Tuesday, October 1, 2013

UJAMBAZI WA FEDHA KATIKA MABENKI WAVITISHIA VICOBA

                                                      
 Wanachama wa vicoba Kata ya Ulete wakiwa katika sherehe ya uzinduzi wa vikundi viwili vya vicoba, kikundi cha UAMSHO na kikundi cha ULETE , ambapo vikundi hivyo vimepatiwa shilingi Milioni tano na laki tano na Dr. Willium Mgimwa ambaye ni mbunge wa jimbo hilo, kama njia ya kuwaunga mkono- mbunge huyo pia ni waziri wa fedha na uchumi.
 Bw. Joachim Mgimwa mgeni rasmi wa sherehe za uzinduzi wa Vicoba vya UAMSHO na kikundi cha ULETE ambapo mgeni huyu kwa niaba ya Dr. Mgimwa alipatiwa  Kiti kama ni ishara ya  Dr.Mgimwa kuendelea kukalia kiti cha Ubunge alionao. 
 Wakisherekea uzinduzi huo katika ukumbi wa Kata ya Lumuli Iringa vijijini.
 Bi. Tisiana Kikoti mratibu wa Vicoba mkoa wa Iringa, akifungua Shampeni, kama ni ishara ya kuvizindua vikundi hivyo vya Vicoba katika hafla hiyo.
 Bi. Tisiana Kikoti akiwa tayari amefungua Shampeni katika sherehe hiyo.
 Bw. Joachim Mgimwa  mgeni rasmi wa sherehe za uzinduzi wa vicoa akiwa na katibu wa mbunge Dr. Willium Mgimwa- Bw. Simangwe
                                                                  "Baada ya uzinduzi sasa tunasherekea kwa pamoja"
          "Tunaserebuka kwa raha zetu, sasa je!!" 
 "Kiti hiki tunakukabidhi ukampe Mh. Willium Mgimwa, hii ni ishara yetu kuwa sisi wanavicoba tunamkalisha katika kiti hiki aendelee kukalia nafasi ya uongozi alionao, huyo ndiyo mbunge wetu kwa miaka 25 ijayo," Wakisema wanavicoba.
              
WIMBI la uvamizi wa majengo ya taasisi za kifedha nchini, kumezitia shaka benki za wananchi waishio vijijini - Vicoba, kwa madai kuwa matukio hayo yanawafanya wahofie fedha zao kuibiwa, na hivyo kuomba msaada kwa serikali kuweka ulinzi madhubuti kwa benki hizo za vijijini ikiwa pamoja na kujengwa kwa vituo vya polisi kila kata.

Wakizungumzia kutanda kwa hofu hiyo katika uzinduzi waVicoba, kikundi cha Uamsho na Ulete vya Iringa vijijini, wanachama hao wamesema fedha zao zipo mashakani kutokana na uwepo wa matukio ya uvamizi wa benki nchini kukithiri, licha ya kuwa taasisi hizo kubwa za kifedha zina ulinzi, na kuwa hali hiyo ni tishio kwa baadhi ya vikundi ambavyo havina hata akaunti katika benki, kwani hulazimika kuweka fedha nyumbani.

Benitho Kimuli mwanachama wa Vicoba amesema matukio ya ujambazi katika benki kubwa ambazo zina ulinzi ni tishio kwao wanaoanzisha benki za wananchi vijijini, kwani vikundi vyao havina ulinzi wa kutosha.

"Tunakutana na kuchangishana fedha, ambazo baada ya muda tunakopeshana, benki hizi zinatusaidia sana sisi wananchi wa vijijini, kuwa na uhakika wa kutatua matatizo yetu, lakini kikubwa ambacho ninakiona hapa ni hili tatizo la ujambazi, benki zetu hizi hazina ulinzi, tungeiomba serikali itusaidie japo ujenzi wa Vituo vya Polisi kwa kila Kata ili kuwa na askari jirani," Alisema Kimuli.

Diwani wa Kata ya Lumuli Mh. Charles Lutego alisema kukosekana kwa vituo vya Polisi katika Kata ni changamoto kubwa inayotishia usalama wa fedha za wanavikundi vya Vicoba, kwani majambazi wanaweza kuvamia katika vikundi hivyo na kuiba fedha.

