Moja ya mashine za kutolea mipira ya kiume Kondom- ATM Mashine ambazo zimewekwa katika maeneo mbalimbali ya starehe ili kurahisisha upatikanaji wa zana hizo, lengo likiwa ni kuzuia maambukizi mapya ya Virus Vya Ukimwi- VVU.
Jengo la halmashauri ya Wilaya ya Kilolo-m Mkoani Iringa
KUKOSEKANA kwa mashine za kutolea mipira ya kondomu za kike,
ikiwa pamoja na kondomu hizo kutopatikana kwa urahisi, kumeifanya jamii ione
serikali inawajali zaidi wanaume kwa kuwalinda kuliko kundi la wanawake ambao
wamekuwa waathirika wakubwa wa ugonjwa huo.
Farida Shirima mmoja wa wananachi mkoani Iringa amesema
wanaume wamepewa kipeumbele katika kulindwa, kwa kutengenezewa mashine maalumu
zinazotoa huduma ya kondomu hizo “ATM Kondom Mashine” huku kila eneo zana hizo zikipatikana kwa urahisi, hali
ambayo ni tofauti kabisa na upande wa kondom za kike ambazo hata katika baadhi
ya vituo vya huduma za afya hakuna.
Nao madiwani wa halmashauri ya Wilaya ya kilolo, wakati
wakijadili masuala mbalimbali ya maendeleo na uchumi, vikiwemo vikwazo vya
maendeleo kama ugonjwa wa ukimwi, wamesema ipo haja kwa serikali kuagiza
kondomu za kike ili nazo zipatikane kwa wingi na hivyo wanawake kuwa na fulsa
katika kujikinga na magonjwa ya zinaa na ukimwi.
Wakizungumzia hali hiyo madiwani hao wamesema upatikanji wa
mipira hiyo ya kike ni shida tofauti na kondomu za kiume ambazo licha ya
kupatikana kila mahali pia imetengenezewa mashine maalumu kwa ajili ya kutoa
huduma hiyo “ATM Kondom Mashine” ambazo zimewekwa katika maeneo mbalimbali ya
Starehe.
Akilalamikia hatua ya kukosekana kwa Kondomu za kike katika
maeneo yaliyo mengi, mmoja wa madiwani Anna Kulanga amesema serikali imewekeza
nguvu zake nyingi katika kondomu za kiume kwa kuhakikisha zinapatikana kwa
urahisi, huku kondomu za kike zikisahaulika na kuwa nadra sana upatikanaji wake.
Kulanga amesema tatizo hilo linachangia wanawake kushindwa
kujikinga na maambukizi mapya ya VVU, kutokana na kukosa zana hizo, ambazo zimesahaulika
baada ya serikali kuelekeza nguvu zake kwa kutenga bajeti katika mipira hiyo ya
kiume.
“Mh. Mwenyekiti sisi wanawake katika kitengo hiki cha ukimwi
inaonekana kama tumesahaulika, maana hata unapokwenda katika vituo vya afya ya
uzazi unapatiwa kondomu za kiume, wakati matumizi ya mipira hiyo ni hiyari ya
mwanaume, atumie au laa, tunaitaka serikali ione kuna haja kubwa ya kutenga
bajeti ili kuzifanya kondomu za kike zipatikane sawa kama zilivyo vya kiume,”
Alisema Kulanga.
Aidha amesema wanawake waliowengi wanajikuta wakilazimika kufanya
mapenzi bila kinga, na hivyo kuangamia kwa kupata maambukizi ya Virusi vya
Ugonjwa wa ukimwi, kwa madai kuwa baadhi
ya maeneo ya vijijini bado kuna tabia ya mfumodume wa wanaume kuwa na wanawake
wengi.
Naye mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo Joseph
Muhumba amesema tatizo hilo ni kubwa kwani hata ofisi zilizo nyingi katika vyoo
kumewekwa huduma hiyo ya kondomu za kiume pekee na kuitaka Halmashari kutenga
bajeti ya fedha za kununulia zana hizo za kuwalinda wanawake na ukimwi.
“Kweli hili ni tatizo kubwa, ipo haja kwa serikali kuona
umuhimu wa kutenga bajeti ili kuliokoa kundi hili la wanawake, nao wawe na
maamuzi ya kutumia zana zao au laa, kama ilivyo kwa wanaume, tunasema wanawake
ni jeshi kubwa na ukiwaelimisha wao umeielimisha jamii, basi ipo haja kuwalinda
kwa kuona hawaangamii kwa ukimwi,” Alisema Muhumba.
Mratibu wa shughuli za Ukimwi Wilaya ya Kilolo Faraja Chaula
alikiri kuwepo kwa uhaba wa mipira hiyo ya kike, na kuwa hata elimu juu ya
matumizi yake bado haijawafikia wanawake walio wengi.
Chaula amesema katika kukabiliana na hali hiyo Halmashauri
tayari imetenga bajeti ya kununua kondomu za kike katoni 109, ikiwa pamoja na
kutoa elimu sahihi ya matumizi ya zana hizo,ili kuwakinga wanawake na VVU.
“Ni kweli katika shughuli za mapambano ya ukimwi wanawake
ndiyo wahanga, hasa kutokana na shughuli wanazofanya ukizingatia ndiyo wenye
majukumu makubwa ya kulea familia, lakini hawana maamuzi katika suala la
mapenzi na changamoto kubwa kwao ni uhaba wa Kondomu za kike, lakini kwa
kuanzia Halmashauri tumetenga bajeti ya kununua kondomu hizo za kike pamoja na
kutoa elimu ya matumizi ya kondomu hizo,” Alisema.
MWISHO
No comments:
Post a Comment