Thursday, April 11, 2013

WASOMI JAMII YA WAFUGAJI WAPINGA TAMKO LA SERIKALI LOLIONDO


 Baadhi ya wanachuo wanaotoka katika jamii ya wafugaji, wanaosoma katika vyuo vikuu mkoani Iringa, wakibadilishana mawazo kabla ya kuanza mkutano wa utoaji wa tamko juu ya ardhi ya Loliondo.
Bw. Solomon Lekui, akisikiliza maoni ya wanaumoja baada ya kusoma tamko la wanachuo wanaotoka katika jamii ya wafugaji. 



Bi. Nesale Rorian na wenzake wakisikiliza maoni ya wachangiaji wa tamko hilo.


 
 


Wakiwa katika picha ya pamoja baada ya kumaliza mkutano wa kutoa tamko.

HATIMAYE wanafunzi wa jamii ya wafugaji, wanaosoma katika vyuo vikuu mkoani Iringa, wameungana na kutoa tamko juu ya mgogolo wa Loliondo mkoani Arusha, huku wakimtaka waziri mwenye dhamana ya maliasiri na Utalii, Barozi Khamis Kagasheki   kurejea upya namna ya kufanya utatuzi wa mgogolo huo.


Tamko hilo limetolewa na umoja wa wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Iringa wanaotoka katika jamii ya wafugaji, mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Hotel ya Country Side iliyopo katika eneo la Tumaini mjini Iringa.

Akisoma tamko la wanachuo hao Solomon Lekui ambaye ni mjumbe wa umoja wa jamii ya wafugaji wanaosoma vyuo vikuu mkoani Iringa, amesema kamwe hawapo tayari kushuhudia wazazi wao wakipokonywa ardhi ambayo ni mali yao halali.


Lekui alisema wanapinga vikali amri ya waziri Barozi Khamis Kagasheki aliyoitoa tarehe 26 mwezi wa 3 mwaka huu akiwataka kuhamisha katika makazi yao  wananchi wa Loliondo wanaoishi katika eneo linalodaiwa na serikali kuwa ni poli tengefu (Loliondo Game Controlled Area) ambalo lina ukubwa wa kilomita za mrab  elfu 4.

Lekui alisema eneo hilo mabalo linamilikiwa na vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu, Oloipiri, Oloirien, Maloni, Arash, Malambo na Piyaya vijiji vilivyopo ndani ya Loliondo ni mali halali ya wananchi hao, na si vyema serikali kuchukua uamuzi wa kuwaondoa wananchi hao.

Emmanuel Ole Kileli mwanafunzi kutoka chuo kikuu cha Tumaini alisema imekuwa kama desturi kwa wafugaji kulalamika juu ya mambo mbalimbali yanayohusiana na unyang’anyi wa ardhi yao inayoambatana na uhamishaji kwa kutumia nguvu na upotevu mkubwa wa mali na maisha yao.

Ole Kileli lisema Serikali imekuwa mstari wa mbele katika kutekeleza maamuzi magumu kwa wafugaji nchini, kwa madai kuwa wafugaji wanakiuka sheria kwa kuvamia maeneo mbalimbali yasiyo ya ufugaji hasa maeneo ya hifadhi naya kilimo, na kuwa hatua hiyo ni kutokana na kukosekana kwa sera ya ufugaji asili (Pastoralism Policy) ambayo ingehusika kuratibu na kuthamini shughuli mbalimbali za ufugajiasili na mazao yake kwa ujumla.

Saikon Justin mwenyekiti wa jumuiya ya wanafunzi wanaotoka katika  jamii ya wafugaji alisema serikali inapaswa kutafakari vizuri suala la wafugaji kitaifa, na kutafuta suluhu ya kudumu kwani imepelekea wafugaji kote nchini kuiona serikali ya Tanzania kama adui mkubwa kupitia upotevu wa mali na haki zao za msingi kama watanzania siku hadi siku.

“Serikali na wadau kote nchini waache kubeza ufugaji asili kwa madai ya kuwa hauna tija na huchangia kiwango kidogo cha pato la Taifa, kwani ukweli ni kuwa tafiti nyingi zinaonyesha ufugaji asili una tija na unaliongezea taifa kipato hasa katika ngazi ya Halmashauri ambazo zina mifugo  mingi kwani imekuwa ikipata ushuru kupitia sekta hiyo ya Mifugo,” Alisema Saikon.

Samaito Olekopitoo alisema sekta ya Ufugaji inachangia pato la Taifa kwa kiwango kikubwa kwani inatoa ajira nyingi kuanzia ngazi ya kijiji hadi Taifa, kuanzia kwa wafugaji wenyewe, wafanyabiashara wa mifugo na mazao yatokanayo na mifugo, wakiwemo wamiliki wa Bucha, Maeneo ya nyama choma, Hotel, Vibanda vya Chips na wafanyakazi wao kwa ujumla, kwa hiyo sekta ya mifugo ina tija  na maslahi kwa Taifa.

Aidha waliiomba serikali iundwe Tume maalumu ya kukusanya maoni ya wafugaji kote nchini ili kutafuta namna ya kutatua kikamilifu mgogolo huu, kwa kutumia ushirikishwaji wa matatizo ya wafugaji kote nchini.

Kwa madai kuwa kuna haja ya kutafuta suluhu ya kudumu kwa kuunda sera ya Ufugaji asili ili kuondo ufugaji ndani ya sekta ya kilimo, kwa madai kuwa tafiti mbalimbali zinazoonyesha suala la ufugaji kwenda sambamba na kilimo siyo sahihi hata kidogo.

Nesale Rorian alisema wafugaji na wakulima hawawezi kutekeleza shughuli zao pamoja,  na inaonekana kupitia migogolo mingi ambayo imekuwa ikitokea baina ya wafugaji na wakulima, huku vipaumbele kwenye suala la kilimo, -ufugaji vikiwa haupewi fulsa ya kutosha kama ilivyo kwa kilimo, na kaulimbiu ya KILIMO KWANZA, kwani hapo suala la Ufugaji halikupewa kipaumbele vya kutosha.

Pamoja na hayo wanachuo hao waliitaka serikali iangalie upya maeneo ya wafugaji kupewa wawekezaji pasipo wafugaji wenyewe kushirikishwa na hivyo kuondoa dhana kuwa maeneo ya wafugaji ni maeneo ya wazi na hayana mmiliki.

“Hii ni athari kubwa kwa wafugaji hasa katika ngazi za Halmashauri ambazo wafugaji ni wachache katika hatua ya maamuzi, kwani bajeti zinazopitishwa kwa ajili ya masuala ya ufugaji ni ndogo, huku  wataalamu wa mifugo wakishughulika na masuala ya kilimo,” Walisema.

Keko Olekijepe alisema ufugaji asili ni mfumo wa maisha kama ilivyo mifumo mingine yoyote, na hivyo ni vyema na haki mfumo huu wa Ufugaji ukaheshimiwa na kupewa fulsa kama mifumo mingine katika nchi yetu tukufu ya Tanzania, na kuwa ufugaji asili ukiratibiwa vizuri hauharibu mazingira, tofauti na kilimo ambacho kinachangia moja kwa moja kuharibu uoto wa asili kwa ukataji miti na kuharibu Ikolojia. 

MWISHO



No comments:

Post a Comment