Thursday, September 26, 2013

WATELEKEZA WATOTO KWA ULEVI

Bango la kituo cha kulelea watoto cha Amani kilichopo katika kijiji cha  Mkawaganga, Kata ya Mbigili katika Wilaya ya ya Kilolo mkoani Iringa.
                              Watoto
 Mkurugenzi wa kituo cha Amani Bw. Ingolenz Aohm, akiwa na mtoto mmojawapo kati ya watoto zaidi ya 60 anaowalea katika kituo chake cha Amani, kilichopo Mkawaganga  Kata ya Mbigili katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.  

 Mtoto mdogo mwenye takribani mwaka mmoja na nusu, anayelelewa na kituo cha Amani  akipokea Pipi kama sehemu ya faraja kutoka katika kikundi cha KEPD.
 Viongozi wa KEPD wakitoa baadhi ya misaada kwa watoto wa kituo cha Amani, mara baada ya kuwatembelea watoto hao kama ni ishara ya kujali uwepo wa watoto hao.
 Watoto wa Kituo cha Amani wakipokea baadhi ya misaada kutoka kwa kikundi cha kijamii cha KEPD,  kushoto ni mkurugenzi wa kituo hicho cha Amani Bw. Ingolenz Aohm.
  Watoto wa kituo cha Amani wakicheza ngoma ya kuwakaribisha wageni waliofika kuwatembelea kama ni sehemu ya kujali uwepo wa watoto, ambapo wageni hao kutoka kikundi cha kijamii cha KEPD walitoa misaada mbalimbali kwa watoto hao.
Viongozi wa KEPD wakiwa katika picha ya pamoja na wtoto pamoja na uongozi wa kituo cha Amani kinachojihusisha na malezi ya watoto Yatima na waishio katika mazingira hatarishi.
 Watoto wa kituo cha Amani wakicheza kuashiria furaha yao ya kutembelewa na viongozi wa kikundi cha kijamii cha KEPD, ambacho kilitoa misaada mbalimbali kwa watoto wa kituo hicho.
 Watoto wa kituo cha Amani wakipiga ngoma kushangilia ugeni wa kikundi cha kijamii cha KEPD mara tu baada ya kuwasili katika kituo hicho kwa lengo la kusaidia watoto hao.
 Mtoto akipokea moja ya misaada iliyotolewa na kikundi hicho cha kijamii cha KEPD cha Kilolo Mkoani Iringa.
Viongozi wa kikundi cha kijamii cha KEPD wakitoa misaada kwa watoto wa kituo hicho cha Amani.

 IMEFAHAMIKA kuwa kuongezeka kwa kundi kubwa la watoto waishio katika mazingira hatarishi na magumu, kunatokana na kukithiri kwa ulevi kwa baadhi ya wazazi na walezi, na hivyo kusababisha familia kushindwa kupata mahitaji muhimu.
Hayo yalizungumzwa uongozi wa kituo cha Amani kinachojihusisha na malezi ya watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi, kilichopo katika kijiji cha Mkawaganga, Kata ya Mbigili katika Wilaya ya ya Kilolo mkoani Iringa, wakati kikundi cha kijamii cha Kilolo Empowerment for Persons With Disability (KEPD) kilipokuwa kikitoa msaada kwa watoto hao.



Mlezi mkuu wa kituo cha amani Grecy Mosha alisema baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakizisahau familia zao, baada ya kuzidiwa na ulevi, na hivyo watoto kukosa huduma, huku baadhi ya familia zikitawanyika kwa tatizo la ndoa za wake wengi.

Mosha alisema pia idadi ya watoto hao inachangiwa na tatizo la ugonjwa wa ukimwi, ambapo baadhi ya watoto hujikuta wakibaki yatima baada ya kufiwa na wazaziu wao, huku walezi walioachiwa watoto hao wakiwa hawana uwezo wa kuwamudu kwa kukidhi mahitaji.

"Hapa kwetu tuna jumla ya watoto 62, watoto hawa baadhi yao tumewapokea wakiwa wachanga kabisa baada ya wazazi wao kufariki, lakini wengine walitelekezwa na walezi au wazazi wao kwa ulevi, unywaji wa pombe kupindukia unachangia sana familia kushindwa kupata mahitaji na hivyo watoto wengi huamua kukimbia na kurandaranda mitaani," Alisema Mosha.

Mkurugenzi wa kituo hicho cha Amani raia wa Ujerumani Ingolenz Aohm alisema changamoto ya kipato duni inachangia uwepo wa watoto hao yatima, kwani baadhi ya watoto wanaopelekwa katika kituo hicho huwa na tatizo la ugonjwa wa utapiamlo.


"Kuna watoto hapa ambao tangu wameletwa hakuna hata ndugu wanaokuja kuwaona, wamewatelekeza kwenye kituo, na sisi hawa ni watoto wetu kwani tunawahudumia hadi wanapofikia umri wa kujitegemea, kuna wale ambao tunawasomesha hadi vyuo vikuu, huku baadhi yao wakiwa katika vyuo vya ufundi, mpaka wanapokuwa na uwezo wa kujitegemea," Alisema Ingolenz.
Hata hivyo viongozi wa KEPD, Tumaini Ngajilo, Biliery Maketa na Kelvin Mwambela waliitaka jamii kuwajibika ipasavyo katika kuwalea watoto yatima na waishio katika mazingira hatarishi na magumu pasipo kuwaachia wageni kutoka nje ya nchi, kwa kuwa jukumu hilo nila kila Mtanzania.

"Kuna kila sababu ya kuwasaidia watoto hawa, tusisubiri tu wafadhili kutoka nje ya nchi au asas, hili ni jukumu na wajibu wetu watanzania wenyewe, kwani watoto hawa ni wetu, na kila mmoja aone anaguswa na tatizo la watoto hawa,' Alisema Ngajilo.

Kwa mujibu wa Kelvin Mwambela mhasibu wa KEPD jumla ya shilingi Milioni moja na laki saba zimetumika katika kutoa misaada mbalimbali kwa kundi hilo la watoto yatima na walemavu wa ngozi (Albino) katika Wilaya hiyo ya Kilolo.

Kituo hicho cha Amani kinahudumia zaidi ya watoto 60 wanaoishi ndani ya kituo, huku kikitoa misaada mbalimbali ya kijamii kwa wagonjwa wa majumbani, na watoto wenye mazingira magumu, ambao wanaishi na bibi au babu zao wasio na uwezo wa kifedha.
                                        MWISHO

No comments:

Post a Comment