Sunday, June 9, 2013

SIMBA AWAONYA WANAWAKE

 WAZIRI wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto Mh.Sophia Simba akiwahutubia wananchi wa Manispaa ya Iringa katika Kata ya Kihesa wakati wa uzinduzi wa mradi wa kuwaongezea uelewa wanawake wa Tanzania kuhusu utawala bora, chini ya ufadhiri wa Shirika la Children Care Development Organization (CCDO)
 Viongozi wa Manispaa ya Iringa wakisikiliza hotuba ya Waziri Sophia Simba.

 Waziri Simba akikabidhi zawadi ya Kompyuta kwa mshindi wa Insha kwa mwanafunzi Shindo Sungura mwanafunzi wa Iringa Girls, aliyeibuka mshindi wa kwanza.
 Waziri Simba akikabidhi Kopyuta kwa mwanafunzi Jusper Kasera mwanafunzi wa shule ya sekondari Mwembetogwa akiwa ni mshindi wa pili.
 Mh.Ritha Kabati mbungw wa viti maalumu CCM Mkoa wa Iringa  akizungumza na wananchi katika hafla hiyo ya uzinduzi wa mradi huo wa kuwaongezea uwezo wanawake katika masuala ya utawala bora.

 Waziri Simba akiwa katika picha ya pamoja na viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Iringa, waliokaa kulia ni Meya wa mji wa Iringa Amani Mwamwindi, wa pili kulia ni mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu- wa kwanza kushoto ni Mh. Ritha Kabati mbunge Viti maalumu Iringa na mwenye suti ya kijani ni Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Iringa Zainabu Mwamwindi.
 Waziri Simba (katikati) akiwa na jopo la uongozi wa CCDO.

Waziri Simba akiwa na madiwani wa manispaa ya Iringa, (wa kwanza kushoto) ni Naibu Meya wa manispa ya Iringa Mh. Gervas Ndaki.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania mkoa wa Iringa (UWT) Mh. Zainabu Mwamwindi akipiga makofi wakati wa ngoma ya asili ya Wahehe( Kiduo) katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo.

WAZIRI wa maendeleo ya jamii, jinsia na watoto Mh.Sophia Simba amewataka wanawake kujituma katika kazi  pamoja na kujiendeleza katika masuala ya elimu ili kuepukana na tatizo la unyanyasaji wanaopatiwa kutoka kwa baadhi ya wanaume wanaoendeleza tabia ya mfumo dume.

Waziri Simba ameyasema hayo katika uzinduzi wa mradi wa kuwajengea uelewa wanawake wa Tanzania, kuhusiana na masuala ya Utawala bora, mradi unaofadhiliwa na  shirika la Children Care Development Organization (CCDO) uliofanyika Kihesa katika Manispaa ya Iringa.

Simba amesema wanawake wakijiunga katika vikundi mbalimbali vya kiuchumi ikiwa pamoja na kujiendeleza kielimu wataepukana na kufanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji kutoka kwa wanaume, huku akiwaasa nao wanawake kuacha tabia ya kuwafanyia ukatili watoto kwa kuwapiga mara kwa mara.

Amesema kipigo siyo njia ya kumuonya mtoto bali akinamama wanatakiwa kutumia lugha za sauti katika kuwaonya watoto ambao ni tegemeo la Taifa la kesho, ili wawe na mwenendo ulio bora katika jamii.

Amesema kuna haja kwa wanawake wakatumia fulsa zilizopo kuingia katika ngazi mbalimbali za uongozi ili kuongeza wigo na kuondokana na umasikini wa kipato ili waweze kuzihudumia familia zao.

Serikali ya Tanzania inatambua kwamba mhimili wa jamii yetu ni mwanamke, kwani ndiye mama, mlezi katika mazingira yote, wanawake ni maskini zaidi …licha ya kufanya kazi  kubwa na ngumu katika ustawi wa kaya na familia, niseme tu kuwa ninayo furaha kubwa kuungana nanyi  wananchi wa Mkoa wa Iringa na Watanzania katika uzinduzi wa mradi huu wa kuwaongezea uelewa wanawake wa Tanzania kuhusu utawala bora, nawashukuruni sana viongozi wa Shrika la Children Care Development Organization (CCDO)  kwa kunialika kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa mradi huu unaofadhiriwa na Shirika la Mfuko wa Maendeleo kwa Wanawake Afrika (African Women’s Development Fund) kupitia kauli mbiu MWANAMKE ANAWEZA BILA KUWEZESHWA,”.  

Aidha Simba amesema hata hivyo kwa sasa hali ni bora kwa upande huo wa kundi la wanawake, tofauti na siku za nyuma, kwani wanawake wamepiga hatua kubwa ya maendeleo licha ya kuwepo kwa changamoto mbalimbali zinawakabiri.

