Sunday, January 27, 2013

KAGASHEKI AWATIMUA KAZI MAMENEJA 6 WA MSITU WA TAIFA SAO HILL- AFUTA VIBARI FEKI ZAIDI YA 200


 Waziri wa maliasiri na utalii Mh. Khamis Kagasheki  akiwa na kaimu mkuu wa Mkoa wa Iringa Dr. Letisia Warioba, ambaye ni mkuu wa Wilaya ya Iringa.
 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Mh. Steven Mhapa akiwa na mkurugenzi wa Manispaa ya Iringa, Bi. Teresia Mahongo, katika kikao cha Waziri Kagasheki na viongozi mbalimbali wa mkoa wa Iringa, kabla waziri hajaenda Wilaya ya Mufindi.

  


Viongozi mbalimbali wa mkoa wa Iringa wakiwa katika eneo la Msitu ktika kijiji cha Kibengu katika Wilaya ya Mufindi, kuangalia maeneo yenye migogoro, katika ziara ya siku mbili ya Waziri wa maliasiri na utalii, Barozi Khamis Kagasheki.
 Waziri Kagasheki akipata maelezo kutoka kwa mbunge wa jimbo la Mufindi Kaskazini Mh. Mahamoud Mgimwa, kutokana na kupewa ramani inayotoa maelezo ya msitu huo.
 Meneja mpya wa Shamba la Taifa la Sao hill, Bw. Salehe Beleko (aliyenyoosha kidole) akieleza jambo kwa viongozi waliofika wilayani humo na Waziri kagasheki kupata ufafanuzi wa mgogoro wa msitu huo wa Taifa.


 WAZIRI wa maliasili na utalii Khamis Kagasheki ameiondoa madarakani kamati ya shamba la miti, la Taifa la sao hill lililopo katika wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, baada ya kutambua ubadhirifu katika kitengo cha ugawaji wa vibari vya uvunaji miti wa shamba hilo.

Kagasheki amechukua hatua hiyo, baada ya wananchi wilayani humo, kumlalamikia juu ya urasimu wa kupata vibari, huku asilimia kubwa ya wananchi wa Mufindi wakikosa fulsa hiyo na kubaki walinzi na vibarua wa shamba hilo.

Wakizungumza katika mkutano wa wadau wa msitu uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya wilaya ya Mufindi, wananchi wamwambia waziri kuwa shamba hilo hawanufaiki nalo kwani  licha kuwepo katika Wilaya yao, wamekuwa wakitumiwa kama vibarua na walinzi huku vibari wakipatiwa watu wan je na wilaya hiyo.

“Waziri ujio wako nadhani utakuwa ni msaada juu ya kilio chetu cha siku nyingi, hapa tuinahujumiwa sana, ardhi ile iliyopandwa miti, ni mali yetu sisi wana Mufindi, wazazi wetu waliitoa kwa serikali ili iwanufaishe wananchi wa Mufindi na Taifa zima, lakini kuna watu wanaitumia ardhi hiyo kanakwamaba ni mali yao binafsi, sisi hapa unapotuona hatuana hata kibari kimoja, lakini kuna watu wanatumia majina ya ndugu zao wenye madaraka wanamiliki vibari zaidi ya viwili,” Alisema Methord Matekeleza.

Naye Godwin Kidulile alisema endapo viongozi wa msitu huo wangetoa fulsa kwa wananchi wa Mufindi kwa kuwapatia vibari mgogoro huo haungekuwepo, lakini vibari hivyo vya uvunaji vinatolewa kwa upendeleo mkubwa na hivyo wazawa kubaki kama vibarua katika shamba hilo.
Isack Sika mchungaji wa kanisa la AIC alisema yeye na wazazi wake walichukuliwa kama manamba ili kupanda miti iliyopo katika shamba la sao hill, lakini kitendo cha kunyimwa umiliki wa kibari cha uvunaji miti kunamfanya ajisikie vibaya kwani hana analonufaika na msitu huo.

Fermina Msaki alisema watu wamekuwa wakitoka mikoa mbalimbali na kupatiwa vibari licha ya baadhi yao kutojua hata matumizi yake, na kuamua kuviuza kwa gharama kubwa na kunufaika na msitu huo, huku wakazi wilayani humo wakinyimwa.

Alisema kuna baadhi ya wananchi wanapata vibari kutokana na majina makubwa ya ndugu zao na wale wasio na ndugu wenye uwezo huo wakibaki kuwa watazamaji wa msitu huo na mbao namna zinavyosafirishwa.

Wananchi hao walisema Wilaya ya Mufindi ambayo niya pili kwa kuwa na mapato makubwa lakini wananchi wake ni masikini kutokana fulsa hizo za kiuchumi kumilikiwa na wananchi wa nje ya Wilaya yao, huku wachache wenye uwezo wakilazimika kununu kwa gharama kubwa kwa watu waliopatiwa vibari.

"Awali tuliambiwa kigezo kkikubwa tujiunge katika vikundi, na pia tuwe na mitambo na mashine za kupasulia mbao, vyote hivyo tumetimiza, lakini cha ajabu kila tunapojaza majina yetu kwa ajili ya kupata vibari vya uvunaji tunaokosa na kuyaona majina ya watu ambaoi wala siyo wakazi wa Mufindi, hili jambo Waziri endapo litafumbiwa macho itatulazimu msitu huo kuuterekeza, hatuwezi kugeuzwa walinzi wakati hatunufaiki chaochote, ukianza moto kwenye shamba sisi ndiyo wa kwanza kutuchukua tukazime, wakati wanaonufaika ni watu wengine, tumechoka,” Walisema.

