WAVUNAJI, wasafirishaji na wauzaji wa zao la Mbao katika Msitu wa taifa Saohill uliopo katika Wilaya ya Mufindi wameifungulia kesi Halmashauri ya Wilaya hiyo kwa madai ya kupandisha ushuru wa kulipia mbao kutoka shilingi lakimoja kwa kila gari hadi kufikia shilingi Milioni moja.
Hatua hiyo ilikuja baada ya Halmashauri hiyo ya Mufindi kuanza kutoza ushuru wa ongezeko jipya pasipo kuwasiliana na wadau hao, jambo lililosababisha wavunaji, wanunuzi na wasafirishaji wa bidhaa hiyo itikanayo na misitu kugoma kutoa ushuru huo mpya wa shilingi Milioni moja kwa kila gari.Mgomo huo uliofuatiwa na mkutano mkubwa wa dharura wa wadau wa zao hilo la misitu, uliofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi baada ya wavunaji, wanunuzi na wasafirishaji zaidi ya 200 kumtaka mwanasheria wa Halmashauri hiyo kutoa ufafanuzi wa tangazo la ongezeko la kodi hiyo ya ghafla.
Akizungumzia hatua hiyo msemaji wa wadau hao Dickson Lutevele alisema uongozi wa halmashauri hiyo umekurupuka kupandisha ushuru pasipo kuwasiliana na wahusika na hivyo kuleta mzozo juu ya kiwango hicho kikubwa cha tozo la ushuru.
"Hatutaweza kukubali kupanda kwa bei kubwa kiwango hiki kutoka tozo la shilingi laki moja hadi shilingi milioni moja, tena pasipo mkurugenzi kutupa taarifa ila tunaona ameweka matangazo kwenye mbao za matangazo wakati hatujapewa nafasi ya kuzungumzia ongezeko hilo, hili ni jambo la ajabu sana," Alisema Lutevele.
Edson Kihongole alisema kumekuwa na uchepushaji wa ushuru huo, kwani asilimia kubwa baada ya kukamatwa na kukosa kiwango kinachotakiwa kulipia, watozaji wa ushuru wamekuwa wakichukua hela ndogo ambayo haitolewi stakabadhi.
"Huu ushuru ni maslahi ya watu binafsi, kwa sababu mimi kuna siku walinitaka nilipe shilingi laki mbili na nilipowaambia sina walinitaka nitoe shilingi elfu ishirini na kwakuwa nilikuwa ninaharaka niliwapa na sikupewa risiti, kwa hiyo hapa tutambue kuwa ushuru huu unaokomaliwa ni maslahi binafsi sio unaingia katika mfuko wa serikali," Alisema Kihongole.
Henry Lukambika alisema hatua ya halmashauri hiyo kupandisha ushuru wa mbao utawakwamisha wafanyabiashara hao, kwani wengi wanaweza kuondoka katika msitu huo na kufanyia shughuli zao katika maeneo mengine nje ya Halmashauri ya Mufindi na hivyo Halmashauri hiyo kupoteza mapato.
Aidha wadau hao wa misitu walimtaka mwanasheria wa Halmashauri hiyo Ellah Msigwa kufafanua sheria ya tozo la ushuru huo mpya, kwa madai kuwa wanachofahamu ni ulipaji wa kodi wa asilimia sifuri hadi tano ambayo ni laki moja na nusu.
Msigwa alisema msitu wa Sao hill ambao ndiyo unazungumziwa unaingia katika kipengele "a" ambacho kinasema kodi hiyo inapaswa kulipwa kwani ni msitu unaovunwa niwa serikali na kuwa sheria hiyo ilikubaliwa tangu mwaka 2006.
Wambura Mbwana aliutaka uongozi wa Halmashauri hiyo kuajili watumishi walio na ufahamu juu ya masuala ya sheria, kwani sheria hiyo imepindishwa kwa maslahi ya wachache na hivyo kusababisha mgomo huo ambao umeiingizia hasara pia serikali baada ya wao wafanyabiashara kushindwa kusafirisha bidhaa hiyo ya mbao.