"Hili linatutia shaka sana, kama benki hizo kubwa ambazo zina ulinzi wa kutosha tunasikia majambazi wameiba, iweje sasa kwa sisi huku vijijini benki zetu ambazo hazina ulinzi, ipo haja kwa serikali kuboresha mazingira ya usalama kwa wananchi wa vijijini ili kutowakatisha tamaa wananchi hao ambao wameonyesha nia ya dhati ya kuondokana na umasikini," Alisema Lutego.


Naye mratibu wa Vicoba mkoani Iringa Bi. Tisiana Kikoti ametoa onyo na kalipio kali juu ya fedha za wanachama wa vicoba ambapo baadhi ya viongozi wamekuwa wakitaka kujinufaisha na benki hizo za vicoba huku wakiwa hawataki kutoa ushirikaino kwa wanavicoba.

"Mimi nawaambieni ukweli kabisa, nyinyi viongozi mnapenda sana kuwatumia hawa wanavicoba, na hata wanapokuja viongozi wa ngazi za juu mnapenda kujitutumua kuwa mmeanzisha vikundi hivi, lakini ukweli ni kwamba hamna ushirikiano mzuri na wanavicoba hawa," Alisema Kikoti.

Hata hivyo Bi. Kikoti aliwataka viongoizi wa serikali ya kijiji hicho kukabidhi fedha za wanavicoba ambazo hundi ya fedha hizo zilitolewa na mkuu wa amkoa wa Iringa Dr. Christine Ishengoma katika uzinduzi wa moja ya kikundi mwaka 2012.
"Ninashangaa kusikia kutoka kwa viongozi wa Vikundi kuwa eti hela iliyotolewa na mkuu wa mkoa shilingi laki moja hadi leo mwaka unakatika pesa hiyo hawajakabidhiwa wanavikundi, sasa mimi siwezi kulinyamazia suala hili, ninachotaka wanakikundi wangu wapewe hela yao, toeni mfukoni mwenu kama mnasema hundi iliisha muda wake nyinyi ndiyo mmesababisha, cha msingi mkaombe huindi nyingine wanachama wangu wapewe pesa yao," Alisema Bi. Kikoti.
 
Ofisi ya mbunge wa jimbo la Kalenga Dr. Willium Mgimwa ambaye ni Waziri wa fedha nchini, kupitia mwakirishi wake Johakim Mgimwa imetoa ahadi ya kuviwezesha vikundi hivyo viwili jumla ya shilingi Milioni 5 na laki 5.

Aidha Bw. Johakimu aliwataka wavikundi hao kuwa wabunifu katika kufanya shughuli za kiuchumi ili kuondokana na umasikini ikiwa pamoja na kuchangia masuala muhimu ya kijamii, kama kuwasaidia watoto Yatima na kujitolea katika michango ya elimu na afya pasipo kuwategemea wahisani kutoka nje ya nchi.
"Wanavicoba ili vikundi vyenu viwe endelevu mnapaswa kuwa wabunifu sana, buni miradi itakayowaleteeni faida, fanyeni shughuli za kiuchumi katika kuondokana na hali ya umasikini, lakini muwe ni watu mnaojitolea kwani mtaweza kubarikiwa zaidi, kwa mfano kuwasaidia watoto yatima, na hata kujitolea michango yenu kujenga miundombinu ya kielimu kama vyoo vya shule, siyo jambo la vyoo mpaka msubiri wahisani kutoka nje ya nchi, haipendezi kabisa, kwa Watanzania tunaweza bila kusubiri misaada kwani hata ukisoma vitabu vya uchumi unaona suala hilo.

Joachim alisema fedha hizo zitakazotolewa na Dr. Mgimwa zimezingatia ukubwa wa hisa kwa vikundi hivyo, kwani vikundi vina zaidi ya shilingi Milioni 16 hali inayoonyesha wanachama wake wamejitoa kuelekeza nguvu zao kuondokana na umasikini na kukuza uchumi, na awali katika kikundi cha Udumuka walipatiwa shilingi Milioni tatu kutokana na kikundi kuwa na akiba ya zaidi ya shilingi Milioni 7 na kuwa waziri Mgimwa ataendelea kuwasaidia wanavikundi ambao wanaonyesha mwamko zaidi.
MWISHO
 
 
 
 

No comments:

Post a Comment