Monday, August 12, 2013

ALBINO NA HATARI YA MAFUTA YA MIONZI YA JUA


Watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) wakiwa katika mafunzo ya ujasiriamali na semina ya utunzaji wa ngozi zao, katika chuo cha maendeleo ya jamii Ilula katika wilaya ya Kilolo mkoani Iringa.



IMESEMEKANA kuwa watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) wapo katika hatari ya kupotea kwa kufariki kwa ugonjwa wa saratani ya ngozi (Kansa) baada ya kukosa huduma ya mafuta ya kuzuia mionzi ya jua.

Hayo yalizungumzwa na mtaalamu wa magonjwa ya ngozi  na ngono dk. Paul Luvanda katika mafunzo ya ujasiriamali na namna ya kutunza  ngozi kwa Maalbino katika Wilaya ya Kilolo mkoani Iringa, mafunzo yaliyoandaliwa na asas ya kiraia ya Kilolo Empowernment for Persons With Disability (KEPD) kwa kushirikiana na shirika la Tulime.
Dk. Luvanda alisema Albino wanatakiwa kujikinga na vifaa maalumu vya kuzuia mionzi ya jua ili kuepukana na madhara yatokanayo na mionzi ya jua  ambayo hupelekea kupata ugonjwa wa Kansa  ya ngozi na hatimaye kupoteza maisha

“Mnatakiwa kuwa makini sana kwa kuliepuka jua kwa namna yoyote ile, mjinginge kwa kuvaa kofia zenye upindo mpana ili kuzuia jua, lakini mnapaswa kutumia mafuta maalumu ya kuzuia mionzi, jua ni hatari sana kwenu kwani baada ya kuchoma ngozi na kupata vidonda unapata kansa,” Alisema Dk. Luvanda.

Luvanda alisema tatizo la Albino walio wengi ni kutojijali kwa kufanya kazi katika mazingira hatarishi yenye jua kali na kuwa hiyo ndiyo sababu ya Albino hao ngozi zao kuharibika kwa kupata vidonda ambavyo baadaye husababisha Kansa ya ngozi  na hivyo kuywa vigumu katika kupata matibabu na kusababisha vifo.

“Nimekuwa nikiwaeleza sana juu ya madhara ya jua, kwa mfano pale Stendi ya Iringa kuna kijana anapiga debe lakini muda wote anashinda juani, kila ninapomueleza juu ya hatari ya hali ya ngozi yake anakuwa mgumu kunielewa, jamani  kila mmoja anatakiwa kujijali kwanza yeye mwenyewe,” Alisema.

Anna Masasi Albino mshiriki wa mafunzo hayo alisema matatizo ya kuharibika kwa ngozi zao kunatokana na kutopatikana kiurahisi kwa  mafuta maalumu ya kupaka na hivyo kuitaka serikali kuwapa kipaumbele watu wenye ulemavu wa ngozi kama ilivyo kwa wagonjwa wa kifua kikuu na waathirika wa ugonjwa wa ukimwi.

“Tatizo kubwa ni haya mafuta madukani hayapatikani, tunaiomba serikali itupe kipaumbele kama inavyofanya kwa wagonjwa wa Ukimwi na Tb, na sisi tupatiwe kadi maalumu ya kupata matibabu yakiwemo hayo mafuta, kinachotufanya tusijali ngozi ni hali duni ya maisha yetu, haiwezekani ukajifungia ndani tu kwa kuzuia ngozi wakati huna kitu mfukoni na unafamilia inayokutegemea,” Alisema Anna.

Anjela Kigula mshiriki wa mafunzo hayo  alisema licha ya kuvaa kofia na nguo zenye kuzuia mionzi ya jua bado ngozi yake imekuwa ikiharibika kwa kupasuka hasa mdomo na hivyo kuiomba serikali kuwasaidia mafuta hayo yapatikane kwa urahisi.

Naye Kanuti Nyamike aliitaka wizara ya elimu kupitia baraza la mitihani kuacha kutoa muda sawa wa kufanya mitihani kwa watu wenye ulemavu wa ngozi na walio wazima kwani wenye ulemavu wa ngozi uoni wao ni hafifu na hivyo huwawia vigumu kufanya vizuri mitihani katika muda uliopangwa.

“Mimi lalamiko langu ni juu ya baraza la mitihani kutoa muda sawa kwa sisi wenye ulemavu wa ngozi ambao hata macho yetu tunaona kwa shida sana, sasa wanapotoa muda sawa na wasio walemavu kwetu inakuwa ni shida sana kufanya mtihani vizuri  kwani tunaona kwa taabu sana, muda unapokuwa umekwisha wa kufanya mtihani, unakuta bado hujamaliza maswali ya mtihani, ningeomba tupatiwe muda tofauti na wasio walemavu,” Alisema Kanuti.

Aidha Erick Mgovamwende alisema kuna kila haja ya Maalbino kutambua udhaifu walionao kwa kukwepa kufanya kazi hatarishi ambazo zitapelekea kupoteza maisha kwa ugonjwa wa kansa.

Akizungumzia lengo la mafunzo hayo katibu wa asas ya kiraia ya Kilolo Empowernment for Persons With Disability (KEPD) kwa kushirikiana na shirika la Tulime Tumaini Ngajilo alisema semina hiyo ya ujasiriamali imelenga kuwaongezea uwezo walemavu wa ngozi ili kuwafanya waweze kufanya shughuli za kiuchumi.

Huku mwenyekiti wa asas hiyo ya KEPD Biliel Maketa akisema kuwa elimu ya namna ya kutunza ngozi  itawasaidia kujikinga na hatari mbalimbali zinazosababisha wao kuharibika kwa ngozi zapo huku wengi wao wakipatwa na ugonjwa wa Saratani ya ngozi baada ya kupigwa na jua.

“Tayari tumefanikiwa kuwapata Albino zaidi ya 40 katika Wilayah ii ya Kilolo na tumewapatia misaada mbalimbali kama Mafuta ya ngozi, yanayozuia mionzi ya jua, Kofia za kujikinga na jua pamoja na miwani, lengo ni kuwaondoa katika hatari hiyo ya ugonjwa wa Kansa lakini pia kuwafanya waweze kufanya kazi za kuwaongezea kipato na hivyo kutunza familai zao,” Alisema Maketa.


No comments:

Post a Comment