Saturday, August 31, 2013

PSPF YAKOPESHA NYUMBA



PSPF YAWAKOPESHA NYUMBA WATUMISHI

MFUKO wa pensheni kwa watumishi wa Umma PSPF mkoani Iringa umeanza mpango wa ujenzi wa nyumba zaidi ya nyumba 200 zitakazogharimu zaidi ya shilingi bil. 9 ambazo zitatolewa kwa njia ya mkopo kwa watumishi waliojiunga na mfuko huo.

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa mpango huo, katika ziara kamati ya mipango miji na mazingira ya madiwani wa manispaa ya Iringa, meneja wa PSPF mkoa wa Iringa Msafiri Mugaka alisema tayari nyumba 25 zimekamilika katika jumla ya viwanja 200 walivyopatiwa na Manispaa ya Iringa.
 
Mugaka alisema kukamilika kwa mradi huo wa ujenzi wa nyumba hizo 25 za awamu ya kwanza, kutawafanya waanze ujenzi wa awamu ya pili na lengo likiwa ni kuwaondoa watumishi na adha za kuishi katika nyumba za kupanga kwa kuwapatia makazi yao.

Aidha Mugaka alisema ujenzi wa nyumba hizo 25 umegharimu shilingi bil. moja (1), na kuwa mkopo huo mteja alitakiwa kurejesha ndani ya miaka 25 kwa makato ya mshahara, na kuwa hatua hiyo itatoa fulsa kubwa kwa wateja wa mfuko huo kumiliki nyumba zao wenyewe.

"Tumetambua kuwa watumishi walio wengi mpaka wanastaafu wanakuwa hawana makazi, basi tukaamua kutoa fulsa hii ili kuwawezesha watumishi walio wateja wa PSPF kukopa nyumba kwa kurejesha mkopo kwa njia ya makato ya mishahara yao, tunajenga hapa nyjmba zaidi ya 200 lakini mahitaji ni mengi sana, na tutajenga zaidi kulingana na jinsi tutakavyopatiwa viwanja, kwani mradi wetu huu ni endelevu," Alisema Mugaka.

Alisema pia mpango huo utaboresha maisha ya watumishi kwani walio wengi hadi muda wa kustaafu huwa hawana makazi kwa kukosa fulsa za mikopo ya muda mrefu na kuwa maisha ya utumishi yanahitaji makazi na nyumba bora.

"Tumeamua kuandaa maisha bora kwa wanachama wetu, tunafahamu watumishi wengi wa umma hadi unafika muda wa kustaafu huwa hawana makazi, na hii inatokana na mifuko mingi kutotoa fulsa za mikopo kama hii ya nyumba, tunawawezesha wanachama wa PSPF kulipa mkopo huu kwa muda mrefu, mkopo wa miaka 25 ni sawa kila mwezi kulipia laki mbili, itasaidia watumishi waliojiunga na mfuko huu wasiwe na maisha magumu kwa kukosa makazi kwa siku za baadaye," Alisema.
 
Aidha alisema mradi huo wa ujenzi kwa nyumba 200 zilizopo katika eneo la Mawelewele utakamilika ndani ya miaka mitatu, ambapo wataendelea kujenga katika maeneo mengine kwa kadri watakavyopatiwa viwanja.

Mwenyekiti wa kamati ya mipangomiji na mazingira, diwani wa kata ya Mtwivila Vitus Mushi alisema mkopo huo wa PSPF utawasaidia watumishi walio wengi waliojiunga na mfuko huo kuwaondosha na adha za kupanga nyumba, kwa kuwa mfuko huo umetoa fulsa kwa watumishi wa umma kuwa na makazi bora.

"Nyumba za kupanga siku hizi zimepanda sana kodi zake, sasa malipo ya mkopo huu wa muda mrefu kwa mwezi ni sawa na kodi ya mwezi mmoja, hii ni fulsa tosha kwa watumshi wa umma, malipo ya miaka 25 ni kipindi kirefu sana, tena mtu unakuwa katika nyumba yako," Alisema Mushi.

Naye naibu meya wa manispaa ya Iringa Gervas Ndaki alisema awali Manispaa ilitoa viwanja hivyo kwa mfuko mwingine ambao haukuweza kufanya maendelezo ya viwanja hivyo na ndipo wakaamua kuwapa PSPF ambao kwa kipindi cha muda mfupi tayari wametekeleza adhma ya ujenzi huo.

Hata hivyo alisema endapo kasi ya ujenzi itaendelea na kumaliza nyumba hizo 200 manispaa itaona uwezekano wa kuwaongezea viwanja vingine PSPF ili watumishi wengi wa Manispaa ya Iringa wanufaike na mkopo huo wa nyumba.
 
"Baaada ya kuwagawia hawa PSPF viwanja hivi 200, leo tunaona mafanikio haya yameanza, kwa kasi hii tunaweza kuangalia na maeneo mengine tukawapatia viwanja ili kuwaondoa watumishi wetu na tatizo la nyumba za kupanga," Alisema Ndaki.
MWISHO.
 
 
 

No comments:

Post a Comment