Wednesday, April 27, 2011

Tembo waua mtu, Lyadebwe Njombe



TEMBO WAUA MTU NJOMBE, WAHARIBU MAZAO KATIKA VIJIJI 4


MTU mmoja Vitus Mwinami mkazi wa kijiji cha Lyadebwe ameuawa na Tembo waliovamia vijiji mbalimbali vilivyopo katika Wilaya mpya ya Wanging’ombe, Njombe mkoani Iringa na kufanya uharibifu wa mazao mashambani.

Akizungumzia kifo hicho kaka wa marehemu Shukrani Mwinami alisema kaka yake Vitus Mwinami aliuawa na Tembo hao ambao walipita katika kijiji cha Lyadebwe Kata ya Kijombe wakati marehemu na wenzake walipokuwa wakitoka shambani.


Mwinami alisema marehemu Vitus alikuwa na wenzake wawili ambao baada ya kuona kundi kubwa la wanyama hao, wawili hao walifanikiwa kukimbia licha ya kuwa nao walijeruhiwa na wanyama hao.


Ofisa mtendaji wa kijiji cha Lyadebwe Alex Peramiho alisema kundi kubwa la Tembo 15 limevamia vijiji vya Lyamluki, Kangaga, Ukomola, Utiga, Ikwavila na kijiji cha Lyadebwe katika kata ya Kijombe na kufanya uharibifu.

“Alisema kuna Tembo 15 wamevamia vijiji vyetu katika kata hii ya Kijombe, hali hii ni tishio kubwa kwa wananchi hasa mauaji haya yaliyotokea hapa Lyadebwe, tunashindwa hata kufanya shughuli za maendeleo kwa kuhofia wanyama hawa,” Alisema Peramiho.


Ofisa wanyamapori wa Wilaya ya Njombe Obeid Ngailo alikiri kutokea kwa tukio hilo na kuwa idara yake inaendesha doria ili kuwarudisha wanyama hao katika njia zao ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ruaha.

Ngailo alisema maiti ya marehemu huyo waliikuta kiwa imeharibiwa vibaya ikiwa pamoja na kutolewa wake utumbo nje na wanafanya jitihada za kila hali kuhakikisha wanyama hao wanaondoka ndani ya makazi ya watu kwa kuwarudisha hifadhini.

“Tunachofanya ni kuwaondoa katika makazi ya watu na kuwarudisha katika hifadhi, lakini wakituzidi nguvu itabidi tuwaue, hawa Tembo unajua wanatoka hifadhi ya Ruaha na wanakwenda pori la akiba la Mpanga Kipengere,” Alisema Ngailo.

Aliwataka wananchi kuwa makini na wanyama hao ikiwa pamoja na kutoa taarifa mapema kwa maafisa wanyama pindi wanapopata tetesi za uwepo wao katika maeneo yao ili kupunguza uharibifu unaopelekea kupoteza maisha yao.


Aidha naibu waziri wa maji na mbunge wa jimbo la Njombe Magharibi injinia Gerson Lwenge alihudhulia msiba huo na kutoa shilingi laki moja kwa wafiwa ikiwa ni rambirambi kwa ndugu wa marehemu waliofikwa na msiba huo.

Inj. Lwenge aliwataka maafisa wanyamapori wanaweka mikakati madhubuti ya kudhibiti uharibifu unaofanywa na wanyama hao ikiwa pamoja na kuhakikisha hawaingii katika makazi ya watu kwakuwa hali hiyo ni tishio la usalama wa wananchi.


MWISHO

No comments:

Post a Comment