Sunday, February 24, 2013

WALIOPATA MATOKEO MABAYA KIDATO CHA NNE WAISHAURI SERIKALI


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Mh. Jesca Msambatavangu, ambaye pia ni diwani wa Kata ya Miyomboni/ Kitanzini, akitoa nasaha kwa wanafunzi wa kidato cha nne ambao matokeo yao ya mitihani hayakuwa mazuri, huku akiwasihi kuacha kukata tamaa.
Bi. Baby Baraka Chuma, Mkurugenzi wa kozi fupi na masomo endelevu katika chuo kikuu cha Ruaha (RUCO) Mkoani Iringa, akisikiliza maoni ya wanafunzi hao (Hawapo pichani) 
 Wanafunzio hao wakisikiliza kwa umakini mawazo mbadala baada ya kufeli mtihani wa kidato cha nne.

 Wanafunzi hao wakiwa katika ukumbi wa Chuo kikuu cha Ruaha (RUCO) mkoani Iringa.
 Mh. Jesca Msambatavangu (Katikati) akisisitiza jambo kwa wanafunzi hao, ambapo cha msingi amewataka vijana hao kutokata tamaa katika elimu, kwa matokeo hayo ya kidato cha nne, kulia ni Bi. Baby Baraka Chuma.

 Mwanafunzi akiwaza jambo, katika ukumbi huo wa chuo kikuu cha Ruaha (RUCO).
 Wanafunzi wakiwa katika viwanja vya chuo kikuu cha RUCO mkoani Iringa.


HATIMAYE wanafunzi wa kidato cha nne waliopata matokeo mabaya ya mtihani wa Taifa, wa mwaka 2012 wamekutana kujadili mustakabari mzima wa nini kifanyike dhidi yao, ili kuokoa ndoto zao ambazo zinadalili  ya kuzima ghafla, wakati wengine wakichukua uamuzi batili.

Mpango huu ambao umeratibiwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa,Bi- Jesca Msambatavangu, na kufanyika katika chuo kikuu cha Ruaha-Ruco, lengo likiwa ni kusikiliza vilio na simanzi za wanafunzi hao, ili kuwaonyesha njia mbadala ya kufanya baada ya kupata matokeo hayo.

Wanafunzi hao ambao wameonyesha nia ya uendelea na masomo, licha ya kuwa katika sintofahamu ya kile kilichofanya matokeo yao kuwa mabaya, wamehudhuria mkutano huo kwa wingi, huku wakiitaka serikali itambue kuwa yenyewe ndiyo chanzo cha kuua ndoto zao za maisha.

Gerlady Kiyeyeu aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya St. Michael ya Wilayani Kilolo amesema serikali inatakiwa kufanya jitihada dhidi yao, ili kutopoteza ndoto za kundi kubwa hilo la watanzania ambao ndiyo Taifa la baadaye, huku akiitaka  serikali kuacha kuendeleza mgogolo na walimu.

“Serikali yetu kwa matokeo haya inatakiwa, au irudie kusahihisha upya mitihani yetu, au ituruhusu kurudia kidato cha nne pasipo na gharama ypyote, la sivyo itambue kuwa inatupoteza kimsingi watanzania, na kuvunja mioyo ya wazazi wetu, ambao kwa kiwango kikubwa wana hali duni,” Amesema Gerlady.

Naye Upendo Vitus aliyekuwa mwanafunzi wa sekondari ya Tagamenda katika manispaa ya Iringa, amesema matokeo hayo kwa kiwango kikubwa hana uhakika kama ni hyao, kwani mtihani waliofanya ulikuwa wa kawaida na walikuwa na uhakika mkubwa wa kufaulu.

“Kuna baadhi yetu tulianza kufanya Tution ya kujiandaa na masomo ya kidato cha tano, lakini tumeshtushwa sana na matokeo haya, mimi ninaiomba serikali iondoe gharama za kulipia mtihani kwa sisi wote tunaorudia, ili kutupa nafasi wote, tuweze kurisit,” Amesema Upendo.

