Monday, October 7, 2013

HALMASHAURI YACHEMSHA MWAROBAINI WA WEZI WA DAWA ZA WAGONJWA


 Katibu wa afya Wilaya ya Iringa Bw. Willison Luvanda akitoa elimu kwa bodi ya afya juu ya majukumu ya kazi katika kuhakikisha huduma ya afya inaboreshwa na kutatua changamoto zilizopo, katika kikao cha kuidhinisha bodi hiyo, kilichofantika katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo, katika ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
 Mkuu wa Wilaya ya Iringa Dr. Retisia Warioba akitoa nasaha kwa bodi ya afya ya Wilaya ya Iringa.
 Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Pudensiana Kisaka naye akisisitiza juu ya uaminifu na utendaji bora wa kazi kwa bodi hiyo ya afya.
 Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Iringa Mh. Aloyce Masua akitoa kiapo cha utii wa kazi kwa mujibu wa katiba katika kifungu cha sheria za afya, kinachowataka wajumbe wa bodi hiyo kuapa juu ya utendaji wao wa kazi.
 Wajumbe wa bodi na wadau wa sekta ya afya wakisikiliza kwa umakini mkubwa mafunzo ya namna ya kazi za bodi ya afya katika kikao hicho.
 Afisa habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bw. Kisika (kushoto) akiwa na Dr. Rosalia Mkolomi katika kikao hicho cha kuapishwa wajumbe wa bodi ya afya.

Bw. Mpelembwa (mwenye miwani) mdau wa afya kutoka idara ya elimu akisikiliza kwa makini kazi za bodi ya afya.
Afisa lishe Wilaya ya Iringa Bw. Martin Chacha akiwa katika kikao hicho cha uapishwaji wa wajumbe wa bodi ya afya 
 Bw. Nuhu Chorobi ambaye ni mjumbe wa bodi ya afya akipitia baadhi ya dondoo za majukumu yake ya kazi katika bodi hiyo
 Bi. Blandina Mkumbwike akitoa mada juu ya kazi za bodi na mafanikio endapo majukumu yatafanyika kwa weredi wa kutosha.
Mganga mkuu wa Wilaya ya Iringa Dr. Ignus Mlowe akiwa na afisa habari Bw. Erick Mwezakurungi Bange  


ILI kufanikisha huduma bora ya afya nchini, watumishi wa idara hiyo nyeti ya afya wametakiwa kuwa waaminifu, kwa kuzingatia taratibu na kanuni za sheria, ikiwa pamoja na kuacha wizi wa dawa za wagonjwa, tabia ambayo imekuwa ikifanywa na baadhi ya watumishi wa idara hiyo.
 
Hayo yamefahamika katika kikao cha bodi ya afya cha Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kilichoundwa ili kusimamia huduma ya afya na kwa kuwahimiza wananchi kujiunga katika mfuko wa huduma ya afya ya jamii (CHF).

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Steven Mhapa amesema kamwe Halmashauri yake haitawafumbia macho watumishi wasio waadilifu, na ambao ni kikwazo kwa wananchi, na kuwa tayari wamewasimamisha baadhi ya watumishi wa idara ya afya, ambao wamekiuka maadili ya utumishi wa Umma.
 
Aidha Mhapa amesema Halmashauri haitakuwa taryari kumvumilia mtumishi asiye na nidhamu, kwani dawa nyingi zimekuwa zikisafirishwa kutoka katika bohari ya dawa MSD lakini zimekuwa zikichepushwa na kushindwa kuwafikia wananchi ambao ndiyo walengwa.

Ameitaka bodi hiyo kufanya kazi kwa ufanisi ili kukidhi viwango, kwani baadhi ya watumishi wa afya tayari wamesimamishwa kazi ili taratibu za kisheria zichukue mkondo wake, na kuwa wataalamu wanapaswa kufanya kazi kwa mujibu wa miongozo inavyowataka, kwani kamwe Halmashauri yake haitawavumilia watumishi wazembe na wanaofanya kaziu kwa kujitakia.

"Cha msingi bodi inatakiwa kuacha kuketi katika ofisi na kusubiri kupokea taarifa, kama bodi itakaa katika ofisi na kusubiri taarifa hapo mjue hakuna mabadiliko yoyote katika sekta ya afya, msingi bodi mnatakiwa kuwa makini kwa kutembelea katika vituo husika vya afya na zahanati, lakini mnapaswa mfanye kazi kwa kuangalia hali halisi namna huduma zinazotolewa na usahihi wa dawa zinazoagizwa na kufika kwenye vituo," Alisema Mhapa.
 
Nao wadau wa bodi hiyo wamesema kukosekana kwa vifaa tiba, zikiwemo dawa za wagonjwa katika vituo vya afya, kunatokana na baadhi ya wataalamu wa idara ya afya kutokuwa waaminifu kwa kuchepusha dawa na kuzipeleka katika mifumo isiyo rasmi, jambo linalosababisha wagonjwa wengi kukosa matibabu.

Nuhu Chorobi mjumbe wa bodi hiyo ya afya kutoka kijiji cha Kidamali Wilaya ya Iringa amesema uelewa mdogo juu ya utambuzi wa upataji wa huduma bora bado ni changamoto kubwa kwa wananchi, na kuwa kupitia bodi hiyo wananchi watapata mafanikio kwa kasi kwa kushirikiana na wananchi wenyewe, ikiwa pamoja na kamati za vituo husika kuwa imara kwa kutambua wajibu wao.

"Kamati zitakapokuwa imara hata huduma za afya zinakuwa bora, lakini wananchi wanatakiwa kuchagua wajumbe wa kamati walio na weredi na ambao wanatambua wajibu wao, kwani wananchi mategemeo yao makuu ni kupata huduma bora za afya," alisema Chorobi.

Blandina Mkumbwike mratibu wa huduma ya afya ya jamii Wilaya ya Iringa amesema uelewa duni miongoni mwa wananchi ni changamoto inayokwamisha baadhi yao kutojiunga na mfuko wa afya ya jamii CHF, kwa kuwa uwezo wa kulipia kiwango cha fedha husika wanao, ila wanakosa elimu juu ya mfuko huo namna unavyofanya kazi.

Mkumbwike amesema tatizo la baadhi ya wananchi kutojiunga na mfuko wa CHF linatokana na hofu juu ya baadhi ya dawa kutotoshereza na hivyo kushindwa kuwafikia kwa kiwango sahii, huku wizara ikishindwa kufikisha dawa kwa wakati katika maeneo husika kutokana na bajeti finyu, na kuwa changamoto ya uchache wa dawa itamalizika endapo tu wananchi watajiunga kwa wingi na mfuko huo.

Akitoa ufafanuzi wa udhibiti wa dawa za wagonjwa, mkuu wa Wilaya ya Iringa Dr. Retisia Warioba amesema bodi hiyo inatakiwa kuleta ufanisi kwa kuboresha huduma ya afya ikiwa pamoja na kudhibiti wizi wa dawa, ili kuwezesha upatikanaji wa dawa kwa wananchi.

Dr. Warioba ameitaka bodi kuwa na uaminifu ili kuleta tija katika huduma ya afya, ikiwa pamoja na kuwashawishi wananchi kujiunga na mfuko wa afya ya jamii.
Hata hivyo hakimu mkazi wa Wilaya ya Iringa, Aloyce Masua akitoa kiapo cha utii kwa wajumbe wa bodi hiyo amesema uadilifu katika kazi ni nguzo muhimu katika kufikisha huduma bora kwa wananchi, huku mganga mkuu wa Wilaya ya Iringa Dr. Ignas Mlowe akisema changamoto ya ukosefu wa dawa ni kubwa katika vituo vya kutolea huduma ya afya, na hiyo ni kutokana na maeneo mengi ya wilaya hiyo wananchi wake kusumbuliwa na ugonjwa wa Malaria.
 
 
MWISHO

 

No comments:

Post a Comment