Sunday, July 21, 2013

WAVUNJA NYUMBA YA MSHTAKIWA WA MATUKIO YA UBAKAJI BAADA YA KUACHIWA HURU


Wananchi na askari wakitazama Mabaki ya nyumba ya mshtakiwa wa tukio la Ubakaji wa mtoto wa miaka mitatu, nyumba ambayo imevunjwa na wananchi, kwa madai ya hasira za wananchi baada ya mahakama kumuachia kwa dhamana mshtakiwa Chesco Mbwilo.
Inspector Michael Sabai, akitoa ufafanuzi wa dhamana katika      mkutano wa dhalula, wa wananchi wa kijiji cha Kiwere.

Bi. Jestina Mgimba-mke mkubwa wa mshtakiwa Chesco Mbwilo, kiwa na familia yake ya watoto wanne.
Mwananchi Dolnd Sanga akichangia mawazo yake.
Mwananchi akichangia mawazo juu ya madhara ya sheria za kuwaachia watuhumiwa wa matukio ya Ubakaji wa watoto.
Wananchi wakiwa katika mkutano wa dharula kujadili suala la kuachiliwa mshtakiwa wa tukio la Ubakaji.

WANANCHI wa kijiji cha Kiwere kilichopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, wameandamana na kuvunja nyumba ya Chesco Mbwilo mstakiwa wa kesi ya Ubakaji, kupinga hatua ya Mahakama kumuachia huru mshtakiwa huyo jambo ambalo wamesema limevunja mahusiano ya polisi jamii na ulinzi shirikishi.


Akizungumzia mkasa huo wa kuvunjiwa nyumba na kuiacha familia ya mtuhumiwa yenye watu zaidi ya watano ikiwa haina makazi, mke wa mshtakiwa huyo amesema wananchi walipofika katika nyumba yake walimtaka awaonyeshe mumewe na baada ya kumkosa ndipo wakachukua uamuzi wa kuvunja nyumba.

Wananchi hao walivunja nyumba kubwa ya Bati na kusababisha  mali zote za ndani kufukiwa na Tofali, huku wakichoma kwa moto Mkokoteni wa kukokotwa kwa wanyama, pamoja na badhi ya mali na hivyo kuiacha familia hiyo ikiwa haina makazi.



Wakizungumzia sababu za kuchukua uamuzi huo, wananchi hao wamesema hatua hiyo imetokana na watoto wengine watano kumlalamikia mshtakiwa huyo kuwa amekuwa akiwafanyia ukatili huo wa ubakaji kwa kuwarubuni kwa Maandazi na Kamera, huku wakielekeza lawama zao kwa Mahakama, ambayo imetoa dhamana.


"Serikali inatuhimiza sisi wananchi tushirikiane kuwafichua waharifu, sisi tuliifanya kazi yetu vizuri, ili kudumisha dhana yao ya Polisi jamii na ulinzi shirikishi, sasa mtuhumiwa aliyebaka tukawapelekea, tumeshangaa tunamuona mitaani, kama siyo dharau ni nini ?? Na sisi tungemkamata tungemalizana wenyewe maana tumechoka na tabia za bwana huyo, hata huko alikotoka alifukuzwa kwa ajili ya tabia hii hii!! Hatuwezi kuyafumbia macho mambo kama haya, la sivyo watoto wetu wote wataangamia, na kutakuwa hakuna hata haja ya kujenga shule kama watoto wanawaua kwa namna hii, ubakaji hauna tofauti na uuaji, huwezi kujua mtoto kama ni mzima maana siku hizi kuna ugonjwa wa Ukimwi," Alisema mmoja wa wananchi hao.



Jeshi la polisi limefika katika kijiji hicho, na kuuazimu uongozi wa serikali ya kijiji cha Kiwere kuitisha mkutano wa dharula, huku wananchi wakisema wamechukua uamuzi wa kuvunja nyumba ya mshtakiwa baada ya kumuona mitaani huku mtoto aliyefanyiwa ukatili huo akiwa bado hajapona.



Aidha wananchi wameitaka serikari  kuiondoa familia ya mshtakiwa huyo, ili kudumisha amani baina yao na wazazi wa watotoi waliofanyiwa ukatili, huku wakilalamikia barua iliyomdhamini mshtakiwa kutolewa na kijiji cha Magubike wakati mtuhumiwa ni mkazi wa kijiji cha Kiwere.


Baba mzazi wa mtoto aliyebakwa amesema baada ya kumfikisha kituo cha Polisi mtuhumiwa, aliambiwa asifuatilie kesi hiyo kwa kuwa inaendeshwa na Jamuhuri, na kuwa mpaka sasa hajafahamu hata tarehe ya kesi ya mtoto wake, na kitendo cha kuachiwa mtuhumiwa huyo ni kuwapa mwanya wananchi wengine wenye tabia za ubakaji kuendeleza matukio hayo kwa watoto.



Diwani wa Kata hiyo ya Kiwere Pascal Mwamwano pamoja na jeshi la polisi kupitia askari wake..Inspekta Michael Sabai wamewasihi wananchi hao wapunguze hasira kwa kutoidhuru familia ya mtuhumiwa, kwa madai kuwa haihusiki na vitendo hivyo vya ubakaji na kuwa dhamana ni haki ya mtuhumiwa endapo hakabiliwi na kesi ya mauaji.

Wananchi hao ambao hawakuwa hata na chembe ya UOGA mbele ya jeshi la polisi, waliwaeleza polisi kuwa wao ndiyo chanzo cha uvunjifu huo wa amani, huku malumbano yenye kelele yakichukua nafasi yake pasipo chombo hicho cha dola kuchukua hatua zake zilizozoeleka kwa hofu ya kuibua tatizo kubwa zaidi.

Hali hiyo iliingiliwa na mwenyekiti na diwani wa Kata hiyo ya Kiwere akiwaomba wawe wasikivu katika kupata muafaka wa tatizo hilo.

Kwa mujibu wa ushauri wa insp. Sabai amewataka wananchi hao kuandika barua itakayopelekwa katika Mahakama, wakiomba familia ya mshtakiwa huyo kuhama katika kijiji hicho, huku akiwasihi waache kuchukua sheria mikononi, kwa kuwa huo ni ukiukaji wa sheria.

Kwa mujibu wa viambatanisho vya tukio la ubakaji, mstakiwa alifunguliwa jarada la kesi katika kituo cha Polisi mjini Iringa kwa kumbukumbu namba "IR/RB/3879/2013, CRO Incharge Polisi kituo cha Iringa" huku uthibitisho wa daktari ukionyesha mtoto huyo alijeruhiwa vibaya katika sehemu zake za siri.


Hata hivyo mshtakiwa huyo ana wake wawili na watoto zaidi ya 5, na nyumba iliyovunjwa ya mke mkubwa imeachwa bila makazi ikiwa na watoto wanne, watatu wakubwa na mmoja ni kichanga wa zaidi ya mwezi mmoja, na kesi ya mshtakiwa huyo ilipelekwa katika Mahakama ya Wilaya ya Iringa.



MWISHO

No comments:

Post a Comment