Wednesday, May 22, 2013

KIKWETE ATOA ONYO KWA WADOKOZI WA FEDHA ZA UJENZI


 Eneo la uzinduzi wa mradi huo wa barabara.
 Akiwa na viongozi mbalimbali eneo la uzinduzi wa mradi huo.
 Akisalimiana na wananchi. 

RAIS Jakaya  Kikwete  ameziagiza mamlaka zote zinazosimamia ujenzi wa barabara, kutowafumbia macho watu wachache wanaokwamisha miradi hiyo kwa tamaa zao za fedha.

Rais Kikwete  aliyasema  hayo wakati akizungumza na wananchi wa jimbo la Isimani mkoani Iringa katika uzinduzi wa mradi wa barabara eneo la Migoli - Mtera  alipofika kuweka jiwe la msingi la ujenzi  wa barabara  ya Iringa - Dodoma.

Rais Kikwete  alisema  mamlaka zinazohusika zisipodhibiti wizi huo miradi ya ujenzi ukiwamo huo wa Iringa- Dodoma unaweza kukwama kutokana na udokozi wa mafuta, vipuri na alama za barabarani, na kuwa ili  kutunza barabara  hizo ni vema  wanaohujumu miundombinu  wakafichuliwa na kuchukuliwa hatua kali.

Hata  hivyo  alisema mbali ya  serikali kuendelea  na uboreshaji  wa miundo mbinu hapa  nchini bado anawataka  watanzania  kutambua jitihada  hizo .

Alisema kuwa  sasa  watanzania  wanaweza kusafiri hadi Kenya na Uganda  kwa barabara ya lami na kuwa bado jitihada  zitaendelea daima.

 Rais   Kikwete  alisema  kuwa  mbali ya  serikali  kujipanga kwa  ujenzi  wa barabara bado lengo la  serikali ni  kuhakikisha nchi  nzima inaunganishwa kwa mtandao  wa barabara  ya lami na kuwa kazi hiyo tayari  imeanza.

Alisema  kuwa serikali  yake  toka  imeingia madarakani  imeendelea  kuongeza  fedha  katika mfuko  wa barabara  na kuwa lengo ni kuendelea  kuongeza  zaidi fedha katika mfuko  huo ili  kuwezesha  ujenzi  wa barabara nchini kuweza  kukamilika 

 Aliwapongeza  viongozi wa TANROADS kwa kazi nzuri  wanayoendelea  kuifanya na kwa  mbali ya kupongezwa bado hawapaswi kulewa  sifa na badala  yake  kuendeleza  jitihada za  kusimamia  kazi  hiyo kwani upo usemi unao sema kuwa mgema akisifiwa pombe huweka maji .

Pia  Rais Kikwete alimpompongeza  waziri wa fedha Dkt Wiliam Mgimwa kwa kuendelea  kuidhinisha  fedha kwa ajili ya miradi ya barabara hapa nchini na kuwa  bila  wizara  hiyo  kutenga bajeti  kazi hiyo ingeendelea  kuwa ngumu.

Akizungumzia kuhusu amani na utulivu nchini Rais Kikwete  alisema  wapo  baadhi ya  watu usiku na mchana  wamekuwa  wakipanga mipango mibaya ya  kuvuruga amani ya nchi  hii na hivyo noi vema  watanzania kuwaepuka  watu wenye nia ya kuchafua nchi hii kwa kuchochea  vurugu.

Alisema  iwapo  watanzania  watakataa kuwasikiliza watu hao wala kushirikiana nao  kamwe Tanzania haitaingia katika machafuko yanayopangwa na watu hao  wasio penda mema.


Akitoa  taarifa  ya ujenzi  wa barabara  hiyo waziri wa ujenzi Dk.  John Magufuli alisema  kuwa  wizara yake haitasita kuwachukulia hatua  makandarasi ambao  watashindwa kutekeleza mikataba yao kama ilivyo elekezwa.

Waziri Magufuli alisema  kuwa  wizara  yake chini ya Rais Kikwete  itaendelea  kusimamia  ujenzi  wa barabara na kujenga kwa kiwango cha lami na  kuwa  wale  wanaopinga  jitihada hizo  waendelee kusubiri kuandamana katika barabara  zilizojengwa na serikali ya CCM.


Waziri Magufuli alisema kuwa ujenzi wa barabara  hiyo ya Iringa -Dodoma yenye urefu wa Km 260  itajengwa kwa zaidi ya bilioni 232 fedha kutoka benki ya maendeleo Afrika (ADB) na serikali ya Japani pamoja na serikali ya Tanzania.

Wakati  huo  huo  wafanyakazi  na vibarua  wanaofanya kazi katika kampuni  hiyo ya kichina  inayotengeneza  barabara  ya eneo la Migoli katika barabara hiyo ya Iringa - Dodoma nusuru  wavurugu siku baada ya kupaza  sauti mbele ya  Rais wakilalamikia   fedha kiduchu  wanazo  pata kwa siku kwa kufanya kazi katika kampuni hiyo.

Vibarua  hao  na  wafanyakazi  walisikika  wakipaza sauti  wakati Rais Kikwete akiaga kwa ajili ya kuelekea katika chakula  cha mchana kuwa wanapunjwa  sana mishahara na kuomba kusaidia kupiganiwa  ili kulipwa kima cha chini cha mishahara ya  serikali.

"Mheshimiwa  Rais una ondoka  ila sisi  wafanyakazi tunaomba kusikilizwa kilio chetu ....hawa  wachina  wanatufanyisha kazi kwa ujira mdogo sana mheshimiwa tunaomba kusaidiwa ....walipaza  sauti wafanyakazi na vibarua hao ambao  walikuwa wamesimama  juu ya mashine  zao za kazi"

Hata  hivyo Rais Kikwete hakuweza  kujibu  chochote  juu ya madai hayo kutokana na eneo  hilo kutawaliwa na kelele nyingi za burudani.

MWISHO

No comments:

Post a Comment