Amesema changamoto nyingi na kubwa ni zile zinazohusiana na baadhi ya utamaduni, mila na desturi zetu zinazozaa mifumo ya kijamii unaokinzana na haki, uhuru na maendeleo ya mwanamke, na kuwa mapambano dhidi ya mila na desturi.

“Tatizo hili ni mapambano yetu sote,  na ninarudia kuwahakikishia kuwa mimi ni mpiganaji mwenzenu kupitia Wizara ninayoiongoza ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto,  nitahakikisha changamoto hizi zinapungua kama siyo kuisha kabisa, kwani tuna uhakika sasa hata bila ya kuwezeshwa wanawake tunaweza na kila kilio kina mwenyewe, kwenye kilio hiki  wenyewe hasa ni sisi wanawake ni lazima tupige kelele kwa sababu hiyo  ni muhimu CCDO ikaonekana iko mstari wa mbele katika mapambano haya kwa ujasiri mkubwa zaidi, Sisi katika Serikali tunazitambua changamoto zinazotokana na mila na desturi hizi na tunazifanyia kazi kwa nia ya kuzibadili kwa maslahi ya wanawake na jamii nzima.

Amesema katika kukabiliana na changamoto hizo, hakuna njia ya mkato zaidi ya wanawake wenyewe kujihusisha katika maamuzi ya kisiasa na kisera na katika utekelezaji wake, kupitia Wizara anayoiongoza na ubia na Wizara nyingine  atakuwa mstari wa mbele kupigania haki za mwanamke na kutumia fursa zilizopo kupigania  ongezeko la ushiriki wa wanawake katika nafasi za wanawake katika uongozi na haki za watoto ambalo ni suala lenye umuhimu wa kipekee.

 “Pamoja na mafanikio hayo ya wazi, bado tunayo kazi kubwa ya kuhamasishana sisi wanawake na jamii kwa ujumla ili ione umhimu wa wanawake kushiriki kikamilifu katika kujisomea, kupeleka mabinti shule, elimu na shughuli za uongozi na uendeshaji katika jamii zetu kwa ujumla, kwani ushiriki wao katika elimu siyo wa kutosha wala kuridhisha, kwani        ieleweke kwamba pamoja na kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi, yapo mambo ambayo yanahusu maendeleo ya wanawake ambayo inabidi yaendelee kufanywa sasa, Kwani katika Serikali tumeweka vipaumbele katika mambo matano yahusuyo maendeleo ya mwanamke nchini,".

Amesema suala la kwanza katika kuongeza ushiriki wa wanawake katika ngazi ya uongozi  ni  kuongeza uwakilishi wa wanawake kwenye vyombo vya maamuzi ili kumuongezea nguvu mwanamke zaidi kutoka hatua iliyofikiwa sasa Katika kufanikisha jambo hilo muhimu, na pia kuna masuala yanayohitaji mabadiliko ya sheria na Sera dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia kwa mwanamke na mtoto kwani sauti moja haitoshi pasipo kuungana  na kuleta nguvu ya pamoja ambayo ni matumaini na ushirikiano.

“Kwa upande wa nafasi za kuchaguliwa, ni muhimu kwetu sisi wanawake kujitokeza kwa wingi kuhamasishana kuwania nafasi za uongozi pindi fursa zinapopatikana kuanzia ngazi za Vitongoji, Kata, Wilaya, Mkoa hadi Taifa bila kutanguliza woga  wa ushindani kutoka kwa wanaume kwani wanaumme wanapaswa kutambua kuwa mwanamke anazohaki sawa kama mwanaume mbele ya sheria,”.

Na kuwa juhudi nyingine zilizofanyika katika kutokomeza ukatili wa kijinsia nchini ni uzinduzi wa Kamati ya Kitaifa ya Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake, Watoto na Albino tarehe 19 Desemba, 2011na madhumuni ya kampeni hiyo ilikuwa ni kuongeza uelewa wa jamii kuhusu madhara ya ukatili dhidi ya wanawake na wasichana katika Afrika na kuziomba Serikali husika ziwajibike katika kupiga vita ukatili kwa wanawake na wasichana.

Hata hivyo Simba amesema tatizo linaloisumbua wizara yake ni watoto wa kike kutokumaliza shule kwa kupata mimba jambalo ambalo amesema linachangia kwa kiwango kikubwa kurudisha nyuma maendeleo ya mtoto wa kike wa Kitanzania, na kuwa wizara inaendelea kukabiliana nalo, ikiwa ni pamoja na kuchukua hatua madhubuti za kupunguza tatizo la mimba za wanafunzi, huku akiitaka CCDO  kuwa mstari mbele katika harakati za kukabiliana na tatizo la watoto wa kike kutokumaliza masomo kwa sababu za kuolewa au kupata mimba na mambo mengine yanayofanya watoto wa kike wasimalize masomo kupitia mijadala mbalimbali.

MWISHO
        


No comments:

Post a Comment