Mwenye shati ya Njano, ndiye katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi Bw. Jackob Nkomola alifikishwa mahakamani kwa tuhuma ya kutishia kuua, na baadaye kumfanyia vurugu mmiliki wa mtandao huu wakati akitimiza majukumu yake ya kihabari Mahakamani hapo.
Jengo la Mahakama ya Mwanzo Wilayani Mufindi.
Mtuhumiwa wa kesi ya kutishia kuua, ambaye ni katibu wa CCM Wilaya ya Mufindi Bw. Jackob Nkomola akiwa nje, ya mahakama licha ya kutotimiza masharti ya dhamana, ambapo alipata mwanya wa kumfuata mmiliki wa mtandao huu na kumkuda, akizuia kupigwa picha.
KATIKA hali isiyo ya kawaida, katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mufindi Jackob Nkomola amefanya vurugu katika Mahakama ya Mwanzo ya Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa , kwa kumvamia Mwandishi wa habari kwa kile alichokiita ni hasira ya kesi yake.
Tukio hilo limetokea leo majira ya saa tatu na nusu katika Mahakama ya Mwanzo iliyopo katika Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa, baada ya katibu huyo kusomewa shtaka na hakimu wa Mahakama hiyo ya mwanzo Mh. Zakaria Mushi.
Akisoma shtaka hlililomfikisha mahakamani hapo hakimu Mushi amesema mtuhumiwa Jackob Nkomola anashtakiwa kwa kosa la kutishia kuua kwa maneno,na kuwa ni kesi ya kwanza katika mwaka huu 2013 na hivyo kuvunja sheria kifungu namba 89 kifungu kidogo “A”.
Aidha hakimu huyo aliieleza mahakama kuwa mshitakiwa alitenda kosa hilo, siku ya tarehe 3 mwezi wa kumi mwaka 2012 katika eneo la Mkombwe, ambapo alimtishia Alexandel Tweve mkazi wa Mafinga.
Mtuhumiwa alikana shtaka hilo na hakimu kutoa masharti ya dhamana ya ahadi ambayo inathamani ya shilingi Laki mbili, na adhaminiwe na mtu mmoja atakayetambulishwa kwa barua kutoka katika ofisi ya serikali ya kijiji au Kata.
Kupitia masharti hayo mshatakiwa alikuwa na mdhamini ambaye hakukidhi vigezo vya kuwa na barua ya uthibitisho kutoka katika ofisi za serikali ya kijiji na hivyo kuzuiliwa kwa muda wa saa moja akiwa chini ya ulinzi, hadi kesi itakaposikilizwa tarehe 30 mwezi huu wa kwanza 2013.
Hakimu alimtaka mstaki wa kesi hiyo kufika na mashahidi wake aliowaorodhesha, na baada ya mwandishi wa MTANDAO huu, Televisheni ya Star TV na vyombo mbalimbali anavyovifanyia kazi kutoka nje kwa ajili ya kupiga picha, mtuhumiwa alinifuata kunikuda akihoji ridhaa ya kupiga picha.
“Kwa nini unanipiga picha?? Nani amekuruhusu unipige picha, kwanza wewe ni nani??, umepokea rushwa huko uje uniandike mimi, na nitaona kama habari hiyo itatoka,” Alihoji Katibu huyo.
Nilimjibu kuwa “Mimi ni mwandishi wa habari, nimepata ruhusa kutoka kwa hakimu wa mahakama hiyo kuifanya kazi yangu, na sijampiga picha yeye, bali nilikuwa ninapiga picha ya kibao cha mahakama na jengo,”.
Hatua hiyo iliwashangaza watu waliohudhuria kesi hiyo katika viunga vya mahakama hiyo, wakihoji mamlaka ya mtuhumiwa kumfuata umbali wa hatua zaidi ya tano mwandishi, huku mtuhumiwa akiwa chini ya ulinzi kwa kuwa bado alikuwa naashikiriwa na Mahakama hiyo kwa kutokidhi vigezo vya dhamana yake.
Nilikimbilia kwa hakimu wa mahakama hiyo kutaka msaada juu ya tukio hilo, na ndipo hakimu Mushi alinitaka kufika katika kituo cha polisi kutoa taarifa ya tukio hilo.
Nikiwa njiani nilipata wazo la kumpigia simu Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mufindi Bw.Cosmas Kaguo na kumueleza juu ya tukio hilo na kuniomba nionane naye kabla ya kufika katika kituo cha Polisi cha Mafinga.
Hatua ya mwenyekiti wa CCM Kaguao, - pia iliambatana na kuitisha kikao cha dharua cha kamati ya siasa na kuomba radhi juu ya tukio lililotokea, na baada ya muda dakika 20 Katibu huyo wa CCM (Mtuhumiwa) aliingia katika moja ya ofisi ya Halmashauri hiyo ya Wilaya ya Mufindi, iliyopo katika ukumbi wa mikutano na kuomba radhi juu ya kile alichokifanya katika viunga vya mahakama.
Ombi la mwenyekiti wa CCM Wilaya, nililikubalia kwa hatua za kutofungua kesi katika kituo cha polis, na hatua za kihabari ili kuijulisha jamii kilichotokea zikiendelea.
Pia niliwafahamisha wahariri wangu wa vyombo ninavyofanyia kazi, huku baadhi yao wakifanya mazungumzo ya live katika kikao hicho kupitia simu za mkononi.
Akitoa utetezi wake, mtuhumiwa huyo alisema “Ninaomba unisamehe sana Oliver, unajua kesi yangu hii niya kisiasa, na kukufanyia hivyo ni hasira baada ya mtu anayenituhumu kutumia njia mbalimbali za kuniangamiza, ninajua nimekukwaza wewe, lakini pia nimeidhalilisha taaluma yako, ninakuomba unisamehe,” Alisema Nkomola.
Hata hivyo wachagizaji wa masuala ya siasa Wilayani humo walisema katibu huyo amekuwa akitumia vibaya wadhfa alionao, na kujisahau kama kuna mikono ya sheria , na kuwa nguvu ya kufanya vurugu katika chombo hicho cha mahakama ambacho ni muhimili mkuu wa serikali, ni kutokana na jengo la Mahakama hiyo kuwa ni mali ya chama cha mapinduzi(CCM).
“Angekuwa mtu mwingine aliyefanya vurugu Mahakamani angechukuliwa hatua pale pale, kufanya fujo mbele ya mahakama, tena mahakimu wanaona, si jambo la mdhaha, ni kuidharau Mahakama, laki amefanya vile kwanza akijua yeye ni kiongozi mkubwa wa chama Wilayani humo, lakini pili, ni juu ya jengo lao, anaona kama anayo haki ya kufanya chochote yeye kama baba mwenye nyumba wa Mahakama hiyo, lakini si sifa ya kiongozi bora hata kidogo, na kusema nitaona kama habari hiyo itatoka inamaa yeye ndiyo anayezuia na kuruhusu habari?, anataka kutwambia yeye ndiyo mratibu au mhariri wa vyombo vyote vtya habari!!” Walihoji.
Kikao hicho cha usuruhishi dhidi ya tukio hilo, kilichukua zaida ya saa nzima hadi kumalizika kwake.
Mmiliki wa mtandao huualiipta tetesi ya habari ya kesi hiyo, akiwa na ziara ya kikazi ya siku tatu kufuatilia masuala ya elimu wanafunzi wanaoanza kidato cha kwanza na darasa la kwanza, pamoja na kujua changamoto zinazoikabiri sekta ya elimu na Kilimo Wilayani humo.
MWISHO
No comments:
Post a Comment