Akitoa majibu ya malalamiko ya wananchi hao, Kagasheki alisema licha ya kilio hicho cha wananchi, pia ameona changamoto mbalimbali, zinazowanyonya wananchi hao.

“Nimesikia yote mliyonielkeza, lakini nimeyaona mengi nilipokuwa huko, kuna vibari vimeombewa kwa ajili ya kuvuna Mikaratusi, lakini unakuta miti iliyovunwa ni Paina, lakini pia kuna hivi wanaviita Viunga, vinaonyesha kama vimegawiwa kwa wananchi, lakini wananchi hawajapewa,” Alisema.

“Unakuta muombaji mmoja anavibari zaidi ya kimoja hadi viwili, lakini picha ni ile ile ya mtu moja, hata kama ni makosa mengine ni makusudi na matusi kwa Taifa,hata kama unamtetea mtu, hapo hebu nipe sababu ya mtu huyu kuwa nisimfukuze,jana nilitamka na leo ninatamka, kamati ya mgao iliyokaa sasa na meneja wa Sao hill, meneja msaidizi na mameneja wanne wa tarafa za msitu nimewasimamisha kazi, Kwani kamati hii haiwezi ikatenda haki, ni familia moja,”  Alisema

Kagasheki alisema amechukua uamuzi huo kwa viongozi hao kwa kuwa wao ndiyo  wanahusika kusimama kazi ya ugawaji wa vibari vya uvunaji miti katika msitu  huo wa Sao hill, huku akisema “kati ya watu 561 ya watu walioomba vibari kati yao  269 ndiyo walikuwa na vibari rasmi na waliobaki hawakuwa na vibari vyao ninavifuta, kwani walilolifanya haliwezi kuwa ni bahati mbaya,” Alisema.

Wakati akizungumza na viongozi wa mkoa wa Iringa katika ofisi ya katibu tawala Kagasheki alisema udhaifu kwa baadhi ya watumishi katika Wizara yake, unatokana na tama ya rasilimali zilizopo katika Wizara hiyo huku baadhi yao wakiamua kujitia muhanga ili kuzipata mali hizo.

Alisema baadhi ya watumishi katika wizara hiyo ni chanzo cha migogoro na utendaji kazi mbovu, hasa katika kipengere cha kumiliki  vibari vya uvunaji wa  rasilimali mbalimbali na kuwa  lengo kuu la ziara yake mkoani Iringa ni  kusikiliza malalamiko ya  wananchi wa Mufindiu juu ya mgogolo wa umiliki wa vibari vya uvunaji wa miti katika shamba hilo la Taifa la Sao hili.

Pia alisema, wizara hiyo bado inachangamoto mbalimbali kutokana na uwepo wa mtandao mkubwa unaoundwa na baadhi ya watumishi wa wizara ya maliasiri na utalii  kwa kushirikiana na wafanyabiashara.

“Mtandao huu ni mkubwa sana, ndani ya miezi saba tu niliyokaa katika wizara hii ya maliasiri na utalii , nimeona mengi, ndiyo maana baadhi ya watumishi wapo radhi kujitoa muhanga hata kufukuzwa kazi, ili kutekereza adhma yao, lakini jambo hili limeanza kushughulikiwa, hii mali ya asili hii kupata vibari vya uvunaji kuna tatizo, watu wanasigana, wanavutana, lakini adhma ya ujio wangu ni kutatua matatizo haya,” Alisema Kagasheki.

Alisema matatizo yapo ndani ya wizara ya utalii, kutokana na uwepo wa mtandao mkubwa, huku baadhi yao wakiwinda, wengine wakisafirisha na wengine wakiuza, lakini kupitia vyanzo vya wananchi wamefanikiwa kuwapata viongozi wakubwa wanaojihusisha katika mtandao huo(Ring leaders).

Akisoma taarifa ya sekta ya maliasili na utalii mkoa wa Iringa kaimu katibu tawala mkoa wa Iringa Wamoja Ayubu alisema maeneo ya hifadhi yenye mgogo wa mipaka na wadau mbalimbali ni pamoja na shamba la Taifa la Sao hill hasa katika vijiji  vinavyolizunguka shamba hilo.

Wamoja alisema vijiji vyenye migogoro na shamba ni pamoja na Itimbo, Wami, Ugesa, Vikula, Usokami, Kibengu, Mfukulembe na kijiji cha Udumuka na kuwa mkoa kupitia kamati za ushari umeanza kulishughulikia tatizo hilo.

Mgogoro huo wa ugawaji wa vibari umedumu kwa muda mrefu, huku wananchi wakilalamikia uwepo wa baadhi ya watu kumiriki  vibari vingi , huku wazawa wa Wilaya hiyo ya mufindi wakikosa fulsa hiyo na hivyo kujikuta wakiwa watumwa ndani ya ardhi yao, na hatua hiyo inaweza kuwa ni muarobaini wa tatizo hilo.
MWISHO

No comments:

Post a Comment