Rais Jakaya kikwete akiangalia moja ya mradi wa maji, katika tarafa ya Pawaga Iringa, uliopangwa kuzinduliwa katika maadhimisho ya siku ya maji, ambayo kitaifa yamefanyika katika mkoa wa Iringa. |
RAIS Jakaya Kikwete amezindua mradi wa maji wa zaidi ya shilingi Bilioni 73 wa maboresho ya huduma ya maji mjini Iringa, wenye uwezo wa kuhudumia zaidi ya wananchi laki 2 mradi uliojengwa kwa ufadhili wa wahisani mbalimbali ikiwemo Jumuiya ya Ulaya (EU).
Akitoa taarifa ya mradi huo Mhandisi wa Mamlaka ya Maji Safi na Maji taka Manispaa ya Iringa (IRUWASA), Bw. Marco Mfugale amesema mradi huo una uwezo wa kuzalisha mita za ujazo wa maji elfu 61 kwa siku.
Akihutubia wananchi wa mkoa huu, kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji ambayo kitaifa yamefanyika katika uwanja wa Samora mkoani hapa, rais Kikwete amewataka wananchi kuacha tabia ya kuharibu miundombinu ya maji, na kuwaonya wote wanaorejesha mifugo na kuendesha shughuli za kilimo katika bonde la hifadhi ya Ihefu linalotiririsha maji yake katika Mto Ruaha Mkuu.
Aidha amesema upungufu wa mvua na maji umekuwa ukisababishwa na mabadiliko ya tabia nchi ambayo chanzo chake ni shughuli za kibinadamu, na kuwa dunia iko mbioni kukumbwa na vita kuu nyingine itokanayo na watu kupigania maji kwasababu ya uhaba wa huduma hiyo
Hata hivyo Kikwete amewaasa wabunge na madiwani kuacha kuwaunga mkono wananchi wanaochangia uharibifu wa mazingira, kwa kuogopa kutopigiwa kura wakati wa uchaguzi, kwa kuwa maji yatokayo katika Mto Ruaha Mkuu ndiyo hutumika kwa shughuli za kuzalishia umeme katika Bwawa la Mtera.
No comments:
Post a Comment