Tuesday, May 7, 2013

DC AWASWEKA NDANI VIONGOZI


 Mkuu wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, Gerlad Guninita (wapili kushoto) akitoa amri ya kukamatwa viongozi katika uwanja wa mkutano wa kijiji cha Mlafu. (kulia ni kamati ya ulinzi na usalama wa Wilaya hiyo.
Kituo cha Polisi cha Mbigili ambacho viongozi hao wameshikiliwa kwa kukaidi amri ya kuitisha mkutano wa utatuzi wa mgogolo wa wananchi.
Uwanja wa mkutano ukiwa na msafara wa mkuu wa Wilaya pekee.

KATIKA hali isiyo ya kawada, viongozi wa Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, wamemchezea mchezo mchafu mkuu wa Wilaya hiyo ya Kilolo Gerlad Guninita, kwa kumuita katika mkutano usio na wananchi, ambao ulilenga utatuazi wa mgogolo wa ardhi.

Tukio hilo la aina yake limetokea baada ya mkuu huyo kufunga safari ya kuitika wito huo, ambao ulilenga utatuzi wa mgogolo wa ardhi ambayo imechukuliwa kwa kiasi kikubwa na mtu mmoja jambo ambalo ni uvunjwaji wa sheria za ardhi, huku akikuta katika uwanja wa mkutano hakuna wananchi jambo lililompandisha hasira mkuu huyo.

MKUU huyo  alifika katika eneo la mkutano majira ya saa sita kasoro na kukaa kwa zaidi ya saa moja bila mafanikio ya kuwapata wananchji, jambo lililobainisha mapungufu katika utendaji wa kazi wa viongozi hao na mkuu huyo kutoa amri kwa askari polisi walioambatana na msafara huo kuwakamata viongozi hao waliosababisha hasara kubwa kwa Halmashauri hiyo.

Guninita alijikuta katika mkutano huo akiwa yeye, kamati ya ulinzi na usalama, wataalamu wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo pamoja na wanahabari ambao walikuwa wameambatana nae katika msafara huo.

Mkuu huyo wa wilaya ya kilolo alisema hakuna haja ya kuwachekea viongozi wsa aina hiyo, ambao hawatilii maanani vilio vya wananchi wao, kwa kupuuzia muafaka wa mgogolo huo unaowasumbua wananchi.

“Sioni sababu ya kuwachekea watu wa aina hii, hawa ndiyo wanachangia kudhorotesha maendeleo, OCD hakikisha unaondoka na hawa viongozi, ofisa tarafa wa tarafa ya Mazombe na huyu kaimu mtendaji wa Kata hii ya Mlafu, siwezi nikafunga safari ndefu  kutoka kilolo na msafara mzima halafu nafika hapa hakuna wananchi, kama kulikuwa na tatizo kwa nini msingenijulisha kwa simu ili nisipoteze muda wangu nawa wataalamu wangu hawa, hawa wakakae Rock up hadi kesho ili liwe fundisho kwa viongozi wa aina hii hapa Kilolo,” Alisema Guninita.

Alisema viongozi hao kupitia mikutano yao ya awali walimuomba afike kijijini hapo ili kufanya mazungumzo na wananchi wa kijiji hicho juu ya mgogolo huo wa ardhi, na walimtaka tarehe 30 mwezi uliopita naye aliomba udhuru kwakuwa alikuwa na kikao cha utoaji wa taarifa ya utekerezaji wa shughuli za maendeleo, wakampangia mkuu huyo wa Wilaya afike tarehe 7 ya mwezi huu Mei  kuzungumza na wananchi na hatimaye kuikuta hali hiyo.

Seljo Nyauhele, mjumbe wa serikali ya kijiji cha Mlafu na Festo Kakoko mwenyekiti wa akitongoji cha Masukanzi walisema wanaungana na hatua ya mkuu huyo wa Wilaya, kwani licha ya kuwepo kwa dharula ya msiba viongozi hao walipaswa kuandaa mazingira ya mkutano ili wananchi wapate muafaka wa tatizo lao linalowakabili kwa muda mrefu.

Naye Gaitan Mwagala, diwani wa Kata aya Mlafu alisema siku ya nyuma walikuwa walijadili na kupanga masuala mbalimbali ya mkutano huo, na aameshangazwa  kukuta uwanja wa mkutano ukiwa hauna watu.

“Unajua kuna haja ya kupeana adhabu pale tunapofanya ndivyo sivyo, jana tulikuwa na kikao cha ODC, tukakubaliana kutengeneza mazingira ya mkutano, lakini ninashangaa kuona hali hii, watu wengine wafundishike kwa namna hiyo,” Alisema  Mwagala.

Waliokamatwa na kuswekwa lumande ni pamoja ofisa tarafa wa tarafa ya Mazombe Silvanus King’ung’e na Kaimu mtendaji wa Kata hiyo ya Mlafu Thomas Nyabangi  ambapo walifungiwa katika Lumande ya kituo cha Polisi cha Mbigili.

Hata hivyo mkuu huyo wa Wilaya Guninita amesema hatua hiyo ni fundisho kwa viongozi wengine ambao wamekuwa wakipuuzia maagizo yenye maslahi kwa wananchi, huku baadhi ya wananchi na viongozi wa kijiji hicho wakiunga mkono hatua ya mkuu huyo.

Moja ya hasara zilizotokana na uzembe wa viongozi hao, ni pamoja na Halmashauri kujingia hasara ya matumizi yasiyo ya halali ya mafuta ya magari ambayo yaliwabeba wataalamu mbalimbali wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, gari la kamati ya ulinzi na usalama, gari la wanahabari pamoja na gari la mkuu wa Wilaya mwenyewe, jambo ambalo litachangia matumizi yasiyo ya halali ya fedha za wananchi (Walipakodi).



MWISHO


No comments:

Post a Comment