Sunday, January 13, 2013

VYUO VIKUU WAANDAMANA KUPINGA GESI KUSAFIRISHWA

Wanafunzi wa vyuo vikuu mkoani Iringa wakiingia katika bustani ya manispaa ya Iringa, kutuimiza azma yao ya kuwaunga mkono wananchi wa mkoa wa Lindi na Mtwara kupinga vikali hatua ya serikali kutaka kusafirisha gesi asili kwenda jijini Dar es Salaam.



Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo cha RUCO Bw. Willium Lufili akitoa neno katika mkusanyiko wa wanachuo wanaotokea mikoa ya Lindi na Mtwara, ambao wanasoma mkoani Iringa.
Wanachuo wa vyuo vikuu mkoani Iringa wakiimba wimbo wa kupinga zoezi la kutaka kuisafirisha gesi asili.



Bw. Juma Chilavi mwakirishi kutoka katika chuo kikuu cha Tumaini naye akitoa neno katika mkusanyiko huo.


Bw. Namangaya Mhaji (Mwenye suti) Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya wanafunzi wanaotokea mikoa ya Lindi na Mtwara, akiteta na mwanazuoni katika bustani ya manispaa ya Iringa.




 


WANAFUNZI wa vyuo vikuu vilivyopo mkoani Iringa ambao wanatoka katika mikoa ya Kusini ya Mtwara na Lindi, wameendeleza sakata la mjadala wa kupinga vikali gesi asili ya Mnazi Bay kupelekwa Jijini Dar es Salaam, wakiitaka Serikali kuwapa muda wa kutosha wakazi wa mikoa hiyo kujadili mustakabali wa madai yao kuhusu rasilimali hiyo.

Wanavyuo hao wa Jumuiya ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya Ruaha (RUCo) , Chuo kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (MUCE)  na Chuo Kikuu cha Tumaini (IUCo) walioazimia kufanya maandamano hayo huku wakiwahusisha wananchi wa mkoa wa Iringa wanayotokea mikoa ya Lindi na Mtwara walikwamishwa na zoezi hilo baada ya jeshi la polisi kutoruhusu maandamano na hivyo kufanya mkutano katika bustani ya manispaa ya Iringa.

Aidha wanafunzi hao waliitaka serikali isiwaone viongozi wa vyama vya siasa na dini wanaounga mkono wakazi wa mikoa hiyo kwamba ni wachochezi, bali ifahamu kuwa wanalenga kuipunguzia serikali gharama kubwa za mchakato wa ujenzi wa mabomba ya kusafirisha gesi hiyo kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam umbali wa km. 560 ambazo  zitagharimu sh. trilioni 1.9


Akisoma tamko la pamoja la wanachuo hao, Namangaya Mhaji Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya wanafunzi wanaotokea mikoa ya Lindi na Mtwara, alisema wameamua kufanya hivyo ili kuungana na wenzao wa mikoa hiyo katika kutetea kile wanachokiamini kuwa kuisafirisha rasilimali hiyo ni kuendeleza kuwakandamiza wananchi wa mikoa hiyo.

“ Tunamkumbusha Rais  Kikwete ahadi yake ya mwaka 2009-2010 aliyoitoa na kuahidi katika ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kwamba mikoa ya Kusini (Lindi na Mtwara) itakuwa na ukanda wa viwanda. Aliwahimiza wakazi wa Mtwara kujenga hoteli za kisasa na tayari zimejengwa za kutosha lakini je, ikiwa gesi asilia itasafirishwa kupelekwa Dar es Salaam ni viwanda gani tena ambavyo vitajengwa,”Alisema.

Katika madai yao,wanafunzi hao waliikumbusha pia serikali juu ya ahadi walizoahidi kuwafanyia wakazi wa Kusini ambazo hazijatekelezwa hadi sasa ikiwemo ahadi ya serikali ya kujenga tawi la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mkoani Mtwara pamoja na Hospitali ya Rufaa katika mikoa ya Lindi na Mtwara.

“Tunamuomba Rais Kikwete na wananchi wote kwa ujumla watuelewe kuwa hatuna maana kwamba gesi yote ya Lindi na Mtwara itumike kwa wananchi wa mikoa hiyo bali kiwanda au mitambo ya kufua umeme wa gesi ijengwe Mtwara na Lindi na siyo Dar es Salaam, kisheria na katika hali ya kawaida rasilimali yoyote ile inayopatikana katika eneo fulani ni lazima iwanufaishe wananchi waishio katika eneo husika, hivyo rasilimali iliyopo mikoa ya Lindi na Mtwara ni lazima wananchi wanufaike nayo,”Alisisitiza kiongozi huyo.

Juma Chilavi mwanachuo wa Tumaini alisema kuna umuhimu mkubwa kwa serikali kuwasikiliza wananchi wa Lindi na Mtwara, kwa kujenga kiwanda cha gesi katika mkoa hiyo ili kuwasaidia wananchi wake katika kukuza uchumi wao.

“Kupitia kiwanda cha gesi hii ambayo mwenyezi Mungu ameamua kututunuku ili kuboresha maisha yetu, wananchi watapata ajira na hivyo kiwango kikubwa cha watu kukimbilia jijini Dar es saalam kitapungua, na kwa kweli wananchi wa Mtwara na Lindi wana maisha magumu sana, sioni haja ya serikali kung’ang’ania kuisafirisha gesi hiyo,” Alisema Chilavi.

Naye Shabani Yusuph alisema wafanyabiashara wadogowadogo ambao wamepewa jina la “wamachinga” wanatoka katika mikoa hiyo kutokana na baadhi yao kukimbia hali duni ya maisha mikoani mwao.

Halima Chitunu mwanachuo wa Mkwawa alisema ujenzi wa kiwanda cha gesi katika mkioa hiyo ya Lindi na Mtwara wanawake wangeweza kukua kiuchumi tofauti na hali halisi ilivyo sasa, kwani uchumi wa wanawake katika mikoa hiyo ni duni tofauti na wanawake wa mikoa mingine.

“Wanawake wa Lindi na Mtwara wanamaisha magumu sana, tungeiomba serikali yetu isikilize kilio cha wananchi wake, badala ya kuwabeza na kuona kama malalamiko yao ni  upuuzi,” Alisema Halima.

Rais wa serikali ya wanafunzi wa chuo kikuu cha RUCO (Ruaha University) Willium Lufili  alisema idadi kubwa ya wananchi wataendelea kukimbilia jijin I Dar es Salaam na hivyo kulifanya jiji hilo kuwa na msongamano mkubwa, kutokana na serikali kutoona umuhimu wa kujenga viwanda na rasilimali za kiuchumi katika mikoa mingine.

“Serikali inalalama juu ya mrundikano wa wananchi jiji Dar, lakini wananchi wanafuata shughuli mbalimbali za kiuchumi ambazo zimewekwa huko, na kuisahau mikoa mingine kama haipo ndani ya nchi yetu, uchumi wa mikoa ya kusini ni duni kutokana na viwanda vingi na vitu vya msingi kupelekwa Dar es salaam au mikoa ya Kaskazini, Alisema Lufili.
MWISHO.









No comments:

Post a Comment