Saturday, May 18, 2013

WAKULIMA WAANDAMANA KUPINGA ONGEZEKO LA USHURU


Moja ya stakabadhi ya ushuru wa zao la Mpunga, ambapo gunia 80 zilitozwa shilingilaki moja na elfu 60.
Wakielekea ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, kuonana na Mkurugenzi. 


 Wamefika nje ya geti la ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Iringa (Siasa ni Kilimo).

 Ofisa habari wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa- Evaristo Myovela (Albino) kifanya mazungumzo na wakulima hao.
 Baadhi ya wakulima wakiwa nje ya ofisi za wakala wa Vipimo mko wa Iringa, ndani ya uwanja wa Saba saba Manispaa ya Iringa.


HATIMAYE wakulima wa zao la Mpunga mkoani Iringa wameandamana hadi katika ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, wakilalamikia kupanda kwa gharama za ushuru wa zao hilo, kutoka shilingi elfu moja hadi  shilingi  2000.

Wakizungumzia hatua ya uamuzi huo wakulima hao wamesema, wamechoshwa na kiwango kikubwa cha ushuru ambacho kinadumaza hali ya uchumi wao, na kushindwa kujikwamua kiuchumi na hata kuhofia kuingia katika shughuli ya kilimo hicho mwaka huu.

Deo Mbongo amesema na Anjerous Lijuja wamesema wanaogopa hata kuvuna Mpunga msimu huo, kwani bei za kuuza sokoni zimeshuka, huku gharama ya ushuru ikiongezeka kwa asilimia 100 na hivyo wao kama wakulima kupata hasara.

“Kingine tunacholalamikia hii serikali yetu ni juu ya kutaka tupunguze ujazo wa gunia, yaani mpunga uwe na kilo 75 badala ya 100, wakati hapo tena ushuru wamepandisha kwa asilimia 100, sasa hii inatuumiza sana,” Alisema Lijuja.

Agnes Kutika amesema awali walikuwa wakilipa ushuru wa gunia moja kwa shilingi moja (1000/=) na mwaka jana mwishoni ushuru huo umeongezwa hadi kufukia kiasi cha shilingi elfu mbili (2000/=) huku Manispaa nao wakitaka shilingi mia tano kila gunia moja baada ya kufika nao katika mashine.

“Hali hii ni kutuumiza sisi wakulima, hakuna tunachokipata, unalima kwa gharama kubwa, mbolea na pembejeo zote ni bei juu, lakini wakati wa mavuno tena serikali inatukamua kisai cha kupoteza mitaji yote, sioni hata sababu ya kutangaza eti “Kilimo Kwanza”, mimi hapa nilipo nina watoto wanaonitegemea pamoja na watoto yatima ninaowalea, sasa kwa mfumo huu naona kabisa ninakwama, kwani hata hela ya mkopo niliochukua kwa ajili ya kuendeshea kilimo cha Mpunga imekatika zaidi ya shilingi laki tano,” Alisema Agnes.

Abdala Luvanda fedha walizoendeshea shughuli za kilimo ni mikopo kutoka katika taasisi za kifedha, na kuwa wao wakulima wapo hatarini kuingia katika madeni na benki hizo kutokana na serikali kuruhusu kuingia kwa Mchele kutoka nje ya nchi, jambo lililoporomosha bei za zaoa hilo sokoni.

Yohana Fungo amesema kuna haja serikali ikakaa nao katika meza ya pamoja ili kuona hasara wanazopata kwa kutozwa ushuru mkubwa  usiozingatia jasho la mkulima, kwani pasipo kufanya hivyo kilimo ambacho ndiyo tegemeo kuu la wananchi walio wengi kitakwama.

Ofisi ya mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa kupitia ofisa habari wake Evaristo Myovela  amesema watazungumza na wakulima hao, ili kuona kama kuna sababu za kupunguza ushuru huo.

“Sisi kama serikali wananchi ndiyo tegemeo letu, tutakaa nao hawa wakulima ili kusikiliza malalamiko yao, na kama kuna haja ya kutekeleza ombi hili la kupunguza ushuru tutafanya hivyo,” Alisema Myovela.

Hata hivyo wakulima hao walifunga safari hadi katika ofisi ya wakala wa Vipimo mkoa wa Iringa, kujua sababu za kutaka gunia la Mpunga kuwa na ujazo wa kilo 75 pekee badala ya kilo 100 za awali.

Akitoa ufafanuzi juu ya kupungua kwa ujazo huo, meneja wa wakala wa vipimo  mkoa wa Iringa Samwel Kilyunguzi amesema hatua hiyo ni katika kupiga vita Lumbesa, kwani ujazo mkubwa ni hasara kwa mkulima, mfanyabiashara, serikali pamoja na wamiliki wa magari.

“Serikali inaingia hasara kutengeneza barabara zinazoharibiwa na ujazo mkubwa wa mizigo katika magari, lakini pia hata wamiliki wa magari nao wanapata hasara ya kuharika mapema magari kwa kubebeshwa mizigo mikubwa kupita tani zinazotakiwa, wale Makuli wanaoshusha na kupakia mizigo hiyo pia wanapoteza maisha kwa kujitwika mizigo mikubwa kushinda uzito wao, na pia mkulima naye anapata hasara kwa kuuza ujazo mkubwa, kwa hiyo tunapiga vita Lumbesa kwa lengo la kuepusha hasara kwa makundi hayo yote,” Alisema Kilyunguzi.

Wakulima hao waliitaka Halmashauri hiyo kupunguza gharama za ushuru huo, kutoka shilingi elfu mbili hadi kufikia shilingi elfu moja, ili kuweza kumudu gharama nyingine na kuweza kujikwamua kiuchumi.



No comments:

Post a Comment