Wednesday, October 9, 2013

MTUHUMIWA WA UTEKAJI WA MAGARI NA WIZI WA MAFUTA AKAMATWA

Bango la kampuni ya E.  Awadh & Co. LTD ambayo moja ya gari lake limetekwa na kuibiwa mafuta, huku dereva wake na utingo wakifanyiwa ukatili mkubwa na WATEKAJI hao katika eneo la Igumbilo mjini Iringa.
 Viongozi wa Kampuni ya Edha Awadh Company Ltd, kushoto ni ofisa usalama wa kampuni Bw. Maridady Ndalo kutoka jijini Dar es Salaam, akiwa na mwakirishi wa kampuni hiyo mkoa wa Iringa Bw.  Abubakary Shadry wakiwa eneo la Mahakama ya Rufaa Mkoa wa Iringa wakifuatilia kesi hiyo ya Utekaji, huku jeshi la polisi likiwa limefanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja na kuendelea kutafutwa watekaji wengine saba, waliohusika katika tukio hilo.
Nukushi ya Kampuni ya E.Awadh & Co. LTD, inayojihusisha na shughuli za usafirishaji wa mizigo mbalimbali, yakiwemo mafuta, Shaba nk.

JESHI la Polisi mkoani Iringa limefanikiwa kumtia nguvuni mtuhumiwa wa utekaji wa magari mkoani Iringa, Gwelino Gasper Mtonyole almaarufu kwa jina la Rais mkazi wa kijiji cha Nyololo kilichopo wilayani Mufindi mkoani Iringa, baada ya kukutwa na mapipa 15 ya mafuta yanayosadikiwa kuwa niya wizi.
 
Akizungumzia tukio hilo kamanda wa jeshi la Polisi mkoani Iringa ACP Athman Mungi amesema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kunatokana na tuhuma za kufanya unyang’anyi wa kutumia silaha, na kisha kumteka dereva pamoja na utingo wake wa gari la kusafirisha mafuta.
 
Kiongozi huyo wa matukio ya utekaji wa magari anatuhumiwa kushiriki kuliteka roli aina ya Scania lililokuwa likisafirisha mafuta aina ya Disel kutoka jijini Dar es Salaam kwenda Ndola Zambia, ambapo waliliteka gari hilo baada ya dereva kuteremka kwa lengo la kuangalia hitirafu zilizokuwa zikijitokeza na kusababisha gari kufuka moshi.
 
Kamanda wa Jeshi la Polisi ACP Athman Mungi alisema tukio hilo lilitokea maeneo ya Igumbilo, barabara ya Iringa Dar es Salaam, manispaa ya Iringa, ambapo watu nane walimvamia dereva na utingo wa gari hilo na kisha kumfunga kamba usoni na miguu na kisha kumterekeza katika jengo ambalo halijaisha( Pagare).
 
Mungi alisema harakati za kumsaka kiongozi huyo wa shughuli za utekaji wa magari mkoani Iringa zilifanikiwa baada ya gari hilo kukutwa likiwa limetelekezwa Makambako huku mapipa 15 ya mafuta aina ya disel ambayo yalikutwa nyumbani kwake yakidhaniwa kuwa niya wizi, pamoja na mitambo mbalimbali ya kuvutia mafuta.
 
Mungi alisema mtandao huo unasakwa ili kudhibiti tabia za utekaji wa magari na kuwa tukio hilo nila pili kutokea katika kipindi cha mwezi mmoja na jeshi linajinoa kutokomeza matukio ya aina hiyo.
 
Dereva wa roli hilo lenye namba za usajili T945 CAS na tela lake lenye namba T215 CFQ Scania mali ya kampuni ya Edha. Awadh. Co. Ltd, Hassan Ally Mwapili (38) ambaye amenusurika kufa katika tukio hilo, amesema alipigwa kwa marungu, mabegani, kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wake huku akiwa chini ya ulinzi na kuingizwa kitambaa mdomoni na kisha kufungwa kitambaa kingine usoni.
 
"Niliteremka mimi na utingo wangu Mohamed Ungele ili kuona gari kwa nini linafuka moshi, na nikiwa naangalia Pipe yenye hitirafu mara nilisikia sauti ya mtu mmoja ikisema "Chini ya ulinzi' kugeuka mtu huyo alikuwa ameshika Panga na rungu akanipiga na rungu begani, kichwani na sehemu mbalimbali za mwili wangu, Mohyamed kuona vile alishuka chini na kufuata amri ya mtu huyo, na mimi nikiwa chini ya ulinzi huo mara nilisikia yule mtu akiita "Makamanda njooni" Wakaongezeka watu wengine saba na kunikamata na kunifunga kamba miguu na mikoni na wakanigeuza kifudifudi na kunifunga kitambaa kingine Usoni na wakanigeuza tena nikalalia mgongo na kunisindilia kitambaa mdomoni," Alisema Hassan.
 
Alisema watekaji hao walikuwa na silaha za aina mbalimbali yakiwemo mapanga, marungu na bastola waliendelea kumfanyia unyama, huku baadhi yao wakifanya mawasiliano kwa njia ya simu na hapo walimnyanyua na kumpeleka katika eneo ambalo hakulifahamu na kutulaza kwenye majani.
 
"Walikuwa wakinitaka niwape hela nikawaambia mimi sina hela, wakanisachi mfukoni na kuchukua Simu nne, nokia tatu na moja ilikuwa aina ya Sumsung, na muda wote walikuwa wanitupiga huku wakinitaka niwaeleze hela na funguo zipo wapi, nilipozidiwa niliwaeleza kuwa hela zipo kwenye gari, na funguo ilikuwa mlangoni.ambapo hela hizo dola 300 zilikuwa niza kuvushia gari mpakani (Boda).
 
Mwapili aliendelea kueleza kuwa baada ya kutoa maelezo hayo ya fedha na funguo watekaji hao walimnyanyua na kuondoka nae, wakielekea asikokujua, lakini ilikuwa ni polini zaidi, na mara baada ya kuwafikisha huko walisikia muungurumo wa gari, ndiyo walikuwa baadhi yao wakiondoka nalo eneo hilo.
 
"Tukiwa huko na utingo wangu, waliendelea kutupiga na kutueleza kuwa wanatumaliza ili kupoteza ushahidi, huku mwingine akisikika akisema "Bosi akisema mzigo upo poa tutawaacheni, lakini sio tuliokuwa tunawasubiri nyinyi, ila mmeingia kwenye chanel tu, tulikuwa tunalisubiria gari lingine", wakamchukua mwenzangu na kuondoka nae, wakisema huyo mpelekeni kule Site mkamalize kazi, sisi tunabaki na huyu, wakaniwekea jiwe kubwa kifuani, hapo roho yangu ikafa ganzi juu ya uhai wangu kwani nilijua mwenxangu anapelekwa kuuawa na mimi ndiyo kifo changu kinanifuata, mara nikasikia sauti za wale walioondoka na utingo wangu wakija, kumbe hapo ndiyo walikuwa wanapeana ishara ya kuondoka, nikaona kimya kwa muda," Alisema Mwapili.
 
Alisema baada ya muda mfupi akasikia kishindo na kudhani wamerudi tena watekaji, kumbe hapo alikuwa yule Utingo wake, ambaye alimueleza kuwa amejinusuru na kujitoa kamba, na hapo ndipo akapata msaada wa kusaidiwa na utingo kufunguliwa kamba za mikononi na miguuni na kuondolewa jiwe la kifuani.
 
Alisema utingo wake alikwenda barabarani ambapo ilikuwa ni majira ya saa kumi na mbili kasoro alfajiri na kuomba msaada kwa wapita njia na kubahatika kupata IT ambapo utingo huyo alimueleza dereva juu ya mkasa na kuomba msaada wa usafiri ambapo dereva huyo wa gari la IT alifika hadi katika eneo la tukio na kwa kusaidiana na utingo kumbeba na kumuweka katika gari hadi katika kituo cha ukaguzi wa magari "Check Point" cha Igumbilo.
 
Mwapili alisema askari wa eneo hilo walimsaidia kumtoa tambala alilosindiliwa mdomoni, na kwakuwa hali yake ilikuwa mbaya alikimbizwa Hospitali ya mkoa wa Iringa ambako alilazwa kwa siku tatu, na kuruhusiwa baada ya kupata nafuu.
 
Mwakilishi wa kampuni hiyo ya E. Awadh. Co. Ltd mkoani Iringa, Aboubakari Shadri alisema zaidi ya lita 25,000 za mafuta hayo hayajulikani yalikoshushwa au kuuzwa na wanyang’anyi hao na kuwa thamani ya mafuta hayo ni zaidi ya Sh Milioni 80.
 
Mkuu wa ulinzi wa kampuni hiyo, Ndalo Maridadi alisema baada ya kupata taarifa hizo waliwasiliana na wakala wao wa GPRS ili kujua mwenendo wa gari kutoka Igumbilo Iringa.
 
"GPRS walitupa picha, ramani na vituo vyote liliposimama gari, ambapo Nyololo lilisimama kwa masaa mawili na nusu nje ya nyumba ya mtuhumiwa huyo," alisema Ndalo.
 
Aidha alisema kwa kutumia picha na taarifa za GPRS, Polisi walifanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na mafuta zaidi ya lita 4,000 yaliyoibwa katika roli hilo, ambapo taarifa za kimahakama zinasema mtuhumiwa amefunguliwa kesi ya jinai namba 228/2013; Septemba 21, na atafikishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Iringa kujibu mashtaka yanayomkabiri.
 
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa Ramadhani Mungi, alisema wakati mtuhumiwa akikamatwa nyumbani kwake Nyololo alikutwa na zaidi ya lita 4,000 za mafuta hayo zikiwa zimehifadhiwa katika mapipa makubwa 15.
 
Na kuwa gari hilo hadi linapatikana Septemba 21 mwaka huu, likiwa limeterekezwa huko Makambako, mkoani Njombe, hilo lililokuwa limepakia lita 36,000 zenye thamani ya shilingi Milioni 72 huku gari hilo lilmekutwa likiwa limebakiwa na lita 6,000 pekee.
 
Kamanda Mungi amesema wamefanikiwa kumkamata mtuhumiwa huyo Gwelino Gasper Mtonyole (49) mfanyabiashara na mkazi wa Nyololo ambaye alikutwa nyumbani kwake akiwa na mapipa 15 ya mafuta ya Diesel yaliyoibwa katika roli hilo, ambapo alikutwa akiwa pia na mashine mbalimbali za kunyonyea mafuta.
 
Mungi amesema jeshi la polisi linaendelea na msako ili kuwakamata watuhumiwa wengine saba waliobaki, ili kudhibiti tatizo hilo la utekaji wa magari ambao unalengo la kuchafua sifa ya utulivu wa mkoa wa Iringa.
 
Hata hivyo mtuhumiwa huyo amefikishwa katika Mahakama ya Rufaa mkoa wa Iringa, na kufunguliwa kesi ya jinai namba 228/2013; na atafikishwa tena mahakama tarehe 21 mwezi huu Octoba kwa hakimu mkazi Iringa kujibu mashtaka yanayomkabiri.
MWISHO

No comments:

Post a Comment