Sunday, January 5, 2014

MWILI WA WAZIRI MGIMWA WAPOKELEWA IRINGA KWA VILIO


 Ndege ambayo iliubeba mwili wa aliyekuwa waziri mkuu Dr. Willium Mgimwa, ikiwa katika uwanja wa Ndege wa Nduli mkoani Iringa.
 Picha inayoongoza jeneza la marehemu Mgimwa
 Mwili wa Dr. Willium Mgimwa ukiwa katika ukumbi wa "Siasa ni Kilimo" Manispaa ya Iringa, tayari wananchi kutoa heshima zao za mwisho kwa kuuaga mwili wa kiongozi huyo.

 Kada wa chama cha mapinduzi CCM akiuaga mwili wa Dr. Mgimwa kwa mara ya mwisho katika ukumbi wa Siasa ni Kilimo Manispaa ya Iringa, mara tu baada ya jeneza la mwili wa kiongozi huyo kuwasiri mkoani Iringa.
 Nako kijijini Magunga Kaburi analotaraji kuzikwa Dr. Willium Mgimwa mafundi wakiendelea kulijenga, na hapo likiwa katika hatua za mwisho.
 Fundi akiendelea na kazi ya ujenzi wa kaburi la aliyekuwa waziri wa fedha Dr. Mgimwa, katika kijiji cha Magunga.
 Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Dr. Retisia Warioba ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na usalama Wilaya akisimamia kazi ya ujenzi wa kaburi hilo kwa ukaribu zaidi, lengo likiwa ni kufanikisha shughuli hiyo kwa kiwango chenye ubora zaidi.

 Mafundi wakiendelea na kazi ya ujenzi wa kaburi la Dr. Mgimwa.
Ujenzi wa Mahema na kaburi la maziko ya Dr. Mgimwa.

HATIMAYE mwili wa aliyekuwa waziri wa fedha nchini Dr. Willium Mgimwa aliyefariki nchini Afrika kusini wakati akiendelea na matibabu umewasiri kijijini Magunga mkoani Iringa, ukitoke jijini Dar es Salaam.

Mwili wa Dr. Mgimwa umewasiri katika uwanja wa Ndege wa Nduli majira ya saa kumi na moja siku ya Jumapili jioni, huku jeneza la mwili wake likiambatana na  viongozi mbalimbali wa chama na serikali katika msafara huo.

Baada ya kutoka katika uwanja huo wa ndege wa Nduli, msafara mzima ulielekea katika “Ukumbi wa Siasa ni Kilimo” wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, ukumbi uliopo eneo la Gangilonga.

Hatua za awali baada ya kuwasili mwili huo - ulianza kuagwa na wananchi wa mkoa wa Iringa kwa  kuongozwa na Waziri mkuu Mizengo Pinda, na kufuatiwa na Spika wa Bunge la jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Anna Makinda.

Baada ya waombolezaji, wageni, ndugu, jamaa na marafiki kumaliza zoezi la kuuaga mwili huo, safari ya kuelekea katika kijiji cha Magunga atakapozikwa kiongozi huyo ilianza majira ya saa kumi na mbili na nusu jioni.

Mazishi ya kiongozi huyo wa Kitaifa yanataraji kufanyika leo majira ya saa nane mchana, huku viongozi wakuu wa serikali rais Jakaya Kikwete, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, Spika wa Bunge  Anna makinda, baadhi ya mawaziri , wabunge na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali wakitaraji kushiriki katika safari hiyo ya mwisho ya Dr. Mgimwa.

Akizungumzia hali ya maandalizi ya Kaburi analotaraji kuzikwa Waziri Mgimwa,  mwenyekiti wa kamati ya Ulinzi na usalama Wilaya ya Iringa ambaye pia ni mkuu wa Wilaya ya Iringa Dr. Retisia Warioba amesema Kaburi hilo tayari limekamilika ujenzi wake na hatua iliyobaki niyakuweka Marumaru na kuwa mazishi yatafanyika siku ya Jumatatu.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment