Friday, May 3, 2013

MAHAKAMA KUINGIA KATIKA MATUMIZI YA TEKNOHAMA


 Jaji kiongozi wa mahakama kuu ya Tanzania Mhe. Fakihi Jundu, akizindua jengo la Mahakama ya Mwanzo Wilayani Kilolo- katika mkoa wa Iringa.
 Bango la uzinduzi wa Mahakama ya Mwanzo Wilayani kilolo.

 Jaji mfawidhi wa mahakama kuu mkoa wa Iringa- Mhe. Sekieti Kihio, akizungumzia hali ya Mahakama za Mwanzo mkoani Iringa zilivyo chakavu.
 Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Gerlad Guninita akipanda mti kumbukumbu katika eneo la jengo la mahakama ya Mwanzo Kilolo, baada ya kuzinduliwa rasmi wa mahakama hiyo.
 Jaji mfawidhi wa mahakama kuu mkoa wa Iringa- Mhe. Sekieti Kihio akipanda mti wa kumbukumbu katika eneo hilo la Mahakama.
Wananchi wa Wilaya ya Kilolo wakisikiliza hotuba ya Jaji kiongozi baada ya uzinduzi wa mahakama hiyo. Jengo lililozinduliwa ni hilo nyuma ya wanancho hao.
Mahakimu wa Mahakama mkoani Iringa, wakiwa katika picha ya pamoja na Jaji kiongozi wa mahakama kuu Tanzania Mhe. Fakiri Jundu, baada ya uzinduzi wa Mahakama hiyo ya Mwanzo mkoani Iringa.

LICHA ya mahakama nchini kuzoea matumizi ya karatasi na karamu katika uendeshaji wa shughuli kesi na mashtaka , sasa muhimili huo hivi karibuni utaanza matumizi ya Teknohama kwa lengo la kuharakisha maamuzi yake na kupunguza muda wa uendeshaji wa kesi mahakamani hadi kufikia muda wa miaka miwili pekee.

Hayo yalizungumzwa na Jaji kiongozi wa mahakama kuu Tanzania Mhe. Fakihi Jundu wakati akizindua rasmi mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, hiyo pia ikiwa ni hatua ya  kuboresha miundombinu ya Mahakama na majengo yake.

Jaji Jundu alisema hatua ya matumizi ya Kompyuta itarahisisha kazi za Kimahakama ikiwa pamoja na kupunguza malalamiko kwa wananchi juu ya upatikanaji wa nakala za hukumu.

“Hatua hii itatuwezesha kufanya kazi zetu kiurahisi kupitia mfumo wa kompyuta,  wadau wetu watapata kumbukumbu za mashauri ya kimahakama, na pia itapunguza kama siyo kumaliza kabisa baadhi ya changamoto za uhaba wa wahudumu wa kuchapa,” Alisema.

Alisema kuna haja wananchi nao wakajihusisha katika ujenzi wa mahakama ili kuyafanya majengo yake kuwa bora na hivyo kujenga imani ya utoaji wa haki kwa mahakimu wake.

“Tunamazingira magumu sana katika mahakama zetu, kwani hata vifaa vya kuchapa ni duni na tumekuwa tunapeleka kilio serikali lakini majibu ni kuwa bajeti ni finyu,” Alisema Jundu.

Aidha alisema uchakavu wa miundombinu ya mahakama nyingi nchini unasababisha wasomi wa taaluma hiyo kuzikimbia, kutokana na kukosekana kwa hadhi ya majengo ya mahakama, huku baadhi yake zikikosa hata huduma muhimu ya vyoo.

Alisema mahakama ya Tanzania pia imejipanga kupunguza kero za mashauri ambayo yanaendeshwa kwa muda mrefu na kuzifanya kesi zisiendeshwe kwa zaidi ya miaka miwili na mpango huo unanzia katika mahakama za mwanzo.

Naye Sekieti Kihio jaji mfawidhi wa mahakama kuu mkoa wa Iringa alisema  wananchi mkoani Iringa wanapata ataabu katika kupata huduma ya haki kutokana na uhaba wa majengo huku baadhi ya Mahakama zikiwa ni majengo ambayo yamekodiwa kwa chama cha mapinduzi.

“Kwa hali tuliyonayo sasa, mahakama zetu hizi mbovu hazina nafasi, hii ni kutokana na mahakimu wa mahakama za mwanzo kutakiwa kuwa na kiwango cha elimu ya digree, kwa hiyo wasomi hao hawakubali kufanya kazi katika mazingira ya mahakama hizo chakavu, nyingi zinakimbiwa na wasomi hao,” Alisema Kihiyo.

Juma Kisailo kaimu msajili wa mahakama kuu kanda ya Iringa alisema changamoto kubwa katika Mahakama hiyo ya Kilolo ni kukosekana kwa watumishi, vitendea kazi, usafiri, samani za kiofisi pamoja na kukosekana kwa mashine ya kuchapia.

"Mheshimwa jaji, hitaji lingine la muhimu ni kukosekana kwa usafiri na ulinzi wa mahabusu pindi tunapotaka kuwapekeka Mahabusu na pindi wanapotakiwa tena kuletwa Mahakama siku ya kesi zao, na tatizo hili linazikabili mahakama karibu zote za mwanzo, hii inasababisha ucheleweshaji wa kesi za jinai," Alisema Kisailo.

Hata hivyo jaji kiongozi wa mahakama kuu Tanzania aliwataka mahakimu nchini licha ya kufanya kazi katika mazingira duni, kutenda haki kwa wananchi, pasipo kujihusisha na masuala ya upokeaji wa rushwa ili kujenga imani kwa jamii.
Oktavian Magoda mwananchi wa wilaya ya Kilolo alisema awali walitumia muda mwingi kutembea, wakifuatilia mwenendo wa kesi zao, na hivyo kutembea umbali wa zaidi ya km 15, huku wakilazimika kuchukua na chakula cha kula njiani wanapokwenda mahakamani.

MWISHO



No comments:

Post a Comment