Monday, July 22, 2013

HALMASHAURI YA IRINGA YAPATIWA TREKTA KUBORESHA BARABARA


Trekta ambalo limetolewa na ufadhili wa shirika la Kimataifa la Japani ili kusaidia miundombinu ya barabara ya Halmashauri ya Wilaya ya Iringa.
Makamu mwenyekiti mpya wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Costantino Kihwele, ambaye amechukua nafasi ya Ritha Mlagala aliyekuwa akitumikia nafasi hiyo na hivyo muda wake kuisha, akiwa amekalia kiti hicho kwa awamu ya kwanza katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya hiyo ya Iringa.
Maofisa tarafa "VIJANA" wa kwanza kulia ni Adestino Mwilinge wa tarafa ya Kalenga akiwa na Nasson Mwaulesi afisa tarafa wa Pawaga, wakibadilishana mawazo baada ya kutoka katika kikao cha baraza la madiwani.


Halmashauri ya Wilaya ya Iringa imepatiwa msaada wa Trekta na vifaa vya kutengeneza barabara ili kukabiliana na tatizo la miundombinu mibovu, hususani ya maeneo ya vijijini, ambayo imekuwa ni kikwazo kikubwa katika kukuza hali ya uchumi.


Trekta hilo aina ya Holland lenye baadhi ya vifaa vya ujenzi wa barabara lina thamani ya shilingi Milioni 40, na limetolewa kwa ufadhili wa shirika la Kimataifa la Japani kwa lengo la kuongeza nguvu za Halmashauri na wananchi katika kuboresha mtandao wa barabara zenye urefu zaidi ya km 1229.


Akitoa ufafanuzi wa changamoto barabara katika kikao cha baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, mhandisi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Leopord Runji, amesema msaada huo wa Trekta utaongeza nguvu katika kukarabati barabara kutoka urefu wa km 400 pekee kwa kila mwaka hadi kufikia urefu wa km 800.

Injinia Runji amesema kuongezeka kwa urefu huo wa matengenezo ya barabara, kutaleta nafuu kwa wananchi katika kusafiri na kusafirisha mazao yao na hivyo kuzifanya shughuli za kilimo kuwa zenye tija.


Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa Pudensiana Kisaka amesema msaada huo utapunguza kero ambazo zinatokana na miundombinu duni ya barabara, na kuwa wananchi wengi hususani waishio vijijini wanakabiliwa na changamoto ya miundombinu ya barabara hali inayodumaza uchumi kwa kushindwa kufikisha mazao yao katika masoko.


Hata hivyo diwani wa kata ya Lyamgungwe Alex Malangalila amesema katika kata yake kuna changamoto kubwa ya miundombinu hiyo ya barabara, huku baadhi ya wagonjwa wakipoteza maisha kwa kushindwa kuwahi kupata matibabu na wajawazito wakijifungulia njiani, na kuwa msaada huo ni nuru kwa wananchi wake.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment