuesday, April 2, 2013

WANAFUNZI WAJISAIDIA POLINI, WAZAZI WAPEWA ZAMU YA KUKOROGA VYOO


Kibao cha shule y msingi Ndulamo

Na Edwin Moshi, Makete

Shule ya msingi Ndulamo iliyopo kijiji cha Ndulamo wilayani Makete mkoani Njombe, ipo hatarini kukumbwa na magonjwa ya mlipuko kama kipindupindu na kuhara kutokana na kukosekana kwa huduma ya maji.


Akizungumza na mtandao huu ofisini kwake mwalimu mkuu wa shule hiyo Bw. Godigodi Bosco Malangalila amesema tatizo hilo nila muda mrefu na hivyo kutishia usalama wa walimu na wanafunzi.

Malangalila amesema tatizo hilo linahatarisha afya za wanafunzi wake kwani pamoja na ukosefu huo wa maji wakati mwingine shule hulazimika kuvunja vipindi na kuwaagiza wanafunzi kwenda kuchota maji kwenye mito ama visima ambayo si safi wala salama na kulazimika kuyatumia.

“Ndugu mwandishi inasikitisha kwa kweli, hapa shuleni huwa tunatoa uji kwa wanafunzi lakini maji hata ya kuosha vyombo hakuna, ya kutumia vyooni nayo hakuna na vyoo vya shule ni vile vya kutumia maji, lakini wanafunzi huenda kujisaidia hivyo hivyo bila maji” alisema Mwalimu Malangalila,” amesema.

Aidha amesema mara nyingi vyoo vya shule huziba na kulazimika waalimu wenyewe kuvizibua na wakati wengine kuwaita wazazi kuja kuzibua vyoo hivyo lakini hivi sasa wazazi wengi hugoma kuja kufanya shughuli hiyo kwa madai kuwa wao wanachanga fedha za maji kijijini hivyo ni jukumu la vyombo husika kufikisha maji shuleni hapo ili kuinusuru shule hiyo.

Akiongezea Malingalila amesema “Tangu nimefika hapa shuleni kama mwalimu mkuu mwezi Julai 2012, nimeshafunga shule kwa tatizo hili hili, kwa kuwa tunazidiwa,” alisema 

Katika hatua nyingine mwalimu huyo amesema tatizo hilo la ukosefu wa maji pia limeathiri ujenzi wa nyumba ya mwalimu shuleni hapo ambapo ujenzi huo ulikuwa ukamilike Oktoba mwaka jana lakini hadi hivi sasa nyumba hiyo imefikia sehemu ya linta, kwa tatizo kubwa ni ukosefu wa maji

Kwa upande wake Tamali Cyprian Sanga mwanafunzi anayesoma darasa la saba shuleni hapo ambaye pia ni dada mkuu wa shule hiyo amesema tatizo hilo linawathiri kwa kiasi kikubwa wao wanafunzi, kwani huwalazimu kuosha vyombo vya chakula kwa kutumia maji machafu, huku wakikosa baadhi ya vipindi kwa  kwenda kuchota maji mtoni.

“Visima vipo mbali na shule pia vyoo tunavyotumika kwa hivi sasa ni vichafu na hakuna maji ya kuvifanyia usafi na tunalazimika kuvitumia hivyo hivyo,” Amesema.


Naye kaka mkuu wa shule hiyo Alexanda Marko amesema wakati mwingine kutokana na uchafu uliokithiri kwenye vyoo hivyo hulazimika kurudi nyumbani  kujisaidia huku wengine wakijisaidia kwenye msitu wa shule hiyo ambao uko jirani na kuwataka wahusika kulishughulikia ipasavyo tatizo hilo. 

Shule ya Msingi Ndulamo ina jumla ya wanafunzi 633 ambao wanategemea maji ili kuendesha shughuli mbalimbali katika shule hiyo.

MWISHO

No comments:

Post a Comment