Kituo cha afya cha Kiponzelo kilichopo katika Halmashauri ya wilaya ya Iringa, ambapo uzinduzi wa wiki ya chanjo ulifanyika hapo.
Makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Ritha Mlagala akitoa huduma ya chanjo kwa mtoto katika Kituo cha afya cha Kiponzelo, ikiwa ni ishara ya uzinduzi wa wiki ya chanjo nchini.
Akinamama wa kijiji cha Kiponzelo katika Kata ya Maboga, wakiwa na watoto wao wakisubiri kupatiwa huduma ya chanjo katika Kituo cha afya cha Kiponzelo.
Wahudumu wa kituo cha afya cha Kiponzelo wakiendelea kutoa chanjo kwa watoto walio na umri chini ya miaka mitano.
Muhudumu akimpima mtoto katika kituo cha afya cha Kiponzelo.
ZAIDI ya watoto elfu 9 wa Halmashauri ya wilaya ya Iringa wanakabiliwa na ugonjwa wa kupooza huku kifua kikuu kikiwapoteza watoto walio wengi.
Hayo yamezungumzwa katika uzinduzi wa wiki ya chanjo ya watoto, iliyofanyika katika Kata ya Maboga katika kijiji cha Kiponzelo, ambapo kaimu mganga wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Dr. Ernest Kyungu amesema licha ya uwepo wa vituo 65 vinavyotoa huduma za chanjo kwa watoto chini ya umri wa miaka 5 dhidi ya magonjwa 9, lakini bado kuna changamoto ya magonjwa hayo.
Dr. Kyungu amesema magonjwa yanayosumbua watoto kwa kiwango kikubwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa ni Surua, Kifua kikuu, Pepopunda, Homa ya Ini, Donda koo pamoja na ugonjwa wa kupooza.
Aidha Dr. Kyungu amesema watoto 9274 (108%) wameugua ugonjwa wa Kifua kikuu, Pepopunda, Kifaduro, Homa ya Ini, Uti wa mgongo na Donda koo, huku watoto 9188 ambayo ni asilimia 107% na ugonjwa wa kupooza ukiwakumba watoto 9274 sawa na asilimia 108.
Naye makamu mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Ritha Mlagala amewataka akinababa kushirikiana vyema na akinamama katika kuwapeleka watoto wao kupata chanjo ili kuwanusuru na magonjwa hayo.
“Hapa ninawaona akinamama tu wakiwa na watoto, kuna baba ambaye amekuja na mkewe hapa?? Kama yupo ninampa zawadi, (….Kinya..) jamani hili ni jukumu la wote, akinababa muwasaidie wake zenu kuwaleta watoto wapate chanjo, msiwaachie wanawake tu, kungekuwa na mwanaume aliyeambatana na mke wake kumleta mtoto katika chanjo au amemleta mwenyewe mtoto ningempa zawadi,” Alisema Mlagala.
Mlagala alisema lengo la chanjo hiyo ni kuhakiksha watoto wote wenye umri chini ya mwaka mmoja wanapatiwa huduma hiyo ili kuwaepusha na magonjwa hayo, na kuwa ujumbe wa wiki ya chanjo ni “Chanja jamii, jamii yenye afya” na kauli mbiu yake ikiwa ni “Okoa maisha, kinga ulemavu, Toa chanjo,”.
No comments:
Post a Comment