UGONJWA wa kuanguka uliowakumba wanafunzi wa shule ya msingi Mayota, iliyopo katika Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya umesababisha wanafunzi wote waliofanya mtihani wa darasa la saba kufeli.
Akizungumzia ugonjwa huo mratibu elimu Kata ya Lugelele Bw. Edger Kantimbo amesema tatizo hilo lilidumu kwa miezi mitatu mfululizo, ambapo wanafunzi walikuwa wakianguka na kupiga kelele na kusababisha shule hiyo kufungwa.
Amesema pia shule hiyo inakabiliwa na changamoto ya kutofikika msimu wa mvua, na pindi mvua zinaponyesha wanafunzi hushindwa kuendelea na masomo kutokana shule kuwa kisiwa, hivyo walimu kutoishi katika mazingira hayo ya shule licha ya uwepo wa nyumba tano za walimu.
Amesema walimu wote wa shule hiyo hawakai katika nyumba za shule na hivyo kuamua kuishi Lujewa na Kata ya Ubaruku hatua ambayo inachangia walimu hao kutofika kwa wakati unaotakiwa na kuchelewa kuanza vipindi.
Aidha kantimbo amesema shule hiyo iliwahi kushika nafasi ya kwanza kimkoa mwaka 1995, na kiwilaya imekuwa ikiongoza mara nyingi, na kuwa ugonjwa huo ndiyo sababu kubwa ya wanafunzi 18 hao kufeli darasa zima.
Hata hivyo mbunge wa jimbo hilo la Mbarali Bw. Dickson Kilufi amesema ni jambo lisilowezekana shule yenye nyumba za kuishi walimu zikawa hazitumiki kwa sababu tu walimu kutaka kuishi mjini.
MWISHO
No comments:
Post a Comment