Naye Raphaely Mahenge, aliyekuwa mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Iwawa Makete mkoni Njombe, amesema hali duni ya wazazi wake itamfanya ashindwe kuendelea na masomo, kwani tangu aanze kupata akili amekuwa akimuona mama yake  akifanya biashara ya kuuza Makande.

“Mimi niseme mama yangu ni mtu mwenye hali duni, sidhani kama nina uhakika wa kujiendeleza katika shule binafsi na vituo hivi vya QT, kama shilingi elfu 20 alikuwa akilipa kwa awamu na kwa kusuasua, kutokana na biashara yake duni ya Kande, atawezaje leo hii kunilipia ada ya kurisiti mtihani katika vituo binafsi??, Amesema Raphaely.

Akizungumzia mpango huo, mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Bi. Jesca Msambatavangu, amesema lengo kuu ni kuwatia moyo vijana hao wasikate tama kutokana na matokeo hayo, na pia kuwapa njia mbadala ya kujiendeleza katika vyuo vinavyotoa mafunzo na kozi za muda mfupi, ili kuwa na sifa ya kujiunga na vyuo vikuu.

Bi. Msambatavangu amewataka pia wazazi kuacha jazba dhidi ya vijana wao, kwani hasira juu ya wanafunzi hao ndiyo sababu kuu inayochangia uwepo wa matukio ya kujiua.  

Naye Bi. Baby Baraka Chuma, mkurugenzi wa kozi fupi na masomo endelevu, kutoka chuo kikuu cha Ruaha(Ruco) amesema serikali iwaangalie kwa jicho la pili kwani wanafunzi hao hawajafeli kwa kushindwa kujiandaa na mitihani yao, bali waliwekeza licha ya kupata matokeo mbaya, na ndiyo sababu ya baadhi yao kuchukua maamuzi ya kujitoa uhai.

Aidha amesema kuna haja ya kujiuliza zaidi juu ya matokeo hayo na siyo kuwatupia lawama zisizo na maana wanafunzi hao, huku akisisitiza serikali kusikiliza maombi ya wanafunzi hao kurudia tena mtihani wa kidato cha nne pasipo na gharama.  

“Mimi nimepata picha baada ya kusikia mawazo ya hawa wanafunzi pamoja na matukio yaliyojitokeza ya kujinyonga, kwani mwanafunzi ambaye hakufanya vizuri kwa makusudi hawezi kuchukua uamuzi wowote akifeli, kwani anatambua wazi kuwa hakuonyesha jitihada zozote, watoto hawa inaelekea walijiandaa vizuri na ndiyo maana wanaonyesha jazba kwani kile walichokitaraji kimekuja tofauti” Amesema Baby.

Hata hivyo wazazi nao wameonywa kuacha jazba na tabia ya ukali kwa wanafunzi ambao wamepata matokeo mabaya, na kuwa huu ndiyo muda wa kuonyesha upendo dhidi ya watoto wao, kutokana na janga walilolipata.

“Hakuna haja ya kuwa mbogo kwa mtoto katika kipindi hiki kigumu, hapo ndiyo unaweza kumsababishia matatizo mengine makubwa kama haya tunayoyasiki ya kujinyonga, huu ni wakati mgumu kwa watoto hawa, na mzazi ndiyo anatakiwa kuonyesha upendo wake wa dhati kwa kijana wake,”.

Hatua ya kukaa na wanafunzi hao, ni mbinu mbada na sahihi ya kupata mawazo kutoka kwa walengwa, juu ya nini kimefanyika, kuna haja ya masuala kama haya yenye maslahi kwa Taifa ukafanyika uamuzi kama huu ambao umefanywa na Mh. Jesca Msambatavangu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, ambaye pia ni diwani wa Kata ya Miyomboni Kitanzini.

MWISHO

No comments:

Post a Comment