Friday, January 3, 2014

HAPA NDIPO ATAKAPOZIKWA WAZIRI WILLIUM MGIMWA


Eneo hili la makaburi ya ukoo wa akina Mgimwa ndiko atakalozikwa Waziri wa fedha Dr. Willium Mgimwa, ambaye pia alikuwa ni mbunge wa jimbo la Kalenga, ni katika kijiji cha Magunga Wilayani Iringa.
Makaburi ya Ukoo wa akina Mgimwa, yaliyopo nje ya nyumba ya mama mzazi wa Dr. Willium Mgimwa, katika kijiji cha Magunga Wilaya ya Iringa.


 Bi Consolata Mgovano mama mzazi wa Dr. Willium Mgimwa, aliyekuwa waziri wa fedha nchini tanzania, ambaye amefariki mapema wiki hii nchini Afrika Kusini wakati akipatiwa matibabu.
 Mama mzazi wa Dr. Willium Mgimwa akiwa na mtoto wake wa pili, (Mdogo wake Dr. Mgimwa) wakiomboleza kifo cha kiongozi huyo katika kijiji cha Magunga.
 Hapa ni nyumbani kwa Dr. Willium Mgimwa- Kijijini Magunga.

 Nyumba hii ya mama mzazi wa Waziri wa fedha inaonyesha Uzalendo wa kutokuwepo kwa matumizi mabaya ya madaraka na kujimilikisha rasilimali za watanzania.

 Baadhi ya ndugu jamaa na marafiki wakisubiri siku kuwasiri kwa mwili wa aliyekuwa Waziri wa fedha nchini Tanzania, aliyefariki nchini Afrika Kusini wakati akipatiwa matibabu.
 Baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi CCM wakiwa katika msiba huo siku chache za kusubiria mazishi ya Waziri huyo wa fedha.
 Baadhi ya viongozi wa CCM wakibadilishana mawazo katika eneo la msiba kijijini Magunga.

KUFUATIA kifo cha waziri wa fedha nchini Tanzani Dr. Willium Mgimwa, aliyefariki nchini Afrika ya kusini mapema mwezi huu, mtandao huu uliamua kufunga safari hadi katika kijiji cha Magunga, ambako ndiko anataraji kuzikwa kiongozi huyo.

Kijiji cha Magunga kipo umbali wa km 78 kutoka Manispaa ya mji wa Iringa, kwa kupitia njia ya Kalenga, ambako waziri huyolicha ya wadha wake huo pia alikuwa  ni mbunge wa jimbo la Kalenga mkoani Iringa.

Bi. Consolata Mgovano ndiye mama mzazi wa Dr. Mgimwa ambaye naye ni mkazi wa kijiji hicho cha Magunga, na baada ya kufika katika kijiji hicho mtu wangu wa kwanza kuzungumza naye alikuwa ni katibu wa mbunge huyo Bw. Martin Simango, ambaye yeye alinionyesha eneo la maziko ambako atazikwa kiongozi huyo.

Bw. Simango anasema eneo lililochaguliwa kuzikwa Dr. Willium Mgimwa ni maziko ya ukoo wa akina Mgimwa ambapo pia lipo kaburi la baba mzazi wa Waziri huyo, jirani kabisa na nyumba ya mama mzazi wa waziri huyo.

Consolata Mgovano (Mama mzazi wa Dr. Mgimwa) amesema hafahamu mtoto wake ameugua nini mpaka kifo kikamkuta huko Afrika Kusini, na kuwa pengo aliloliacha mtoto wake kamwe halitazibika katika familia yake kwani alikuwa ni msaada mkubwa kwa watoto Yatima walioachwa na dada pamoja na wadogo zake.

Bi. Consolata amesema tukio la kifo cha mtoto wake bado hajaamini kama ni kweli au Laa!! Na kuwa pigo hilo nila ukoo mzima, kwani licha ya kulea familia za marehemu ndugu zake pia alikuwa anakabiliwa na mzigo wa kuwasomesha watoto wa marehemu ndugu zake, jambo ambalo linaweza kuleta utata kwa watoto wa ndugu zake ambao bado wanaendelea na masomo.

Emiflora Ngaga mpwa wa Waziri huyo (mtoto wa dada wa marehemu Dr. Mdimwa) amesema mjomba wake licha ya kuwa ni kiongozi wa ngazi ya juu kitaifa, lakini alikuwa na mahusiano ya karibu na ndugu na jamaa zake jambo ambalo baadhi ya viongozi wamekuwa wakishindwa kufanya hivyo.

“Mjomba licha ya kuwa Waziri lakini akipata nafasi naakuja kijijini kutusalimia, na akifika huku anakuwa mtu wa kawaida kama zamani, nilikuwa ninamuona ni kiongozi wa tofauti kabisa, maana baadhi ya viongozi huwa hawakumbuki kabisa kurudi makwao,” Alisema Emiflora.

Hata hivyo mazingira ya familia ya nyumbani kwa Dr. Mgimwa yameonyesha uwepo wa uadilifu mkubwa wa madaraka yake, kwa kuwa nyumba ya mama yake mzazi haina tofauti na nyingine zilizopo kijijini hapo.

Viongozi wa aina hii wasio na tabia ya kujilimbikizia mali wanaweza za kuwanufaisha wao binafsi na familia zao ni nadra sana, kwa kuwa baadhi yao wamekuwa wakikumbuka zaidi upande wao kuliko wananchi waliowachagua.

Amina Himbu – katibu W/ Iringa amesema kifo cha Dr. Mgimwa ni pengo kubwa kwa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Iringa, kutokana na mchango wake mkubwa katika chama.

Naye Silvesta Kaywanga na Telesisia Nyanza- wakazi wa kijiji cha Magunga, wamesema mbunge wao huyo amekuwa na jitihada za kutekeleza yale aliyowaahidi, na kilichobaki ilikuwa ni ukamilishaji wa miundombinu ya Barabara.
MWISHO

No comments:

Post a Comment