Maadhimisho ya miaka 60 ya siku ya uuguzi na ukunga ambayo watumishi wa idara ya afya wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa walisherekea siku hiyo katika Hospitali Teule ya Tosamaganga iliyopo katika tarafa ya Kalenga.
Watumishi wa idara ya afya Wilaya ya Iringa wakiwa katika maandamano ya miaka 60 ya siku ya uuguzi na ukunga.
Maandamano yakipita mbele ya Hospitali teule ya Tosamaganga, ambapo baada ya maandamano misa takatifu ilifanyika katika Hospitali hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Pudensiana Kisaka, akitoa misaada na zawadi kwa wagonjwa na akinamama wajawazito waliojifungua siku hiyo ya uuguzi na ukunga.
Wauguzi na wakunga wakifurahia jambo nje ya Hospitali teule ya Tosamaganga.
Mganga mkuu wa Wilaya ya Iringa (DMO) Dr. Mlowe (wa kwanza kushoto) akiwa na mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Pudensiana Kisaka katika sherehe ya mika 60 ya uuguzi na ukunga, katika ukumbi wa Hospitali Teule ya Tosamaganga-Iringa. 
Baadhi ya Wauguzi na wakunga wakiwa katika ukumbi wa sherehe.
Diwani wa viti maalumu Kata ya Kalenga Bi. Shakira Kiwanga akiwa na Padre wa kanisa la Tosamaganga katika sherehe hiyo ya uuguzi na ukunga.
Wauguzi wakisikiliza hotuba kutoka kwa mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Pudensiana Kisaka (hayupo pichani).
Bi. Isse Nzelu mtumishi wa idara ya afya wilaya ya Iringa, akisoma lisara ya wauguzi na wakunga, mbele ya mgeni rasmi mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Bi. Pudensiana Kisaka (Hayupo Pichani) siku ya maadhimisho ya miaka 60 y uuguzi na ukunga, katika ukumbi wa Hospitali teule ya Tosamaganga.
Wauguzi wakiteta jambo katika sherehe hiyo.
HALMASHAURI ya Wilaya ya Iringa, bado inaendelea kukabiliwa na changamoto ya vifo vya akinamama wajawazito na watoto wachanga, licha ya uwepo wa mikakati ya kupunguza tatizo hilo.
Akizungumzia changamoto hizo katika maadhimisho ya baraza la uuguzi na ukunga nchini, sherehe zilizofanyika katika Hospitali teule ya Tosamaganga-Iringa, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Pudensiana Kisaka alisema Halmashauri yake inakabiliwa na ongezeko kubwa la vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga wenye umri wa siku sifuri hadi siku 28.
Kisaka alisema kumekuwa na vifo vya wajawazito 303 ambao wanapoteza maisha pindi wanapojifungua kati ya akinamama laki moja ambao wanapatiwa huduma ya kujifungua.
Alisema vifo hivyo vya uzazi vimeongezeka kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na takwimu za kitaifa, ambazo ni asilimia 404 kwa vizazi hai laki moja.
“Changamoto nyingine ni vifo vya watoto wachanga kuanzia siku sifuri hadi siku 28, ambapo kumekuwa na vifo kwa asilimia 15 hadi 19.3 kati ya watoto elfu moja (1000), na changamoto nyingine ni uwepo wa ugonjwa wa Ukimwi kwa kiwango kikubwa ambapo Halmashauri yetu ina asilimia 15.7”
Alisema mabadiliko ya mifumo ya utoaji wa huduma za afya na ongezeko la huduma hizo kama huduma ya ugonjwa wa Ukimwi kunachangia kudhorota kwa utoaji wa huduma za afya kwani hata miundombinu iliyopo haikidhi mahitaji ya utoaji wa huduma.
Aidha alisema hata upungufu wa dawa unachangia huduma ya afya kutolewa chini ya kiwango sahihi kinachotakiwa na kuwa idadi ya wajawazito wanaozalishwa na wauguzi wenye ujuzi ni asilimia 66 ikilinganishwa na kiwango cha kitaifa ambacho ni asilimia 50 kwa takwimu za mwaka 2012.
Alisema katika kukakabiliana na changamoto hiyo na kutoa huduma bora, Halmashauri kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo na sekta ya afya watawapeleka masomoni wauguzi na wakunga kupata elimu ngazi ya Stashahada na Shahada, ili kuwawezesha watumishi hao kutoa huduma bora zaidi.
Naye muuguzi mfawidhi wa Hospitali teule ya Tosamanganga, sister Julieta Mzena alisema changamoto inayoikabili Hospitali hiyo, ni uhaba wa watumishi ambao unachangia msongamano mkubwa wa wagonjwa.
Sister Mzena alisema Hospitali ina manesi waliosajiliwa ni 19 huku wakiwa na wauguzi wakunga 46 na Hospitali inaupungufu wa wauguzi 65 ili kutoa huduma madhubuti.
“Vitu ambavyo vinatukwamiksha katika shughuli yetu hapa Hospitali ni wingi wa wagonjwa ambao hauwiani na idadi ya wauguzi, na hivyo kuwalazimu wahudumu kufanya kazi hadi muda wa kupitiliza,” Alisema Mzena.
Alisema kutokana na hali hiyo, wagonjwa wanaofika katika Hospitali hiyo majira ya saa mbili hadi saa tatu asubuhi, hufanikiwa kupata huduma majira ya saa saba mchana na hivyo kuwepo na msongamano mkubwa zaidi, na watumishi kulazimika kutoa huduma hadi muda wa ziada ili kuwafikia wagonjwa wote.
Hata hivyo muuguzi mkuu wa Wilaya ya Iringa Edmunda Mosha alisema tatizo linalowakabili katika sekta hiyo ya afya, ni baadhi ya wauguzi kutokuwa na maadili mema ya utumishina hivyo kushindwa kufuata kanuni za utoiaji wa huduma kwa namna inavyotakiwa na wizara husika.
"Changamoto inayochangia taaluma yetu ya uuguzi kudharauliwa katika jamii na hata wadau wetu ni pamoja na baadhi ya watumishi wa ngazi ya uuguzi kughushi vyeti vya kujiunga na vyuo vya uuguzi, hali hii inasababisha watumishi wa aina hiyo kushindwa kutoa huduma kwa kiwango kinachostahili," Alisema Mosha.
Katika maadhimisho hayo, wauguzi na wakunga wametoa misaada mbalimbali, vikiwemo vitenge, Khanga na Sabuni kwa wagonjwa wa Hospitali teule ya Tosamaganga.
MWISHO
No comments:
Post a Comment