"Lazima tupinge vitendo hivi vya unyanyasaji na ukatili wa kijinsia kwa mtoto wa kike," Wakiimba
Wanachama wa Clab ya TUSEME wakiwa katika maandamano, katika viwanja vya shule ya sekondari JJ Mungai Mufindi mkoani Iringa.
SHIRIKA la Forum For Africa Women Educationalists (FAWE) kwa ufadhiri wa UNICEF linalojihusisha na utoaji wa huduma za kielimu kwa mtoto wa kike, chini ya mradi wa TUSEME ambao huwawezesha wanafunzi wa shule za msingi na sekondari kujitambua, kujiamini, kujithamini na kuzitete haki zao, limewakutanisha wanafunzi wa Wilaya tisa nchini, ili kubaini changamoto zinazowakabiri.
Akizungumza katika sherehe ya uzinduzi wa kambi ya wanafunzi hao, kambi iliyopo katika shule ya sekondari JJ Mungai katika Wilaya ya Mufindi mkoni Iringa, mratibu wa FAWE Tanzania Bi. Neema Kitundu amesema Wilaya zilizoshiriki katika kambi hiyo ni Temeke, Njombe, Mtwara na Mbeya Vijijini.
Bi. Kitundu amesema Wilaya nyingine ni Mufindi, Iringa vijijini pamoja na Makete, huku Wilaya mbili ya Magu na Mbarali ya mkoni Mbeya, zikishindwa kuwaleta wanafunzi wake kuhudhuria shughuli hiyo.
Aidha Bi. Kitundu amesema shirika la FAWE ambalo lilianzishwa nchini Tanzania mwaka 1996 likiwa na lengo kuu la kuijengea uelewa jamii juu ya haki ya elimu kwa mtoto wa kike.
Amesema shirika hilo barani Afrika mnamo mwaka 1992, humuhamasisha mtoto wa kike aweze kupata elimu bora bila kukwamishwa na vizingiti vyovyote, kwa kumpa uthubutu wa kuchagua masomo ya Sayansi ili waweze kuingia katika taaluma mbalimbali kwa usawa baina yake na mtoto wa kiume.
Amesema shirika la FAWE limekuwa na afua kama TUSEME ambazo zinalenga kuboresha vituo vinavyotoa elimu kwa kujenga majengo yanayowezesha upatikanaji wa elimu bora, ambapo huyaweka mazingira rafiki ya elimu kwa jinsia zote.
“FAWE kupitia afua ya TUSEME tumekuwa tukiboreshaji mazingira ya elimu, kwa kujenga majengo yanayoiunga mkono elimu, mfano kama hapa tulipo shule ya sekondari JJ Mungai, tumeweza kujenga Maktaba bora naya kisasa, na pia tumejenga hili jengo la kulia Chakula (Dinning Hall), hiyo yote ni katika kuifanya elimu itolewe katika mazingira sahihi na bora zaidi,” Alisema Kitundu.
Mwanzirishi wa TUSEME nchini Profesa Penina Mlama amesema tangu kuanzishwa kwa mradi huo mwaka 1996 kumekuwa na mafanikio makubwa, kwa kuzifikia nchi 25 barani Afrika, ikiwa pamoja na mtoto wa kike nawa kiume kutambua haki stahiki dhidi yao.
Proffesa Mlama amesema akiwa chuo kikuu cha Dar es salaam yeye na mwenzie Amandina Lihamba walianzisha mpango huo kwa lengo la kuondoa mfumo dume katika jamii, ambao umekuwa ukimkandamiza zaidi mtoto wa kike, kwa kumbana katika haki ya elimu.
Amesema licha ya TUSEME kumpa uwezo mtoto wa kike ili aweze kutambua changamoto zinazomkabili na kuzitete mwenyewe, pia wanawajengea uelewa watoto wa kiume kuacha tabia ya wao kujiona ni bora zaidi kuliko kike, na lengo likiwa ni kuleta usawa kuanzia ngazi ya familia, jamiii na Taifa kwa ujumla.
Kaimu afisa elimu mkoa wa Iringa Mwalimu Ezekiel Kiagho ambaye ndiye alikuwa mgeni rasmi wa hafla hiyo, amesema shirika hilo ni chachu katika sekta ya elimu, kutokana na ukweli kuwa baadhi ya wazazi na walezi wamekuwa wakiwabagua watoto wa kike katika afua ya elimu.
Kiagho amesema kutokana na elimu inayotolewa na FAWE kupitia mradi wa TUSEME jamii imepata uelewa dhidi ya haki sawa baina ya mtoto wa kike nawa kiume kwa kuona umuhimu wa kuwapeleka watoto wote shule.
Hata hivyo watoto washiriki waliopo katika kambi hiyo, Erick Kisima, Irene Nyavanga wanafunzi kutoka Wilaya ya Mufindi na Jennifer Steven Luvanda kutoka Wilaya ya Makete wamesema bado baadhi ya wazazi na walezi wanaendeleza ubaguzi kwa watoto wa kike katika suala zima la elimu, huku mtoto huyo akibebeshwa zigo la majukumu ya kazi za nyumbani.
“Wazazi tukifika nyumbani, sisi watoto wa kike ndiyo tumekuwa tukifanyishwa kazi nyingi, tofauti na wenzetu watoto wa kiume, hii inachangia kukosa muda wa kutosha kujisomea, tunawaomba wazazi na walezi wetu watugawie majukumu ya kazi za nyumbani kwa usawa ili kutupunguzia mzigo wa kazi,” Alisema Jennifer na Irene Nyavanga.
Erick Kisima amesema pia hata baadhi ya familia zenye uwezo kifedha nazo zimekuwa zikiwakatisha masomo watoto wa kike, kwa tamaa ya kupata mali kwa kuwaozesha, na wengine wakishindwa kuwaendeleza katika elimu ya sekondari kwa imani potofu ya kuwa “Mtoto wa kike niwa kuolewa tu”.
MWISHO
No comments:
Post a Comment