ASKARI wawili wa Jeshi la
Polisi pamoja na Katibu wa Ofisi ya Mwanasheria wa Serikali mkoani
Iringa,wamepandishwa kizimbani baada ya kukamatwa na Taasisi ya Kuzuia na
Kupambana na Rushwa (Takukuru) wakikabiliwa na tuhuma za kuomba rushwa ya sh.
milioni Sita ili wawasaidie watuhumiwa wa pembe za ndovu.
Watuhumiwa hao wamefikishwa
leo mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Iringa, Consolatha Singano kujibu
tuhuma hizo za kuomba rushwa ya sh. mil. sita kutoka kwa washitakiwa
watatu wa nyara za serikali, Patrick, Raymond na Hamisi ambao
wanakabiliwa na kesi ya kukutwa na pembe za ndovu kinyume cha sheria.
Mwendesha Mashtaka wa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) , Imani Nitume, akisoma
jalada la kesi hiyo namba 306 ya mwaka 2012 lenye mashitaka saba, amesema kuwa
watuhumiwa hao walitenda kosa hilo kinyume na kifungu cha sheria namba 15 (1)
(a).
Alidai mahakamani hapo
kuwa askari polisi mwenye namba G. 402 D/C Denis Beatus (32) na Joshua Bratus Mkwama
(37), na Katibu wa Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Iringa,
wanakabiliwa na shitaka la kwanza la kuomba rushwa ya shilingi milioni sita.
Nitume alisema Denis
Beatus anakabiliwa na shitaka la pili la kupokea rushwa mnamo Desemba 12 mwaka
huu kutoka kwa Diska Kshinde Gadama ili kuwasaidia ndugu zake wapate dhamana
katika kesi ya kukutwa na nyaraka za serikali kinyume cha sheria.
Aidha Nitume amesema
pia Katibu wa Sheria Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, anakabiliwa na
shitaka la tatu la kupokea rushwa ya silingi milioni tatu kutoka kwa Joshua
Mkwama katika ofisi ya mwanasheria Desemba 16 mwaka huu.
Mtuhumiwa mwingine,
mwenye namba F 3277 D/C Karume Farijala Kunga (32) ambaye ni askari katika
ofisi ya Mkuu wa Upelelezi mkoa wa Iringa (RCO), anakabiliwa na shitaka la nne
la kupokea rushwa ya laki tano kutoka kwa Denis Beatus.
Diska Kashinde Gandama
mkazi wa Kigamboni Jijini Dar es salaam ambaye ni ndugu wa
washitakiwa watatu wanaokabiliwa na kesi ya kukutwa na nyaraka za serikali
kinyume cha sheria yeye anakabiliwa na shitaka la tano la kutoa rushwa katika
kituo kikuu cha mabasi mkoa wa Iringa na kumpa Denis Beatus, kinyume cha sheria
kifungu cha 15 (1) (b).
Shitaka la sita
linamkabili Denis Beatus na Kashinde Gandama ambao wanadaiwa kutoa
rushwa ya sh. 3,000,000 na kumpa Joshua Mkama ambaye ni Katibu wa Sheria Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu ili kuwasaidia Patrick na wenzake katika kesi
inayowakabili.
Katika shitaka la
saba, Mwanasheria huyo wa Takukuru amedai kuwa, katika ofisi ya RCO, Denis Beatus
alimkabidhi Karume Farijala rushwa ya shilingi laki tano ili kuhujumu kesi
dhidi ya nyaraka za serikali inayowakabili watu watatu.
Watuhumiwa wote wamekana
mashitaka yanayowakabili na mahakama imeahirisha shauri hilo hadi Januari 15
mwaka 2013, huku wakili Alfred Kingwe anayewatetea watuhumiwa hao,
akiiomba mahakama hiyo kutoa dhamana kwa wateja wake kwa kuwa mashitaka
yanayowakabili yanadhaminika.
Hata hivyo
Hakimu Singano alikubali ombi la wakili Kingwe na kutoa masharti ya
dhamana ambapo kila mshitakiwa alipaswa kuwa na wadhamini wawili wenye uwezo wa
kusaini dhamana ya sh. Mil. 2 na mmoja kati yao awe mwajiriwa wa serikali, huku
mahakama hiyo ikizuia hati za kusafiria za washitakiwa hao.
MWISHO
No comments:
Post a Comment