Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake tanzania (UWT) MKoa w Iringa Bi. Zainabu Mwamwindi (wa pili kulia) akiwa katika uzinduzi wa mafunzo elekezi ya ujasiriamali kwa wajumbe wa jumuiya ya UWT Kanda ya Mlandege mkoani Iringa
Wanachama wa jumuiya ya wanawake Tanzania, wa kanda ya Mlandege wakiwa katika uzinduzi wa mafunzo elekezi ya ujasiriamali, mkoani Iringa.
HATIMAYE chama cha Mapinduzi CCM, kimetangaza kupunguza madaraka kwa wale wote waliojilimbikizia uongozi, kwa madai ya kuwa hatua hiyo inawanyima fulsa za kuongoza wanachama wengine.
Huo ni mkakati wa kukijenga chama na kuwafanya wajumbe wengi kushika nyadhfa mbalimbalia za uongozi katika mkoa wa Iringa.
Akielezea mpango huo katika mafunzo elekezi ya Umoja wa Wanawake, mwenyekiti wa UWT mkoa wa Iringa, Zainabu Mwamwindi alisema hatua hiyo ya mgawanyo wa madaraka itasaidia kupunguza ukiritimba wa kukumbatia vyeo vingi.
Mwamwindi alisema viongozi wengi ndani ya umoja huo wamekuwa na vyeo vingi na hivyo kujikuta baadhi yao wakishindwa kutimiza wajibu wao na hivyo shughuli nyingi kukwama.
“Hakuna sababu ya mwanachama moja kuwa na madaraka mengi wakati katika jumuiya hii wapo wajumbe na wanachama wengi amabo hawana wadhfa wowote wa uongozi, imefika wakati kila mwanachama akaona anao mchango wake wa mawazo kwa kupatiwa fulsa ya uongozi,” Alisema Mwanmwindi.
Alisema wajumbe wa UWT wanatakiwa kutambua jumuiya hiyo kuwa ni mali yao, na kila mmoja anayosifa ya kuwa kiongozi wa umoja huo kuanzia ngazi ya matawi hadi Taifa.
“Ninawaombeni sana ndugu zangu, hii jumuiya muione ni mali yenu, tatizo hili tumeliona, katika kata na matawi yetu hakuna chochote kinachoendelea, hii jumuiya ni kimbilio lenu wote wanawake, na mnayo sifa ya kujivunia kwa kuona nanyi ni wanajumuiya na mnayo haki ya kuwa viongozi ili kuiboresha na kuiendesha jumuiya hii,” Alisema.
Alisema UWT imeliona tatizo hilo la mtu mmoja kulimbikiziwa uongozi akawa na kofia nyingi, na kuwa wametambua uwakirishi unakuwa mdogo katika majukumu mbalimbali kutokana na madaraka hayo kukumbatiwa na wachache na sasa wamekusudia kuondoa ukiritimba huo.
Naye Nataria Magohagasenga mjumbe wa UWT alisema hatua hiyo itasaidia kukijenga chama, kwani baadhi ya wanachama walikuwa wakikwepa majukumu mbalimbali kwa walijiona kama hawastahili kuwa viongozi kutokana na viongozi wachache kumiliki madaraka mengi.
“Huu ni uongozi uliopitwa na wakati, wanachama wengi tunao uwezo wa kuongoza, hata sisi tulikuwa tunachoshwa na mfumo uliokuwepo, unakuta mtu mmoja anajitambulisha vyeo zaidi ya vitano, wakati kuna wanachama hawana hata wadhfa mmoja, hili lilikuwa tatizoi kweli,” Alisema Magohagasenga.
Aidha alisema upunguzaji wa madaraka utaongeza imani kwa wanachama na kueneza mtandao wa shughuli mbalimbali zinazofanywa na chama tofauti na sasa ambapo wanaofahamu mazuri yanayofanywa na chama ni wachache.
Aidha alisema hata watu wa chini wapewe uongozi, kwani wanayo mawazo mazuri na uwezo mkubwa wa kuongoza na kukipeleka chama mahala pazuri, kwani tukiwa wajumbe wengi tunapeleka sauti kwa wengi.
Alisema hata wazee wanatakiwa kupewa nafasi ya kusikilizwa kwani wanayo mawazo mazuri lakini wamekuwa wanashindwa kuyatoa kutokana na kunyimwa fulsa hizo kwa kutoshirikishwa katika masuala mbalimbali ya chama.
Akizungumzia malengo ya mafunzo hayo mjumbe wa kamati ya uchumi na fedha UWT mkoa wa Iringa ambaye pia ni diwani viti maalumu kanda ya Mlandege Dora Nziku alisema, elimu hiyo itawasaidia wanawake kuwanoa na kuwapatia weledi wa uongozi.
Alisema semina hiyo elekezi imelenga kutoana elimu ya ufanyaji wa shughuli za kichama, na kuwa baadhi yao itawasaidia kujiamini na kuingia katika vinyang’anyiro mbalimbali vya uongozi katika chama.
Dora alisema mpango huo umelenga pia kuwapa elimu ya ujasiliamali wanawake wa jumuiya hiyo, ili kuachana na tabia ya kuwa tegemezi kwa waume wao, kwani sasa wanawake wanatakiwa kuchangia uchumi katika familia zao.
“Kwenye jumuiya tumetambua kuwa kuna idadi kubwa ya wanawake wasio na kipato cha fedha, hali hiyo inawafanya wawe wanyonge na tegemezi, na hivyo kushindwa kusikilizwa na waume zao, lakini mafunzo ya ujasiriamali yatawawezesha kujitegemea na kujenga upendo katika ndoa zao, na hata kusikilizwa,” Alisema Dora Nziku.
No comments:
Post a Comment