Anyelwise Mahenge alisema katika Halmashauri hiyo kuna magari zaidi ya 50 yanayopakia kila siku mbao, na kila gari hutozwa ushuru wa shilingi lakimoja na nusu, huku kila mwezi Halmashauri ikiingiza zaidi ya shilingi Milioni 54, na kuwa ongezeko hilo halina sababu ya kukuza uchumi kwani fedha ambayo imekuwa ikikusanywa ni nyingi kama inaingia moja kwa moja katika mfuko wa serikali.
"Hoja kuu hapa nikurudi katika ushuru wa awali, kwani huu hatufahamu umetokea wapi na umekubaliwa na nani kama hata uongozi wetu hauna taarifa za kupanda ushuru huu, tunahitaji ulipiaji uwe niwa mti na siyo kwa ubao mmoja kwa hiyo asilimia 5," Alisema.
Walisema kumekuwa na tabia ya rushwa katika maeneo ya vizuizi vya ulipaji wa ushuru wa bidhaa za misitu, na kuwa vizuizi hivyo visiwe kwa ajili ya kuwabana wavunaji.
Mwanasheria wa wadau wa misitu Gabrial Malangalila alisema sheria inazungumzia bei ya kununulia zao husika nasiyo zao litokanalo na mstu, na kuwa ushuru ulipiwe kwa zao la miti na si mbao ambayo inatokana na zao hilo la misitu, kwa madai kuwa wanaokwenda kwenye msitu wa serikali hununua miti au magogo na si zao la kitu kilichotokana na mti, huku akisema kuwa wafanyabiashara hao wahapaswi kutozwa ushuru wa mbao.
"Nitatafsiri kutokana na maneno yaliyopo kwenye sheria, ninaamini wanaokwenda kwenye misitu ya serikali huwa wanakwenda kununua Miti au Magogo, hawaendi kununua zao linalotokana na kitu kilichonunuliwa, kwa hiyo kinachotakiwa kutozwa ni kile kilichonunuliwa na siyo zao la kile kilichonunuliwa, ninamaa ya kuwa mbao haiingii katika tozo hilo," Alisema Malangalila.
Mtafiti na ofisa uchumi misitu Stephano Kingazi alisema wamekuwa wakipingana na uuzwaji na ununuzi wa bidhaa kwa ujazo, wakiwahimiza wafanyabiashara kutumia zaidi vipimo, na kuwa Halmashauri hiyo kutoza zao la Mbao kwa ujazo wa mzigo katika magari ni kuendelea kubaliki ukiukwaji wa taratibu za mizani zinazotaka bidhaa zote ziuzwe kwa vipimo.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Ntiwika Willium Paul alikili kuwepo kwa baadhi ya mapungufu kwa baadhi ya hatua, na kusema kuwa wafanyabiashara hao ni wadau wa maendeleo katika Wilaya hiyo, na tatizo hilo litafikiwa muafaka, huku akiwaomba wadau hao kushirikiana katika kutoa taarifa za uvunjifu wa sheria ikiwa pamoja na uwepo wa tabia za rushwa kwa baadhi ya watumishi wake.
"Hapa tunaangalia pande zote, upande wa kwetu sisi wasimamizi wa sheria, hasa mimi mkurugenzi mtendaji, kwa hiyo sisi wataalamu pamoja na nyinyi tupo hapa kuzungumza ili tufikie muafaka, kwani Halmashauri hii ya Mufindi inajengwa na watu ambao ni walipaji wa kodi na si wengine ni nyinyi," Alisema.
Hata hivyo baada ya malumbano ya muda wa zaidi ya masaa manne pasipo kufikiwa muafaka, wafanyabiashara hao kupitia mwenyekiti wa wavunaji, wanunuzi na wasafirishaji wa mbao Christian Ahia alitoa taarifa ya hatua zaidi juu ya mgongano huo, na kusema wamefungua kesi Mahakamani na hakuna haja ya kuendeleza mjadala wa suala hilo.
"Ndugu zangu hapa nimepokea ORDER ya mahakama kutoka kwa mwanasheria wetu, kwa hiyo kinachofuata ni kuwa tayari tumefungua kesi mahakamani na hakuna haya ya kuendelea na mjadala wa jambo hili," Alisema Ahia.
MWISHO
No comments:
Post a Comment